Marekani, Uingereza zatilia shaka 'haki za raia kisheria' Tanzania

Erick Kabendera mahakamani
Image caption Tamko la Marekani na Uingereza linagusia kesi ya Erick Kabendera kama mfano wa hivi karibuni

Ubalozi wa Uingereza na Marekani nchini Tanzania wametoa tamko la pamoja kuhusu kile walichokiita "wasiwasi wa kuzorota kwa kwa haki za kisheria nchini Tanzania."

Katika tamko hilo, ofisi hizo mbili za ubalozi zinadai kuwa imedhihirika kwa zaidi ya mara moja watu kutiwa kizuizini kwa muda nchini Tanzania bila kupelekwa mahakamani na kubadilishiwa mashitaka na mamlaka zake za kisheria.

"Tuna wasiwasi hasa kwa tukio la hivi karibuni -- jinsi ambavyo halikushughulikiwa kwa haki la kukamatwa, kuwekwa kizuizini na tuhuma za mashtaka ya mwandishi wa habari za uchunguzi Bw Erick Kabendera, ikizingatiwa ukweli kwamba alinyimwa haki ya kuwa na mwanasheria kwenye hatua za awali na kutiwa kizuizini kwake, ambapo ni kinyume cha sheria ya makosa ya jinai," inasema sehemu ya tamko hilo.

"Tunaisihi serikali ya Tanzania kutoa hakikisho la mchakato wa kutenda haki kisheria kwa raia wake, kama ilivyotambua kwamba ni haki ya msingi na kuridhia kwenye mikataba mbali mbali ya haki za kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa, miongoni mwao ikiwemo azimio la kimataifa la haki za kirai na kisiasa."

Erick Kabendera alipandishwa kizimbani Jumatatu ya wiki hii ikiwa ni wiki moja toka alipokamatwa na vyombo vya usalama nchini Tanzania.

Haki miliki ya picha US EMBASSY TANZANIA/Facebook

Mwanahabari huyo meshtakiwa kwa makosa matatu ya ubadhirifu wa kiuchumi. Mosi anashtakiwa kwa kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi, pili kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za Kitanzania na tatu utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.

Kumekuwa na wasiwasi ndani na nje ya Tanzania kuhusu namna ambavyo amekamatwa, na taswira inayotokana na hatua hiyo kwa uhuru wa yombo vya habari nchini humo.

Pia baadhi ya wanaharakati wameonyesha kushangazwa na kubadilika kwa yaliominika kuwa ndio makosa anayotuhumiwa nayo.

Awali maafisa wa polisi na wale wa idara ya uhamiaji walisema anachunguzwa kuhusu utata wa uraia wake.

Baadae mawakili wake walitoa taarifa wakieleza mteja wao atashtakiwa kwa kuhusika na ripoti iliyochapiswha katika jarida la The Economist, lakini mahakamani kibao kikageuka tena na kuwa kesi ya ubadhirifu wa kiuchumi.

Makosa aliyoshtakiwa nayo hayana dhamana na ataendelea kusalia rumande mpaka mwisho wa kesi yake. Agosti 19, kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa tena mahakamani.


Matukio yalivyojiri:

Julai 29:

Taarifa kuhusu kutoweka kwa Mwandishi wa habari za uchunguzi, Erick Kabendera zachipuka Tanzania.

Kulikuwa na utata wa awali kuhusu iwapo ametekewa na watu wasiojulikana kama ilivyo kwa baadhi ya visa vya kutoweka kwa watu Tanzamnia tangu 2015 na kutojulikana waliko hadi leo.

Kamati inayolinda waandishi wa habari barani Afrika (CPJ) kupitia ujumbe huu wa Twitter ilisema inachunguza taarifa ya kutoweka kwa mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania Erick Kabendera aliyechukuliwa kutoka nyumbani kwake na "watu wasiojulikana " na mahala aliko hakufahamaiki.

Hili lilizidi mshindo kutokana na taarifa kutoka kwa ndugu jamaa na marafiki zake walioeleza kuwa alichukuliwa kwa nguvu na watu kutoka kwake nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam eneo la Mbweni.

Julai 30:

Polisi nchini Tanzania yasema kuwa mwanahabari wa Erick Kabendera aliyedaiwa kutoweka - hakutekwa bali amekamatwa.

Kamanda wa polisi kanda maalum ya mji wa Dar Lazaro Mambossasa amesema polisi wanafanya uchunguzi kuhusu uraia wa mwandishi huyo kwa ushirikiano wa idara ya uhamiaji kabla ya kumwasilisha mahakamani.

Julai 31:

Siku mbili baadaye, Idara ya uhamiaji ilithibitisha kuwa inamshikilia Kabendera kutokana na kuwa na mashaka na uraia wake, kamishna wa uraia na mdhibiti wa pasi Gerald Kihinga amethibitisha.

Idara ya uhamiaji imesema kama chombo kilichopewa dhamana ya kusimamia na kutekeleza sheria ya uraia ya Tanzania, inayo mamlaka ya kuchunguza na kuthibitisha uraia wa mtu yeyote anayetiliwa mashaka baada ya kupokea taarifa kutoka katika vyanzo mbalimbali.

Idara ya uhamiaji ilipata taarifa kutoka kwa wasamaria wema kuhusu utata wa uraia wa Bwana Erick Kabendera.

''Baada ya idara kupata taarifa hizo ilianzakuzifanyia kazi.Hata hivyo, Bwana Kabendera mwenyewe hajawahi kuhojiwa kuhusu uraia wake, kwa kuwa hakufika ofisini pamoja na kutumiwa wito mara kadhaa wa kumtaka kufika ofisini kwa mahojiano'' Ilieleza taarifa ya Idara ya uhamiaji.

Julai 31:

Mke wa mwandishi Erick Kabendera aliruhusiwa kumuona mume wake Erick Kabendera siku mbili baada ya kamatwa na jeshi la Polisi siku ya Jumatatu jioni nyumbani kwake Mbweni jijini Dar es Salaaam.

Polisi walimsindikiza Kabendera nyumbani kwake kwa ajili ya kupata nyaraka za uthibitisho wa uraia wake.

Agosti 3:

Mama wa mwanahabari Eric Kabendera, Verdiana Mujwahuzi, 80 amezungumza na wanahabari kwa mara ya kwanza tangu mwanawe akamatwe.

Amepinga kauli ya polisi kuhusu uraia wa mwanawe.

''Kabendera ni mwanangu, nilimzaa hapa Tanzania na hapajawahi kuwa na utata kuhusu anakotoka, polisi iseme ukweli inamshikilia kwa nini'' aliliambia Gazeti la The Citizen nchini Tanzania.

Gazeti la Citizen liliripoti kuwa Siku ya Jumatano Mama Mujwahuzi alihojiwa na watu kumi amabo alifahamishwa baadae ni maafisa wa uhamiaji waliotaka kuthibitisha uraia wa mwanawe.

Mada zinazohusiana