Dawa za kupambana na Ebola zaonyesha ufanisi mkubwa DRC

Mtoa huduma za afya akimchoma sindano ya chanjo mtoto nchini DRC Haki miliki ya picha Reuters

Ugonjwa wa Ebola huenda punde ''ukadhibitiwa na kutibika'' baada ya majaribio ya dawa aina mbili zilizoonesha ufanisi.Wanasayansi wameeleza.

Dawa aina nne zilijaribiwa kwa wagonjwa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako kuna mlipuko mkubwa wa virusi hivyo.

Dawa aina mbili kati ya nne zimeonekana kufanya kazi vilivyo katika kutibu ugonjwa, utafiti umeeleza.

Dawa hizo sasa zitatumika kutibu wagonjwa wote wa Ebola nchini DR Congo, kwa mujibu wa maafisa wa afya wa nchi hiyo.

Taasisi ya taifa ya utafiti kuhusu uzio na maradhi ya kuambukiza ya nchini Marekani (NIAID), ambao ilidhamini majaribio hayo, imesema matokeo hayo ni ''habari njema'' katika mapambano dhidi ya Ebola.

Dawa hizo kwa jina REGN-EB3 na mAb114, zinafanya kazi ya kuvishambulia virusi vya Ebola kwa kuzipa nguvu chembe chembe za kinga za mwili zinazopambana na maradhi.

Ni ''dawa za kwanza, ambazo kisayansi zimeonesha kuwa muhimu katika kupunguza vifo'' vya wagonjwa wa Ebola, alisema Daktari, Anthony Fauci, Mkurugenzi wa NIAID.

Dawa nyingine aina mbili ZMapp na Remdesivir, zilishindwa kufanya vizuri kwenye majaribio hayo.

Matokeo ya majaribio yalikuwaje?

Majaribo, yaliyofanywa na taasisi ya utafiti na kuratibiwa na Shirika la afya duniani, WHO, yalianza mwezi Novemba mwaka jana.

Tangu wakati huo, dawa aina nne zilijaribiwa kwa wagonjwa 700, huku matokeo ya awali kutoka kwa watu 499 wa kwanza yakifahamika hivi sasa.

Haki miliki ya picha Reuters

Kwa wagonjwa waliopewa dawa aina mbili zilizoonyesha kufanya kazi, 29% waliopewa dawa aina ya REGN-EB3 walipoteza maisha na 34% waliopewa dawa aina ya mAb114 walipoteza maisha, NIAID ilieleza.

Tofauti na, 49% ya waliopewa dawa ya ZMapp na 53% waliopewa dawa aina ya Remdesivir walipoteza maisha taasisi hiyo ilieleza.

Matokeo yanamaanisha kuwa mamlaka za afya zinaweza ''kusisitiza watu kuwa zaidi ya asilimia 90 ya watu wanaweza kupona'' ikiwa watapata matibabu mapema, alisema Sabue Mulangu, mtafiti wa magonjwa ya kuambukiza.

Dawa hizi zimekuwa na faida gani?

Akisifu mafanikio ya utafiti, Jeremy Farrar, mkurugenzi wa mfuko wa msaada wa masuala ya huduma za kiafya Wellcome Trust, amesema ''bila shaka dawa hizo zinaokoa maisha''.

Matokeo, Bwana Farrar alisema yanaonesha kuwa wanasayansi wako mbioni kuufanya ugonjwa wa Ebola ''kuzuilika na kutibika''

''Hatuwezi kutokomeza ugonjwa wa Ebola kabisa, lakini tuwe na uwezo wa kuzuia ugonjwa huu kuwa mkubwa katika taifa na ukanda,'' aliongeza.

Kisa cha pili cha Ebola chathibitishwa mpakani mwa DRC

Ugonjwa wa Ebola wathibitishwa mjini Goma, Congo

Hisia kuwa Ebola haitibiki, halikadhalika hali ya kutoaminiwa kwa watoa huduma za afya chini DR Congo, kumeathiri juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa.

Kuna matumaini kuwa ufanisi wa dawa hizo zilizotengenezwa na makampuni ya kimarekani, zitafanya wagonjwa wajihisi ''kujiamini wanapotafuta huduma mapema'', alisema Daktari Fauci.

Lakini njia nzuri ya kumaliza mlipuko huo, aliongea, ni ''kwa kupata chanjo inayofaa''. Chanjo ni aina ya dawa inayoboresha kinga.

Mlipuko huo uko na athari kiasi gani?

Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola mashariki mwa DRC ulianza mwezi Agosti mwaka jana na ni mkubwa kati ya 10 iliyowahi kukumba nchi hiyo tangu mwaka 1976, virusi vilipogundulika kwa mara ya kwanza.

Mwezi Julai, WHO ilitangaza Janga la Ebola kuwa la dharura duniani.

Ugonjwa huu pia uliathiri watu 28,616, hasa Guinea, Liberia na Sierra Leone. watu 11,310 walipoteza maisha kutokana na mlipuko mkubwa kabisa kuwahi kuripotiwa.

Haki miliki ya picha Reuters

Hatahivyo, majaribio ya kupambana na mlipuko wa sasa yamekuwa magumu, kwa ujumla kutokana na kuwepo kwa makundi ya wanamgambo na mashaka kuhusu msaada wa tiba kutoka nchi za kigeni.

Mwanzoni mwa mwezi huu, madaktari watatu wa Congo walikamatwa wakishutumiwa kwa mauaji ya daktari wa WHO.

Takribani vituo vya afya 200 vilishambuliwa nchini humo mwaka huu, na kusababisha kuwepo na mzozo kuhusu chanjo na tiba, Katika tukio moja familia ilimshawashambulia wafanyakazi wa afya ambao walikuwa wakiratibu maziko ya ndugu wa familia hiyo aliyepoteza maisha kutokana na Ebola.

Ebola ni nini?

Haki miliki ya picha BSIP/Getty Images

Ebola ni kirusi ambacho mwanzo husababisha joto la mwili na kudhoofisha misuli na uvimbe kooni.

Kisha mgojwa huanza kutapika, kuharisha na kuvuja damu ndani na hata nje ya mwili.

Watu huambukizwa wanapogusana moja kwa moja kupitia michubuko ya mwili, au mdomo na pua, huku damu, matapishi, kinyesi au kugusa majimaji ya mwili ya mgonjwawa Ebola

Wagonjwa huwa wanakufa kutokana na ukosefu wa maji mwilini na kuharibika kwa viungo vya ndani vya mwili.