Trump awageukia wahamiaji halali masikini

Trump

Uongozi wa Rais wa Marekani Donald Trump una mpango wa kuhakikisha unazidisha ugumu kwa wahamiaji masikini ambao wanatakiwa kuongezewa muda wa viza zao ama kupata kadi ya kudumu ya makazi (kadi ya kijani).

Mpango huo unawalenga wahamiaji ambao wanategemea misaada kama ya chakula na makazi kwa zaidi ya mwaka mzima.

Maombi yanaweza kukataliwa ikiwa serikali itaamua kuwa wanaweza kuwa mzigo wa kutegemea misaada katika miaka ijayo.

''Mabadiliko haya yatachangia kujikimu wenyewe na sio kuwa tegemezi'' maafisa walisema.

Utaratibu mpya unaojulikana kama ''namna ya kujitegemea'' ulichapishwa katika mpango wa serikali siku ya Jumatatu, na utaanza kufanya kazi tarehe 15 Oktoba.

Nani ataathirika?

Wahamiaji ambao tayari ni wakazi wa kudumu wa Marekani wao hawatoathiriwa sana na mpango huu.

Pia hauwahusu wakimbizi na wanaoomba hifadhi. Lakini wale wanaoomba kuongezewa muda wa viza zao pamoja na kadi ya kijani ama uraia wa Marekani waathiriwa na mabadiliko hayo.

Wale ambao hawajafikia kiwango cha kipato kinachotakiwa na wanaweza kuegemea kwenye huduma ya bure ya afya ama nyumba watatakiwa wasiingie nchini Marekani, na wale ambao tayari wapo nchini wanaweza wakakataliwa maombi yao ya kuongeza muda wa kuishi.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Wahamiaji ambao ni masikini na wanaotegemea msaada wa chakula wanalengwa na Trump

Inakadiriwa zaidi ya watu milioni 22 ni wakazi halali wa Marekani lakini hawana uraia na wengi wao wataathiriwa na mpango huu.

Wanaharakati wa haki za kiraia wamesema kuwa mpango huu unalengo la kuwafikia wahamiaji wa kipato cha chini. Kituo cha sheria cha wahamiaji (NILC) kimesema kuwa watamshitaki rais Donald Trump ili mpango huo usifanye kazi.

Lakini ikulu ya Marekani imesema kuwa mfumo huo unawasaidia wahamiaji wenye ndugu kuliko wale ambao wanaojitegemea wenyewe.

Mabadiliko yanayoendana na mipango ya Trump?

Na Anthony Zurcher, Ripota wa BBC Amerika Kaskazini

Ingawa malengo ya Donald Trump wakati wa Kampeni ya uraisi mwaka 2016 yalikua katika hatari ambayo aliiona ya wahamiaji ambao hawajasajiliwa, ni wazi kuwa, mpango wake wa muda mrefu ni kupunguza idadi ya wahamiaji , wote halali na wasio halali.

Tangu kuapishwa kwake, Rais Trump amepunguza idadi ya wakimbizi wanaoingia Marekani kila mwaka. Ikulu ya White House ililizuia bunge la seneti kupeleka muswada mwaka 2018 kwa sababu haukua na mabadiliko kwenye sheria ya wahamiaji halali.

Wakati wa makabiliano hayo, Trump aliripotiwa kutaja majina ya nchi mfano Norway ambapo wahamiaji wanatakiwa wapokelewe kuingia lakini sio kutoka ''nchi chafu.''

Kwa sasa mamlaka zinaweka ugumu kwa wahamiaji kuapta vibali vya kuishi Marekani, na wakati mwingine hadi kuingia nchini humo.

Kwanini mabadiliko yanafanyika hivi sasa?

Huwezi kusikiliza tena
Simulizi ya kushangaza ya wahamiaji wa jadi Marekani

Rais Trump amefanya suala la uhamiaji kuwa kipaumbele katika uongozi wake, mabadiliko haya ni sehemu ya jitihada za kupambana na suala la uhamiaji.

Ken Cuccinelli, kaimu mkurugenzi wa uraia katika kitengo cha uhamiaji alitangaza utaratibu huu siku ya Jumatatu.

Amesema kuwa, kiwango cha elimu, umri na hali ya kiuchumi vitazingatiwa wakati wa kutoa kitambulisho cha uraia.

''Waombaji wanaojua lugha ya kiingereza watazingatiwa,'' aliongeza.

Wiki iliyopita watu zaidi ya 680 walikamatwa wakishukiwa kuwa ni wahamiaji ambao wahajasajiliwa.

Picha za watoto wakilia zilisambaa mara baada ya kutenganishwa na wazazi wao. Maafisa wanasema kuwa wamehakikisha kuwa watoto wanapatiwa uangalizi mzuri.

Idadi ya wahamiaji wanaotaka kuingia Marekani kupitia mpaka wa Mexico imeongezeka huku idadi ya wahamiaji ambao hawajasajiliwa imepungua idadi yao, kwa mujibu wa kituo cha utafiti cha PEW.

Mwezi Mei, Rais Trump aliweka wazi kuwa mpango huu ni umewekwa ili kuvutia zaidi watu wenye ujuzi, umri mdogo na wanaozungumza lugha ya kiingereza.