Mpango wa Makonda kusajili ndoa Dar es Salaam waibua hisia Tanzania

Mkuu wa mkoa wa Dar Es Salaam, Paul Makonda Haki miliki ya picha PAUL MAKONDA

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nchini Tanzania, Paul Makonda mpango wa kuweka hadharani ndoa zilizosajiliwa katika mkoa huo liliibuka kutoka kwa wananchi wenyewe wakieleza changamoto zinazowakabili, na 'sio sheria za Makonda'.

Akizungumza na kipindi cha Dira ya dunia cha BBC, Mkuu huyo wa Mkoa huo amesema jambo hilo na anaamini kuwa ni hatua ambayo itakuwa mwarobaini wa changamoto za mahusiano katika jamii.

Kumekuwa na gumzo baada ya Makonda kutoa tangazo kuhusu mpango huo wa kuzisajili ndoa zote za mkoa huo kwa ajili ya kukabiliana na wanaume wanaowalaghai wanawake kimapenzi.

''Kama kiongozi unapata habari tofauti tofauti wananchi wakitoa mawazo yao,changamoto zilizopo na moja kati ya kazi tulizonazo ni kufikiri njia bora zaidi katika kutatua''.

Makonda amesema lengo lao ni moja tu, ni kutokuwepo kwa mtu kuingia kwenye makubaliano bila kuwa taarifa kuhusu mwenza wake.''

Haki miliki ya picha Google

''Hii inayoenda kukomeshwa katika mkoa wa wetu ambayo tunaifikiria ni namna ambavyo wanawake wanarubuniwa na watu wenye familia zao huku wakijua hawana mahusiano wakati hao watu wana mahusiano''.

Kwa mujibu wa Makonda, sheria ya Ndoa inampa mwanamke haki ya kwenda mahakamani na akalipwa fidia kutokana na hasara aliyoipata kwa ule muda aliopotezewa na mwanaume.

''Hii sheria ya ndoa imekuwepo siku zote sio sheria ya Makonda imetungwa na Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania ni suala la kuelimisha tu Umma kuhusu haki alizonazo mwanamke anapokuwa amerubuniwa na mwanaume''.Alisema.

''Watu ambao wanaingia kwenye hayo mahusiano wanajikuta wanapata watoto na mwisho wa siku Baba hata akifariki mtoto akipelekwa kwenye msiba hukataliwa na kufukuzwa kama mtoto asiyestahili hata kumuaga hata baba yake''.

Tangazo hilo limepokelewa kwa hisia tofauti na wakazi wa jiji hilo, wengine wakiunga mkono jitihada za mkuu huyo wa mkoa katika kupambana na walaghai wa mapenzi, lakini wengine wakiona kuwa hayo ni masuala ya binafsi sana huku wakiwa na mashaka kama mpango huo utafanikiwa.

Tangazo linasema nini?

Bwana Makonda alisema kuna mpango wa kuanzisha kanzi data ya ndoa zote zilizopo kwenye mkoa wake ili kupunguza utapeli wanaofanyiwa wanawake kwa kudanganywa kuolewa.

Kanzidata hiyo itahusisha usajili wa ndoa zote ili wanaume waliooa waweze kubainika na kuwanusuru wanawake wasitapeliwe na kuumizwa mioyo kwa kutegemea ndoa.

Makonda amesema pamoja na kanzidata hiyo atatumia mkutano wa SADC kupata uzoefu kutoka kwa nchi nyingine kufahamu namna gani wanakabiliana na utapeli wa aina hiyo.

Hii si mara ya kwaza kwa mkuu huyo wa mkoa wa Dar es Salam, kujaribu kusaidia kutatua matatizo yanayowakumba wanawake jijini Dar es Salaam.

Mwezi Aprili mwaka 2018, Makonda alitoa agizo kwa wanawake wanaodai kutelekezwa na wazazi wenzao kufika katika ofisi yake ili wapate kusikilizwa.

Na siku iliyofuata mamia ya watu waliotelekezwa na wenza wao walijitokeza katika viwanja vya Ofisi yake.

Hatua ambayo imekosolewa kuwa haikuzaa matunda.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii