Ubelgiji yachunguza 'utekaji' wa watoto walioasiliwa Ubelgiji kutoka DRC?

Suriya Muyombe akiwa ameshika picha ya mtoto wake aliyepotea Haki miliki ya picha Benoit De Freine

Mahakama nchini Ubelgiji inafanyia uchunguzi kituo cha kulelea watoto yatima kinachodaiwa kuwakamata na kuwasafirisha watoto kutoka nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Watoto walifikishwa Ubelgiji na kuasiliwa na familia ambazo ziliambiwa watoto hao ni yatima. Miaka kadhaa baadaye, vipimo vya vinasaba vilithibitisha kuwa baadhi yao si yatima.

Mamia ya maili kaskazini mwa mji mkuu wa DRC, Kinshasa, ni kijiji cha Gemena. Watu wengi hupata kipato kwa njia ya kilimo na uvuvi; wengine ni mafundi seremala na wenye maduka.

Abdula Libenge, mwenye miaka 34, mshonaji nguo, ni baba wa moja ya familia nne katika eneo hilo ambaye mwezi Mei mwaka 2015 alimpeleka mtoto Kishasa kwenye kile kinachodaiwa kuwa kambi ya wakati wa likizo.

Watoto wao hawakurudi tena. Bila kupata msaada wa kisheria au usaidizi wa serikali ya eneo lao, wote walichoweza kufanya ni kusubiri.

Takribani miaka miwili baada ya binti wa Libenge kutoweka, alipokea ugeni ambao hakuutarajia ambao hatimaye unaweza kumpa mwanga kuhusu kilichotokea.

Ni kwa namna gani waandishi wa habari waligundua kashfa hii?

Mwendesha mashtaka wa Ubelgiji amesema kuwa wazazi wa damu wa watoto kadhaa wa DRC walioasiliwa nchini Ubelgiji walikuwa hai bado, na wazazi walikuwa wakiwatafuta watoto wao.

Haki miliki ya picha Benoit De Freine

Waandishi wa habari wa Ubelgiji Kurt Wertelaers na Benoit de Freine walianza safari kutoka Brussels mpaka kwenye karakana ya Abdula Libenge katika kijiji cha Gemena.

Aliwakaribisha nyumbani kwake na kuwaonesha picha ya binti yake.

''Picha ilipigwa siku alipokuwa akiondoka kwenda Kinshasa,'' aliwaeleza. ''Alikuwa mwenye furaha sana. Hatukuwahi kupata nafasi ya kwenda Kinshasa. Hatuwezi kugharamia tiketi ya ndege. Lakini alipata nafasi, na jambo hili lilitufanya kujivunia.''

Ilikuwa moja kati ya picha kadhaa za kundi la watoto watatu wa kike na mvulana mmoja, wakati huo wakiwa na umri wa miaka miwili na minne.

Picha moja inawaonesha wakiwa na kijana mmoja kutoka taasisi ya vijana, msindikizaji wao kwenye iliyoitwa kambi.

''Tulichonacho pekee ni hii picha na kiatu,'' Bwana Libenge aliendelea.

Nje kwenye makazi ya Suriya Moyumbe alikuwa anasubiri huku akibubujikwa machozi, akipapasa picha ya binti yake, ambaye alikuwa mdogo alipoondoka, kwani alikuwa hawezi kuongea.

''Familia ya mume wangu inanilaumu kwa kumpeleka mtoto, sikupaswa kufanya hivyo. Lakini sisi sote tulifikiri ni fursa, ''Aliwaambia waandishi wa habari.

Wertelaers na De Freine walirejea Brussels kuwasilisha ushahidi na mwendesha mashtaka kisha akasafiri mpaka Gemena kuchukua vinasaba.

Nyumba ya kuhudumia watoto yatima jijini Kinshasa tangu wakati huo ilifungwa.

Mwanasheria Julienne Mpemba anazuiliwa nyumbani kwake na anakabiliwa na makosa ya jinai kwa kuwa ndio kiongozi wa taasisi hiyo.

Watu wengine kadhaa wameshtakiwa Ubelgiji na nchini DRC.

'kibao cha uso' kwa familia mpya

Nchini Ubelgiji, habari hii ilianza kuwafikia familia zilizoasili watoto, moja mpaka nyingine.

Wazazi wengine walishapaza sauti wakati wa mchakato wa kuasili, na waliiambia BBC, habari hizi zilithibitisha hofu yao.

''Kufahamu sifa ya DRC, nilikuwa nikiogopa sana, lakini taasisi ilituhakikishia kuwa kila kitu kitafanyika kwa mujibu wa sheria,'' alisema baba mmoja, ambaye alikataa kufahamika jina lake.

''Ilikuwa kama kuchapwa kofi usoni tuliposikia hilo. Hicho ndicho siku zote nilichokuwa najaribu kuepuka. Na sasa, nina mtoto aliyeibwa.''

Mama mmoja alieleza jinsi taasisi hiyo ilipokuwa inamshawishi kuhusu mashaka yake. Lakini siku moja, mtoto wa kike aliyemuasili aliweza kuzungumza vizuri kuhusu familia yake halisi.

''Mara aliposema wewe si mama yangu, mama yangu, tulipoanza kumsomea hadithi za watoto.

''Nilianza kupata mashaka.Nilifikiri alikuwa akimzungumzia mama ambaye alikuwa akiishi naye kabla ya kufika Ubelgiji, lakini hapana, alikuwa mama mzazi.''

Habari hiyo ilipofika Ubelgiji, watoto wanne walihusishwa. Sasa, wazazi waliowaasili watoto 15 wanasubiri matokeo ya vipimo vya DNA.

Mustakabali wa watoto

Mahakama ya familia nchini Ubelgiji itaamua kuhusu mustakabali wa watoto.

''Ni kesi kwa kesi, lakini hatima itategemea kile mtoto atakachosema. Hatuwezi tu kufanya maamuzi kwa kuwa tunafikiri itakuwa vizuri kwa mtoto bila kupata maoni ya mtoto,''.Anaeleza mwanasheria Cantwell

Haki miliki ya picha Benoit De Freine

Kijijini Gemena, Abdula Libenge hakuwa na matumaini makubwa kwa mtoto wake kurejea nyumbani.

''Ninajua watu watasema ni bora akae huko kwa sababu atakuwa na maisha mazuri. Na unajua pengine ana maisha mazuri, lakini sidhani kama ni jukumu la mtu yeyote mwingine kufanya uamuzi huo.''