Ajali ya Morogoro: Idadi ya vifo yafikia 100

aJALI mOROGORO

Idadi ya watu waliofariki kutokana na mlipuko wa lori la mafuta Agosti 10,2019 mjini Morogoro imefikia watu 100.

Idadi hiyo imefikia kiwango hicho kutokana na majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kuendelea kuaga dunia.

Watu 62 walithibitishwa kufariki siku ya mkasa na zaidi ya 70 kujeruhiwa, na toka hapo idadi ya vifo imekuwa ikiongezeka taratibu.

Awali idadi ya majeruhi 46 walisafirishwa kutoka Morogoro mpaka Muhimbili kwa matibabu ya kibobezi, lakini mpaka asubuhi ya leo, Jumatano Agosti 21 ni majeruhi 15 tu ndio waliobaki Muhimbili.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Habari wa Muhimbili, Bw Amini Aligaesha kati ya majeruhi 13 wamelazwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi na wawili wapo kwenye wadi ya wagonjwa wa kawaida.

Huwezi kusikiliza tena
Kilichotokea Morogoro?

Wengi wa majeruhi waliokimbizwa Muhimbili walikuwa wameunguzwa na moto kwa asilimia 80 na kuendelea.

Mkasa huo ulitokea majira ya saa mbili asubuhi ya Jumamosi baada ya lori lilibeba shehena ya petroli kuanguka katika mji wa Morogoro, na watu kuanza kuchota mafuta yaliyomwagika kisha mlipuko mkubwa kutokea.

Kumekuwa na hisia tofauti juu ya ajali hiyo lakini Rais wa nchi hiyo John Magufuli amewataka wananchi wake kuacha kuhukumu waliofariki na majeruhi.

Huwezi kusikiliza tena
Miili ya waliofariki yawasili ili kuagwa shule ya pili ya Morogoro

''Naona watu wanasema kwamba hawa wote walienda kuiba , tusiwe majaji wengine walienda kusaidia huku wengine wakiwa wapita njia , Mwengine alikuwa safarini kuelekea Mtwara, akazuiliwa na moto ulipolipuka ukamkuta'', alisema Magufuli baada ya kuwajulia hali majeruhi siku ya Jumapili.

Baadhi ya waliofariki waliungua kiasi cha kutokutambulika na vipimo vya vinasaba vya jeni (DNA) kupitia ndugu waliopoteza wapendwa wao.

'Tiba ya kisaikolojia' yapelekwa Morogoro

Katika kukabiliana na athari ya janga hilo kwenye jamii, serikali ya Tanzania ilituma timu ya wataalamu wa ushauri, saikolojia na ustawi wa jamii mjini Morogoro kwenda kuwahudumia wale waliopoteza ndugu na jamaa ama kupata majeraha.

Kiongozi wa msafara huo wa wataalamu takribani 30, Dkt Naftali Ng'ondi kutoka Wizara ya Afya Tanzania aliiambia BBC kuwa timu yake ilikita kambi Morogoro kuanzia Jumatatu Agosti 12.

Huwezi kusikiliza tena
Mkasa wa Morogoro umewaacha wengi na msongo wa mawazo

"Yanapotokea matukio kama haya, wale ambao wamepatwa na majeraha pamoja na familia zilizoachwa na marehemu wanakuwa kwenye mshtuko pamoja na msongo wa mawazo kiasi cha kushindwa kurudi katika hali ya kawaida. Inapokuja tiba sasa tunasema ya nafsi na tiba ya roho, akili pamoja na utulivu wa kihisia kwa binadamu hilo linakuwa ni jukumu la wataalamu wanaohusika na huduma za kisaikolojia na kijamii," ameeleza Dkt Ng'ondi.

Huduma ya wataalamu hao inafanyika hospitalini na majumbani ili kuchambua mahitaji yao na kisha kutoa ushauri, hususani wa kuondoa huzuni.

"Kikubwa tulichokigundua ni kuwa kuna vijana wengi wamepoteza maisha na kuacha watoto wadogo pamoja wenza. Pia bado kuna familia ambazo hazijapata ndugu zao, na ile miili ambayo haijatambulika teknolojia ya vinasaba inatumika."

"...kwa wale waliopata majeraha wanaweza kurejea kwenye hali ya kawaida kisaikolojia, lakini kuna tofauti ya uwezo binafsi wa kupona, wengine inaweza kuwachukua muda kidogo. Sisi kwa kipindi cha wiki mbili kazi yetu kubwa ni kuwaunganisha na familia zao na kuwapa msaada wa kiushauri. Na baada ya siku 14 timu ya wataalamu wa mkoa wa Morogoro itaendelea kufuatilia maendeleo yao," ameeleza Dkt Ng'ondi.

Mada zinazohusiana