Kesi kuhusu ombi la Lissu dhidi ya uamuzi wa Ndugai kumfuta ubunge kutajwa leo

Tundu Lissu alitangaza kupeleka mahakamani ombi la kupinga uamuzi wa spika Job Ndugai

Kesi ya aliyekua mbunge wa Singida Mashariki na mnadhimu mkuu wa kambi rasmi ya upinzani bungeni, Tundu Lissu inatajwa leo katika Mahakama Kuu nchini Tanzania. Kesi hiyo ni ya kupinga uamuzi wa kuvuliwa kwake ubunge kutokana na kutohudhuria vikao vya bunge kwa karibu miaka miaka miwili.

Lissu amefungua kesi mahakamani chini ya hati ya dharura, kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai ambaye amempa mamlaka kisheria kufanya hivyo

BBC imezungumza na Tundu Lissu akiwa nchini Ubelgiji kuhusu uwepo wake mahakamani, ambapo amesema

''Kesi inapopangiwa siku ya kusikilizwa au kutajwa au kwa hatua nyingine za kimahakama, pande zote huitwa mahakamani ni nyinyi mnaovutana au wawakilishi wenu wa kisheria au mawakili wenu''.

''Mimi nimefungua kesi kwa kutumia mwakilishi wa kisheria, mtu ambaye nimempa mamlaka kwa maandishi ili kufungua kesi yangu na kuiendesha kwa niaba yangu''.

Akizungumzia kuhusu yeye kutofika mahakamani pamoja na kutakiwa kufika mahakamani bila kukosa na pia kuwasilisha vielelezo vyote atakavyovitumia kwenye kesi hiyo Lissu alisema:

Anayetakiwa kufika mahakamani ni mtu mwenye mamlaka ya kisheria aliyompatia yeye Lissu mwenyewe.

Kuhusu shutuma dhidi yake kuwa alikuwa hajahudhuria vikao vya bunge bila taarifa Lissu amesema kuwa amefutwa ubunge huku ikifahamika wazi kuwa amekuwa nje kwa matibabu tangu tarehe 7 mwezi Septemba mwaka 2017.

Lissu amesema kwa mujibu wa sheria na taratibu za bunge la Jamuhuri ya muungano wa Tanzania, wajibu wa kutoa taarifa kuhusu mbunge anayeumwa sio wajibu wa mbunge mwenyewe, ni wajibu wa waganga walioajiriwa na bunge.

''Kwa hiyo Bunge lilikuwa na wajibu wa kujua muda wote tangu tarehe7 mwezi Septemba mwaka 2017 kuhusu maendeleo yangu afya''.

Kwa mujibu wa Lissu madaktari walio na wajibu wa kufuatilia afya yake, hawakuwahi kufanya hivyo kwani hakuwahi kuwaona hospitalini kwani walitakiwa kwenda Nairobi.

''Walitakiwa kuja Nairobi sikuwaona, walisema wangekuja hawakuja, walitakiwa waje Ulaya hawakuja, hivyo waliovunja sheria si mimi ni wao''.

Lissu amesema alitarajia hatua zilizochukuliwa na spika kutokea kwa sababu alishasema kwa hiyo ilipotokea mwezi wa sita wala haikua ajabu.

''mtu ambaye alishakuwa na nia ya kunifuta ubunge nisingeweza kumzuia, vinginevyo labda ningesema niachane na habari ya matibabu nirudi Tanzania''.

Kuhusu afya yake Amesema anaendelea vizuri sana amemaliza dawa zote mwishoni mwa mwezi uliopita . Ni mwezi wa pili sasa hatumii magongo kwa sasa anafanya mazoezi na juma lijalo siku ya Jumanne atakutana na madaktari wake kwa mara ya mwisho.

''Nikishapona, madaktari wangu wakasema sasa unaweza kurudi Tanzania, nitaanza utaratibu wa kurejea, hili wala sio siri''. Alisema Lissu.

Jimboni Singida Mashariki

Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Miraji Mtaturu, alipita bila ya kupingwa katika hatua za awali za matayarisho ya uchaguzi mdogo ambao ungefanyika kwenye Jimbo la Singida Mashariki, baada ya wagombea 12 wa vyama vya upinzani kutorejesha fomu.

Uchaguzi huo mdogo ulikuwa ufanyike Julai 31, mwaka huu, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Tundu Lissu kuvuliwa ubunge.

Uchaguzi katika jimbo hilo ulikuwa umepangwa kufanyika ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Lissu aliyepoteza sifa za kuwa mbunge kutokana na kutojaza fomu za mali na madeni na utoro bungeni.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii