Winnie Byanyima: Mwanasiasa na mwanadiplomasia kutoka Uganda achaguliwa mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS

Winnie Byanyima Haki miliki ya picha South China Morning Post

Winifred Byanyima, mhandisi, mwanadiplomasia na mwanasiasa kutoka nchini Uganda ameteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa shirika la Umoja wa mataifa la kupmbana na maambukizi ya ukimwi UNAIDS.

Mpaka kufikia sasa, amehudumu kama mkurugenzi mtendaji wa mwamvuli wa kimataifa wa mashirika ya misaada Oxfam.

Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amemteua Bi Byanyima katika wadhifa huo na anayeingia kuichukua nafasi ya mkurugenzi mtendaji aliyekuwepo na aliyejiuzulu Michel Sidibé raia wa Mali.

Kwa mujibu wa UNAIDS Byanyima anaingia katika wadhifa huo kwa uzoefu mkubwa na uwajibikaji katika kutumia nguvu za serikali tofuati na mashirika ya kijamii na sekta ya kibinfasi katika kuangamiza janga la ukimwi duniani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Winnie Byanyima anafahamika kimataifa kuwa mtaalamu na mteteaji wa haki za wanawake

Katika mtandao wake wa twitter, bi Byanyima ameandika : 'Ni heshima kubwa kutakiwa kuongoza jitihada za Umoja wa mataifa na wa dunia kupambana na ukimwi! naukumbatia wadhifa huu kwa unyenyekevu, ari na imani kwamba tunaweza kuliangamiza janga hili kufikia 2030. Natazamia kujiunga na kikosi cha UNAIDS na kushirikiana kwa karibu na wafadhili wenza na washirika kuondosha vizuizi katika kuzuia, kutibu na kutoa huduma'.

Winnie Byanyima ni nani?

Winnie Byanyima, ni mwanaharakati wa mashinani, mteteaji haki za binaadamu na mtumishi wa umma anayefahamika kimataifa kuwa mtaalamu wa masuala ya haki za wanawake.

  • Alizaliwa Mbarara Uganda, mnamo Januari 13 1959 (ana umri wa miaka 60).
  • Ni mkewe kiongozi wa upinzani Uganda Warren Kizza Besigye au Dkt Besigye kama anavyofahamika na wengi na wamebhatika kupata mtoto mmoja wa kiume.
  • Aliwahi kuchaguliwa kwa mihula mitatu na alihudumu kwa miaka kumi na moja bungeni Uganda.
  • Amehudumu pia katika tume ya Umoja wa Afrika na pia mkurugenzi wa masuala ya jinsia na maendeleo katika UNDP.
  • Bi. Byanyima amehudumu katika bodi kadhaa za kimataifa na tume na kwa sasa yuko kwenye bodi kuu ya taasisi ya kimataifa ya utafiti wa wanawake.
  • Ni mwanadiplomasia aliyehudumu katika ubalozi wa Uganda nchini Uingereza na amewahi pia kuwa mjumbe mkuu wa Uganda Ufaransa katika miaka ya 80 na 90.
  • Ana shahada kuu ya uhandisi katika suala la uhifadhi nishati na mazingira kutoka Cranfield Institute of Technology shahada ya kwanza katika uhandisi wa anga kutoka chuo kikuu cha Manchester, Uingereza.
  • Aliteuliwa kuwa mkurugenzi mtendaji wa Oxfam mnamo Mei mosi mwaka 2013.
Huwezi kusikiliza tena
Wanawake watano maarufu wa Afrika waliokuwa wakimbizi

Hii hapa ni mifano mingine ya wanawake wa kiafrika wenye ushawishi kimataifa:

Fatou Bensouda,

Fatou Bensouda, ni wakili kutoka nchini Gambia na mwendesha mkuu wa mashtaka katika mahakama ya kimataifa ya jinai, ICC.

Bensouda mwenye umri wa miaka 58, aliteuliwa katika wadhifa huo mwezi Juni mnamo 2012 na kuchukua nafasi ya Luis Moreno-Ocampo kutoka Argentina.

Kabla ya hapo Bensouda alikuwa naibu mwendesha mkuu wa mashtaka tangu mwaka 2004.

Amewahi kuwa waziri wa sheria nchini Gambia.

Sahle-Work Zewde:

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Bi Sahle-Work ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu ambaye sasa amekuwa kiongozi wa kipekee mkuu mwanamke barani Afrika.

Mwaka jana wabunge nchini Ethiopia walimchagua Sahle-Work Zewde kuwa rais wa kwanza mwanamke Ethiopia.

Bi Sahle-Work ni mwanadiplomasia mwenye uzoefu ambaye sasa amekuwa kiongozi wa kipekee mkuu mwanamke barani Afrika.

Rais Sahle-Work amewahi kuwa balozi wa Ethiopia nchini Senegal na Djibouti.

Ameshikilia nyadhifa kadhaa katika Umoja wa mataifa , ikiwemo mkuu wa kujenga amani katika Jamhuri ya Afrika ya kati.

Kabla ya kuwa rais wa Ethiopia, Bi Sahle-Work alikuwa mwakilishi wa UN katika Umoja wa Afrika.

Kwa mujibu wa katiba ya Ethiopia , rais hana nguvu ikilinganishwa na wadhifa wa waziri mkuu ambaye yeye ndiye, aliye na nguvu za kisiasa nchini.

Ameenah Gurib-Fakim Mauritius

Haki miliki ya picha AFP

Ameenah Gurib-Fakim, aliwahi kuwa rais wa Mauritius kabla ya kujiuzulu kufuatia mzozo wa kifedha uliokuwa unamkabili.

Alituhumiwa kutumia kadi ya fedha aliyopewa na shirika la misaada kununua vitu vya kibinfasi vyenye thamani ya maelfu ya dola.

Bi Gurib-Fakim ni mwanasayansi tajika na mnamo 2015 alikuwa mwanamke wa kwanza kuchaguliwa katika wadhifa wa rais wa Mauritius.

Ngozi Okonjo-Iweala,

Ngozi Okonjo-Iweala, aliyekuwa waziri wa fedha nchini Nigeria.

Bi Okonjo-Iweala, mwenye umri wa miaka 58, ameshikilia nyandhifa mbalimbali za kimataifa, katika sekta ya fedha .

Aliheshimika sana wakati akiwa mkurugenzi mkuu katika benki ya dunia kwa miaka mitatu, kabla ya kushindana katika kinyang'anyiro kuwa rais wa benki hiyo.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii