Rais wa Tanzania John Magufuli ndiye mwenyekiti mpya wa SADC

Viongozi wa SADC

Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika SADC, imetoa wito kwa jamii ya kimataifa kuiondolea Zimbabwe vikwazo vya kiuchumi.

Mwenyekiti mpya wa Jumuiya hiyo ambaye pia ni Rais wa Tanzania, John Magufuli amesema vikwazo hivyo vimelemaza uchumi wa nchi hiyo.

Bw. Magufuli amesema hayo wakati alipokua akikabidhiwa uwenyekiti wa SADC na mtangulizi wake Rais wa Namibia, Dk Hage Geingob, wadhifa ambao ataushikilia kwa mwaka mmoja.

''Tunaahidi kushirikiana na nchi zote Wanachama wa SADC kuhakikisha kupitia mkutao huu ndoto na mawazo ya Baba wetu wa Taifa pamoja na viongozi wengine waanzilishi wa Jumuiya hii yanaendelea kutekelezwa kwa vitendo'' alisema Rais Magufuli akipokea uwenyekiti huo.

Katika hotuba yake mwenyekiti huo mpya, ameomba rasmi Jamii ya Kimataifa kutathmini upya vikwazo dhidi ya Zimbabwe na kuongezea kuwa nchi hiyo kwa sasa ipo chini ya utawala mpya.

Rais wa Zimbabwe Emerson Mnangagwa pia yuko nchini Tanzania kuhudhuria mkutano huo wa kilele wa siku mbili.

Zimbabwe iliwekewa vikwazo hivyo na mataifa ya Magharibi miongo miwili iliyopita kufuatia hatua ya rais Robert Mugabe kuchukua kwa lazima ardhi ya walowezi wa kizungu.

Mwenyekiti huyo mpya ameapa kuhakikisha amani na uthabiti unadumishwa katika kanda hiyo ili kukwamua uchumi wa mataifa wanachama.

Pia ametoa wito kwa nchi wanachama kushirikiana kibiashara badala ya kuagiza bidhaa kutoka nje.

''Narudia tena kuwakaribisha waheshimiwa wakuu wa nchi kwenye mkutao huu wa 39 wa SADC hapa Dar Es Salaam mahali penye amani ambapo ni kitovu cha harakati za ukombozi Barani Africa'' alisema Magufuli

Kiswahili pia kimetangazwa kuwa lugha ya nne rasmi ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc)

Lugha zingine rasmi katika Jumuiya ya SADC ni Kiingereza, Kifaransa na Kireno.

Hapo jana Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli na mwenzake Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini walitangaza kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kirafiki baina ya mataifa hayo mawili wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC

Magufuli na Ramaphosa pia walitoa wito kwa wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini kuwekeza kikamilifu kwenye nchi hizo.

Tayari rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ameanza kutumia lugha ya Kiswahili kwenye Twitter yake akielezea jinsi alivyopokelewa nchini Tanzania ambayo ni mwenyeji wa mkutano wa 39 wa kilele wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika, SADC.

Viongozi pia wanatarajiwa kujadili masuala kadhaa ikiwa ni pamoja na Usalama katikakanda ya Kusimi mwa Afrika na uchimi wake. Mkutano wa leo inaadhimisha miaka 17 kubuniwa kwa Jumuiya ya maendeleo ya matifa ya kusini mwa Afrika

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii