Je mwanamke mjamzito mwenye virusi vya ukimwi anaweza kumnyonyesha mwanae?

Virusi vya HIV vinaweza kuingia kwenye maziwa ya mama na hivyo kumuambukiza mtoto wake wakati anapomnyonyesha Haki miliki ya picha PURESTOCK
Image caption Virusi vya HIV vinaweza kuingia kwenye maziwa ya mama na hivyo kumuambukiza mtoto wake wakati anapomnyonyesha

Maambukizi ya virusi vya Ukimwi(HIV) imekuwa ni changamoto kwa akina mama walioambukia maradhi hayo wanaotaka kuwanyonyesha watoto wao mara baada ya kujigungua.

Hii inatokana na hatari ya uwezekano wa mama kumuambukiza mwanae wakati anapomnyonyesha.

Hofu hii hutokana kuongezeka kwa virusi vya HIV katika seli nyeupe za damu katika na maziwa ya mama anapokuwa mjamzito, hali inayoongeza uwezekano wa kumuambukiza mtoto wake virusi hivyo anapomnyonyesha.

Viwango vya juu vya virusi katika plasma, na huenda katika maziwa ya mama, huonekana kama chanzo kikuu cha maambukizi ya virusi vya HIV kutoka kwa mama hadi mtoto na maambukizi hayo yamekadiriwa kuwa ni karibu 30%.

Katika taifa la Rwanda akinamama walioambukia virusi vya ukimwi wanaweza kujifungua na kunyonyesha watoto wao bila kuwaambukiza mtoto.

Hii ni baada ya serikali ya nchi hiyo kuzindua kampeni ya kusaidia akinamama walio na virusi vya HIV kuwanyonyesha watoto wao bila kuwaambukiza ukimwi.

Kampeni hiyo inafanyika katika hospitali na vituo vya afya kote nchini humo.

Haki miliki ya picha Getty Images

Katika kituo cha afya cha Remera mjini Kigali, misururu mirefu ya akinamama wanaoishi na virusi vya ukimwi haiishi ,baadhi wanaonekana wajawazito ,wengine wanabeba watoto zao, anasema mwandishi wa BBC Yves Bucana ambaye alitembelea kituo hicho.

Wanafika kupata ushauri nasaha kuhusu namna ya kujilinda kuambukiza watoto wao ilhali akinamama waliokwishajifungua wakifika kumuona daktari ili wafanyiwe ukaguzi wa jinsi wanavyofuata utaratibu wa kuwalinda kuambukiza watoto zao.

Ni katika mpango ulioanzishwa na serikali wa kusaidia akinamama wajawazito na wanaonyonyesha kuweza kuwahudumia watoto wao na kuwalinda maambukizo ya HIV.

Emile Musabyimana mkuu wa kituo cha afya anasema:''Tunawasaidia akinamama kuwa na afya njema pamoja na watoto zao.Tunapima kinga yake ya mwili kuona kwamba haijapungua pamoja na kiwango cha virusi alivyo navyo.Tunamfanyia vipimo kadri mtoto anavyokua .Hii haiwezi kumzuiya mtoto kunyonya..hakika asilimia 99 ya watoto hawapati maambukizo yoyote''. Anasema.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Mama wenye virusi vya HIV wanashauriwa kufuata masharti na ushauri wa Daktari ili kuepuka kuwaambukiza watoto wao kupitia maziwa ya mama

Mama mmoja ambaye hakupenda kutajwa jina lake katika taarifa hii ameiambia BBC kuwa vipimo alivyofanyiwa kabla ya kujifungua vilibainisha kwamba ana virusi vya ukimwi,lakini alifuatiliwa kwa karibu na daktari hadi alipojifungua.''Sasa mtoto wangu ametimiza umri wa miezi 9 na hana maambukizi yoyote, na jambo muhimu lilikua ni kumuokoa mwanangu na ili kutimiza hilo ni lazima ufuate masharti na ushauri wa daktari'', alisema.

Akaongeza kuwa :''Masharti ni magumu lakini lazima kuyafuata yaani saa ya kumeza dawa kwako wewe na pia kwa mtoto wako, usizidishe hata dakika moja.Lazima kutembea na dawa ikiwa unahisi saa ya kutumia dawa itafika ukiwa haupo nyumbani, ujue una hatari sana ya kujifungua mtoto na ushindwe. Kumyonyesha mtoto ni raha kitu muhimu kwasababu mzazi anahisi upendo wa mtoto wake na vile vile mtoto anahisi upendo wa mamake wakati wa kumnyonyesha'', alisema.

Bi Uwonkunda Fatuma ni muuguzi anayefuatilia kila siku akinamana wenye kuwa na virusi vya ukimwi katika mpango huu anasema Japo masharti ni magumu lakini si kwamba hayawezikani. ''Hatari ya mama kuambukiza mtoto wake ni kubwa sana, mtoto akiwa na maradhi ya vidonda vya mdomoni ni rahisi sana kuambukizwa HIV wakati ananyonya...tunamshauri mama kuchunguza kila wakati mdomoni mwa mtoto na kusitisha kumnyonyesha kwa muda ikiwa mtoto ana ugonjwa huo ili kwanza mtoto atibiwe.

Image caption Takwimu za mwaka 2018 nchini Kenya zinaonyesha kupungua kwa maambukizi ya mama kwa mtoto ya virusi vya HIV kutoka 14% hadi 11%

Mnamo miezi 24 tunamfanyia vipimo vya mwisho ,tukikuta mtoto hana tatizo inamaanisha kwamba mamake alifuata masharti vizuri na tukamruhusu kwendelea kutumia dawa kwengineko hata nyumbani.''anasema Bi fatuma.

Mama wajawazito wanaoishi na virusi vya Ukimwi wanaweza kupunguza hatari ya maambukizi ya HIV kwa watoto wanaojifungua.

  • Ni muhimu wa kuzaa mtoto katika kituo cha afya cha ngazi ya juu ni kuwepo kwa dawa za kuzuia maambukizi ya virusi na pia mbinu salama za kuzaa zinatolewa, ili kuzuia Maambukizi ya VVU kutoka kwa Mama hadi kwa Mtoto.
  • Matumizi ya Dawa za Kupunguza Makali ya Virusi vya Ukimwi zinazopendekezwa ili kuzuia magonjwa nyemelezi.
  • Kufanya ngono kwa kutumia kondomu na mwenzi wake ili kumlinda kutokana na maambukizi ya Virisi vya Ukimwi, na kuhakikisha kwamba yeye hapati magonjwa mengine yoyote ya kutoka kwake ikiwa anafanya ngono bila kinga na mtu mwingine yeyote.
  • Kula chakula kingi kilicho na lishe bora, kama inavyopendekezwa kwa kina mama wote wajawazito bila kujali hali yao ya Virusi vya Ukimwi.
  • Kudumisha usafi wa kibinafsi, kama inavyopendekezwa kwa kila mtu ili kuzuia maambukizi ya bakteria, virusi, protozoa na fungi, maambukizi ya parasiti na vimelea na wadudu, na matatizo ya ngozi.
  • Jinsi ya kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kutoka kwa Mama hadi kwa mtoto ikiwa ni pamoja na njia salama ya kumlisha mtoto.
  • Kwamba mwenzi au mume wa mama na watoto lazima wachunguzwe kwa Virusi vya Ukimwi.
  • Umuhimu wa kuzuia maambukizi ya VVU kwa watu wengine na jinsi ya kufanya hivyo.
  • Umuhimu wa rufaa kwa ufuatiliaji na maendeleo ya huduma ya afya ya virusi vya Ukimwi, mwenzake na kwa mtoto aliye katika hatari ya kuambukizwa VVU, na wanafamilia wengine.
  • Magonjwa nyemelezi ni maambukizi yanayosababishwa na bakteria au virusi kwa watu ambao mifumo ya kingamwili yao ni dhaifu, kwa mfano kwa sababu ya virusi vya Ukimwi.

Hali iko vipi Afrika Mashariki?

Hakuna takwimu rasmi za akinamama wanaojifungua wakiwa na virusi vya ukimwi nchini Rwanda kutokana na kwamba kuna wachache wanaojifungua bila kufika hospitali.

Hata hivyo kulingana na idara ya afya ya Rwanda, takwimu zinaonyesha kuwa kati ya watoto laki moja wanaozaliwa ni 150 tu wanaokutwa na virusi vya ukimwi.

Katika nchi nyingine ya Afrika mashariki Nchini Kenya takwimu za mwaka 2018 zinaonyesha kupungua kwa maambukizi ya mama kwa mtoto ya virusi vya HIV kutoka 14% hadi 11% miongoni mwa akina mama wajawazito wanaoishi na virusi hivyo, kulingana na ripoti juu ya maendeleo katika kukabiliana na ukimwi, iliyoandaliwa na Wizara ya afya.

Nchini Tanzania pia kumekuwa na kampeni kadhaa za afya ya mama na mtoto na kuzuia maambukizi ya virusi vya HIV.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii