Marekani, Uingereza 'waendelea kufuatilia' kesi ya Kabendera

Erick Kabendera

Ofisi za ubalozi wa Marekani na Uingereza nchini Tanzania zimeendelea kumulika kesi ya mwanahabari maarufu wa uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera.

Wiki mbili zilizopita ofisi hizo zilitoa tamko la pamoja juu ya kuhusu kile walichokiita "wasiwasi wa kuzorota kwa kwa haki za kisheria nchini Tanzania."

Katika tamko hilo, ofisi hizo mbili za ubalozi zinadai kuwa imedhihirika kwa zaidi ya mara moja watu kutiwa kizuizini kwa muda nchini Tanzania bila kupelekwa mahakamani na kubadilishiwa mashitaka na mamlaka zake za kisheria.

"Tuna wasiwasi hasa kwa tukio la hivi karibuni -- jinsi ambavyo halikushughulikiwa kwa haki la kukamatwa, kuwekwa kizuizini na tuhuma za mashtaka ya mwandishi wa habari za uchunguzi Bw Erick Kabendera, ikizingatiwa ukweli kwamba alinyimwa haki ya kuwa na mwanasheria kwenye hatua za awali na kutiwa kizuizini kwake, ambapo ni kinyume cha sheria ya makosa ya jinai," inasema sehemu ya tamko hilo.

Jumatano jioni, ofisi hizo mbili tena kwa kupitia mitandao ya kijamii zilitoa ujumbe kuwa wanaendelea kufuatili kesi ya Kabendera.

"Tunaendelea kufuatilia kesi ya Erick Kabendera. Haki za kisheria ni haki ya raia wot, na kuhakikisha upatikatnaji wa haki hiyo ni wajibu wa serikali zote," unaeleza ujumbe ambao umechapishwa katika kurasa za twitter za Ubalozi wa Marekani na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi Sarah Cooke.

Kabendera anakabiliwa na mashtaka gani?

Kabendera alipandishwa kizimbani Agosti 5 na kusomewa mashtaka matatu ya ubadhirifu wa kiuchumi .

Katika mashtaka hayo Kabendera anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za kitanzania.

Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliowasilishwa, Kabendera anadaiwa kuyatekeleza hayo baina ya Januari 2015 na Julai mwaka huu mjini Dar Es Salaam na kwa baadhi ya makosa anadaiwa kuyafanya kwa ushirikiano wa watu ambao hawakuwepo mahakamani.

Makosa yote hayana dhamana na Kabendera anaendelea kusota rumande.

Alifikishwa tena mahakamani Jumatatu wiki hii, lakini kesi ikaakhirishwa mpaka Agosti 30 baada ya upande wa mashtaka kudai hawajakamilisha upelelezi.

Kumekuwa na wasiwasi ndani na nje ya Tanzania kuhusu namna ambavyo amekamatwa, na taswira inayotokana na hatua hiyo kwa uhuru wa yombo vya habari nchini humo.

Pia baadhi ya wanaharakati wameonyesha kushangazwa na kubadilika kwa yaliominika kuwa ndio makosa anayotuhumiwa nayo.

Awali maafisa wa polisi na wale wa idara ya uhamiaji walisema anachunguzwa kuhusu utata wa uraia wake. Baadaye mawakili wake walitoa taarifa wakieleza mteja wao atashtakiwa kwa kuhusika na ripoti iliyochapiswha katika jarida la The Economist, lakini mahakamani kibao kikageuka tena na kuwa kesi ya ubadhirifu wa kiuchumi.

"Tunaisihi serikali ya Tanzania kutoa hakikisho la mchakato wa kutenda haki kisheria kwa raia wake, kama ilivyotambua kwamba ni haki ya msingi na kuridhia kwenye mikataba mbali mbali ya haki za kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa, miongoni mwao ikiwemo azimio la kimataifa la haki za kirai na kisiasa," inaeleza sehemu ya tamko la awali la Marekani na Uingereza juu ya wasiwasi huo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii