Kufungwa kwa maeneo ya burudani wakati wa sensa kwazua mjadala Kenya

Watu katika eneo la burudani Haki miliki ya picha Getty Images

Raia nchini Kenya wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuelezea kutoridhishwa kwao na hatua ya kufunga maeneo ya burudani ili kufanikisha mpango wa kitaifa wa kuhesabu watu.

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang amezua gumzo nchini humo baada ya kutangaza mabaa na kumbi za burudani kufungwa kwa ajili ya shughuli ya kuhesabu watu maarufu sensa.

Kwa mujibu wa Bw. Matiang'i maeneo ya burudani yatafungwa kuanzia saa kumi na moja jioni Jumamosi na Jumapili ili kuhakikisha wahudumu wa maeneo hayo wote wako nyumbani kufikia saa kumi na mbili jioni wakati ambapo maafisa wa kuhesabu watu wataanza kazi yao.

"Tutafunga maeneo yote ya burudani hususana baa kuanzia saa kumi na moja jioni ili kukupatia muda wa kuwa nyumbani kabla ya maafisa wa kuhesabu watu kufika nyumbani kwako kuanzia saa kumi na mbili jioni," alisema waziri huyo siku ya Jumatano akitoa agizo hilo.

Waziri huyo amewahakikishia Wakenya kuwa hali ya usalama utaimarishwa na maafisa wote wa usalama wamezuiliwa kwenda likizo ili kuhakikisha zoezi hilo linafanywa kwa utaratibu.

Bw. Matiang'i aidha ametoa onyo kali kwa wale ambao watajaribu kusimamia zoezi hilo bila idhini kwa kudai kuwa asasi zote za kigeni na watu binafsi walipigwa msasa kabla ya kuidhinishwa.

Serikali ya Kenya pia inatarajiwa kutumia sensa hii kujumuisha watu walio na jinsia mbili katika juhudi za kuwatambua na kujua hesabu yao.

Taifa hilo linapania kuwa nchi ya kwanza ya Afrika Mashariki kutekeleza sheria ya kuwatambua watu wenye jinsia mbili.

Sensa zilizopita zilikuwa na utambulisho wa jinsia mbili, ya kiume na ya kike. Hatua hiyo iliwalazimu watu zaidi ya 700,000 ambao wana jinsia zote mbili kujitambulisha na jinsia ambayo haikuelezea kikamilifu wao ni nani hasa.

Shughuli ya kuhesabu watu pia inafanyika mara ya kwanza tangu Kenya ilipoidhinisha katiba mpya mwka 2010.

Baadhi ya watu wanasema ukizingatia sababu hizo kuna haja ya wananchi kupewa siku ya mapumziko lakini wamekuwa wakitumia mitandao ya kijamii kuelezea hisia zao kuhusu sensa hiyo.

Lakini mtumiaji Chris-Leo alikuwa na mawazo tofauti kabisa na ikiwa watu wapewe siku ya kupumzika au la.

Chris aliwafananisha wake majumbani na ''magaidi'' kwa waume zao...

Baadhi yao wanasema watajiwekea pombe zao majumbani kabla ya shughuli hiyo kuanza huku wengine wakifanya matani kuhusu baadhi ya maswali ambayo huenda wakaulizwa.

Clive Wanguthi alioandika: Ati matiangi said all bars will be closed during the census??

Kuna wale ambao hupendelea kufuatilia michuano ya Ligi Kuu ya England katika kumbi za burudani hasa mechi zinazochezwa wikendi.

Kwa mfano wikendi hii ya sensa kuna mchuano kati ya Arsenal na Liverpool itakayochezwa muda ambao serikali imeagiza maeneo hayo kufungwa.

Wengine walitania kuhusu baadhi ya maswali watakayoulizwa na maafisa wa sensa.

Wakenya wanaoishi nje ya nchi hawatahesabiwa lakini jamaa zao wataulizwa maswali kuwahusu hasa wale waliohamia nchi zingine kutoka mwaka 2014.

Shughuli hiyo itaanza tarehe 24 mwezi Agosti na kukamilika tarehe 31 mwezi huo huo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii