Pombe ya ulanzi inavyowakwamua kiuchumi wakaazi wa Iringa Tanzania

Pombe ya Ulanza

Nchi za Kiafrika zimekua zikihangaika kukuza na kuboresha chumi zao, kwa kujiwekea na kupanga mikakati mbalimbali kufikia lengo hilo.

Kwa kuzingatia ndoto hiyo nchi kama Tanzania inapania kuwa na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Mikoa ya nyanda za juu kusini mwa Tanzania ambako mianzi hupatikana kwa wiki, wajasiriamali mbalimbali wameamua kutumia rasilimali hiyo kuanzisha viwanda mbalimbali vya usindikaji, ikiwemo vya pombe ya ulanzi.

BBC ilitembelea mkoani Iringa na kujionea jinsi pombe ya kienyeji ya wenyeji wa mkoa huo, Ulanzi inavyogeuzwa moja kwa moja kuwa pombe ya viwandani.

Katika kijiji cha Mlandege wakulima wa ulanzi wanaelezea faida na hasara ya zao hilo la ulanzi.

''Watoto tunawapeleka shule kwa sababu ya hii hii ulanzi na mambo ya kilimo. kwa upande mwingine pia ni kinywaji vile vile ukizidisha ni madhara pia kwa hiyo tunakunya kwa kipimo,'' mmoja wa wanakijiji aliiambia BBC.

Hata hivyo anasema kuwa viongozi wanawashauri sana kuhusu unywaji wa kileo hicho kupindukia.

Diwani wa kata ya Mseke mkoani Iringa, Robert Lawa anasema wananchi katika eneo lake wamekuwa wakipata kipato kutokana na ulanzi huku akieleza pia madhara ya kinywaji cha ulanzi iwapo mnywaji atazidisha.

Anasema mbali na kuwa kinywaji hicho kinampatia mtu kipato, kulipia watoto ada umewasaidia baadhi ya wanavijiji kujikwamua kiuchumi.

''Wakati wa ulanzi mwingi tabia ya watu kufanya ngono zembe, kupata mimba zisizotarajiwa na wengine inawapa uvivu wa kutofanya kazi kabisa,'' anasema Bw. Lana

Kuna baadhi ywa wakaazi ambao wanawanywesha watoto wao pombe hiyo ya kienyeji lakini Diwani Lana anasema kuwa yeye na maafisa wake wamekuwa wakielimisha wazazi juu ya kuwanywesha watoto kinywaji hicho.

Awali ilielezwa kuwa katika maeneo yanayogema pombe ya ulanzi mkoani Iringa kuwa na unywaji wa ulanzi uliopitiliza, ongezeko la utapiamlo na lishe duni kwa watoto ilikuwa ikiongezeka.

Mratibu msaidizi wa afya ya Uzazi na mtoto manispaa ya Iringa Afra Mtuya anazungumzia madhara ya watoto wadogo kupewa ulanzi hali inayomsababishia udumavu.

Bi Mtuya anasema akinamama huwapatia watoto wao pombe ya ulanzi kwa sababu ina ladha tamu kiasi cha kwamba watoto wanavutiwa nayo hali inayomfanya kunywa hadi analewa na kulala.

''Mtoto kama huyo wakati mwingi hali kwa wakati unaofaa na mzazi asipotilia maanani tatizo hilo mtoto laza atapata utapya mlo, uatapa udumavu wa mwili pia na akili,'' alisema.

Ili kuepukana na madhara ya unywaji wa pombe hiyo kiholela na bila vipimo na juhudi za kufanya kinywaji hicho kuwa cha kisasa, na mwamko uliopo sasa wa ujenzi wa viwanda nchini Tanzania hususan vidogo na vya kati.

Kuna baadhi ya watu wameamua kutumia fursa hiyo baada ya viwanda vingi vidogo na vya kati kuanzishwa katika sehemu hiyo.

''Tuliamua kufanya hivyo baada ya kuona kwamba ulanza haunasoko vijijini, halafu wagemaji wenyewe hawagemi kwa usafi tukaona wacha tuboereshe zaidi, ''Sophia Mahmoud Msola, Mwanzilishi wa kiwanda hicho anasema.

Mjasiriamali huyo anasema alipata msukumo zaidi wa kuendeleza biashara hiyo kutokana na tamko la Rais wa Tanzania John Magufuli wakati alipozuru eneo la Iringa na kutangaza kuwa Tanzania inaelekea kuwaya kiviwanda.

''Nilijua hapa nitapata msaada wa kujiendeleza nikaanza kusindika taratibu'' aliongeza mjasiriamali huyo aliyeajiri wafanyakazi watatu, na vibarua wawili.

Anasema changamoto ya kufanya kinywaji hicho kuw acha kisasa ni kuwa kikitiwa kwenye chupa, chupa hiyo inavunjika.

''Ulanzi huwezi kusindika kwenye plasiki''

Aliiambia BBC kuwa ana uwezo wa kuuza kinywaji hicho hadi kreti tano lakini hawezi kufanya hivyo kwa sababu Ulanzi hauwezi kuwekwa kwenye chupa.

Bi Msola anasema laiti angelipata vifungashio mna mtaji wa kutosha angeliweza kujisaidia yeye binafsi na jamii inayomzunguka.

Pombe ya Ulanzi iligunduliwa wakati wa utawala wa machifu wa kabila la Wabena katika Wilaya ya Njombe baada ya mti mchanga wa mwanzi kukatika na kuanza kutoa maji matamu.

Tangu wakati huo, pombe hiyo imekuwa ikithaminiwa na wakazi wa Mkoa wa Iringa na tayari imesambaa na kufika katika maeneo mengine mengi hasa kusini mwa Tanzania.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii