Watanzania na wahamiaji wengine wa kiafrika wahofia ghasia Afrika Kusini

ghasia

Chanzo cha picha, Getty Images

Baadhi ya Watanzania wanaoishi nchini Afrika Kusini wamelalamikia vurugu ambazo zinazoendelea nchini humo kuwa ni muendelezo wa chuki ya wenyeji dhidi ya raia wa kigeni.

Watanzania hao wamedai kuwa bado hali si shwari na inawawia vigumu wao hata kutoka nje kwenda maeneo ya mjini.

"Hali ni mbaya kwa kweli , usalama hamna" Yusuph Omar ameieleza BBC na kuongeza kuwa watu wanapigwa , wanachomwa moto na kuuwawa.

Omar anasema kwamba hajui idadi kamili ya watu waliouwawa kutokana na vurugu hiyo lakini hali zao ziko matatani na wanaishi kwa hofu sana.

Amesema kuwa wenyeji hao wanalenga maduka yote ya wageni haswa na maeneo ambayo magari yanaegeshwa kwa ajili ya kuuzwa(Yadi za magari) , na kuchoma moto magari na vitu vingine vya thamani.

Jumuiya za watanzania, wasomali na wengine walikutana katika kikao hapo jana na kuhamasishana kuwa watu wasilale wanapaswa kupambana na kuhakikisha kuwa uonevu unaisha.

Ingawa changamoto bado ni kuwa wao wako wengi kwa sababu wapo nchini kwao tofauti na sisi ambao ni wageni.

Uamuzi huu umekuja baada ya kuona kuwa hakuna hatua yoyote kali iliyotolewa na serikali na wananchi walipata hasira baada ya mkuu wa polisi kukanusha kuwa hakuna chuki za kibaguzi zinazoendelea".

Hata hivyo aliongeza kuwa vurugu hizi zimelenga raia wa Nigeria kwa sababu wanadai kwamba , wageni hao wanawauzia madawa ya kulevya na kufanya biashara ya binadamu, lakini sio rahisi pia kutofautisha yupi ametoka Nigeria au taifa lingine hivyo wageni wote wa mataifa ya kiafrika tumebaki na hofu ".

Chanzo cha picha, AFP

Jumanne Hassan ni mfanyabiashara wa magari anayeishi Afrika Kusini yapata miaka minne sasa.

Yeye anasema fujo hizi zilianza tangu wiki iliyopita kisa kilikuwa ni dereva wa Taxi aliuwawa na kudaiwa kuwa aliyemuua alikuwa mtanzania au mnaijeria wakati ukweli ni kuwa waliuwana wao wenyewe.

"Raia wa Nigeria na Ethiopia ndio wako hatarini zaidi, sisi watanzania tunawasiliana kwa karibu ili kulindana.

Ujumbe wangu kwa watu wa nyumbani ni kuwa wasiwe na hofu tuko salama ingawa hali si shwari huku", Jumanne alisisitiza.

Maeneo ambayo vurugu zinaendelea ni Alexandria, Pretoria na Johanesburg, na polisi wameweka doria huko.

Rais wa Naigeria atuma mwakilishi Afrika Kusini

Chanzo cha picha, AFP

Kufuatia vurugu hizo, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari ametuma mwakilishi nchini Afrika Kusini kuzungumzia mzozo huo .

Mara baada ya waziri wa mambo ya nje wa Nigeria, Geoffrey Onyeama kuandika katika ukurasa wa tweeter na kusema "Yatosha sasa" .

Naye rais Cyril Ramaphosa amelaani vurugu hizo zisizokuwa na maana kuendelea.

Alisema" hakuna maana kwa waafrika kusini kuwavamia wageni".

Serikali nyingine za mataifa ya kiafrika yameeleza hofu juu ya raia wake dhidi ya chuki hiyo na kutoa tahadhari juu ya vurugu hizo.

Ubalozi wa Ethiopia nchini Afrika Kusini umewashauri raia wake walioko nchini humo kufunga maduka wakati wa vurugu hizo zikiwa zinaendelea katika mji wa kibiashara wa Johannesburg .

Vilevile wameshauriwa kuwa mbali na kutojihusisha na vurugu hizi vilevile kutotoka nje wakiwa wamevaa vito vya thamani.

Wakati huo huo waziri wa usafiishaji nchini Zambia, magari ya mizigo yasisafiri kuelekea Afrika kusini mpaka hali ya usalama itakapotengamaa.

Taarifa zinaripoti kuwa kuna malori kadhaa ya wageni yamekamatwa nchini humo huku magari mengine kadhaa yameripotiwa kuchomwa moto.

Chanzo cha picha, AFP

Siku ya jumatatu kamanda wa polisi Bheki Cele,alidai kuwa fujo hizo ni uhalifu na sio mapigano ya chuki dhidi ya wageni, na kulaumiwa kwa tamko lake .

Mamia ya watu wamekuwa wakionekana wakikimbia na kupora mali za watu katika eneo lenye shughuli za kibiashara na kuchoma moto maduka yanayoaminiwa kumilikiwa na wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika.

Ghasia hizo zilianzia katika eneo la Jeppestown, lililopo katika wilaya ya kati yenye shughuli za biashara.

Lakini zilisambaa hadi kwenye maeneo mengine kama vile Denver, Malvern, Turffontein, Tembisa na maeneo mengine ya vitongoji vya jiji la Johansburg.

Watu 41 wamekamatwa katika wimbi hilo la ghasia.

Video iliyosambazwa kwa kiasi kikubwa kwneye mitandao ya kijamii inayoonyesha magari kadhaa yaliyoungua kwa moto katika kile kinachoonekana kama mahala panapoegeshwa magari makuu kuu.

Chanzo cha picha, AFP

polisi wamefyatua mabomu ya kutoa machozi , na risasi za plastiki kujaribu kusitisha uporaji.

Msemaji wa polisi Kapteni Mavela Masondo amesema kuwa maafisa wa polisi wamekuwa wakikabiliana na moto katka jengo lililotekwa mjini Jeppestown Jumapili.

Amesema kuwa watu 3 walikufa katika moto huo, huku mtu wa nne akipata matibabu baada ya kuvuta hewa ya moshi.

"Wakati bado tunafanya uchunguzi na huduma za dharura , watu waliokuwepo karibu walianza kutumia fursa ya hali iliyopo na kupora maduka."

Luteni Generali Alias Mawela ambaye ni kamanda wa polisi wa jimbo amesema kuwa polisi wamewakamata walau watu

katika kile alichokielezea kama ghasia kubwa.

Haijabainika ni akina nani walioanzisha mashambulio hayo.

Waziri wa polisi Bheki Cele aliyetembelea eneo la ghasia amelaani ghasia hizo ambazo amesema hazina maana.

"Wakati bado tunafanya uchunguzi na huduma za dharura , watu waliokuwepo karibu walianza kutumia fursa ya hali iliyopo na kupora maduka ."

Baadhi yawatumiaji wa mitandao ya kijamii nchini humo wamekuwa wakishirikishana picha na video za ghasia hizo. Mfano Katika picha hii VHo MPHO anaonyesha picha ya eneo la Bree akisema ni krismas katika mtaa huo

Awali aliashiria kuwa kuna kikundi kikubwa cha watu kinachoelekea katikati mwa jiji na wanasomba kila wanakiona njiani:

Wengi miongoni mwa watu 41 waliokamatwa walipatikana na mali walizopora wakiwa wamezibeba mapema jumatatu alfajiri.

Washukiwa wanane walikamatwa ndani ya duka moja.

Kamishna wa polisi wa jimbo la Gauteng Luteni Generali Elias Mawela alielezea matukio haya kama ya ''ukiukaji wa sheria'' na ''yasiyo ya kibinadamu''

"Ni siku ya huzuni wakati watu wanapoamua kutumia matatizo ya wengine kwa ajili ya kuendeleza ukiukaji wa sheria au uhalifu .

Chanzo cha picha, AFP

Mawela amewaonya watu dhidi ya kuendelea kuchochea ghasia.

"wale wanaotaka kuibadilisha Gauteng kuwa mahala pa uhalifu watapatikana na watakabiliana na mkono wa sheria ," alisema.

Mashambulio dhidi ya wahamiaji si jambo geni

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Wafanyakazi wa mataifa ya nje wamekuwa wakilengwa Afrika kusini

Ghasia dhidi ya wahamiaji kutoka mataifa ya Afrika ni jambo ambalo si geni nchini Afrika Kusini, licha ya kulaaniwa na maafisa wa usalama na serikali ya nchi hiyo.

Kundi la wanaume ambao hawana ajira waliwashambulia wahamiaji kutoka Malawi wanaoishi katika mji wa Durban Afrika kusini mwishoni mwa mwezi Machi.

Ilifuata visa vingine kadhaa katika mji huo katika kipindi cha mwezi huo, jambo lililochangia viongozi kutoka vyama vitatu vikuu kushutumua mashambulio dhidi ya raia wa kigeni.