Kabendera na Azory Gwanda: Miongoni mwa visa 10 vya tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari duniani

Erick Kabendera anakabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu wa kiuchumi Tanzania
Maelezo ya picha,

Erick Kabendera anakabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu wa kiuchumi Tanzania

Waandishi habari kutoka nchini Tanzania Erick Kabendera na Azory Gwanda wametajwa kuwa miongoni mwa visa kumi vya dharura vya tishio kwa uhuru wa vyombo vya habari duniani.

Orodha inayochapishwa kila mwezi na One Free Press Coalition, iliidhinishwa na muungano wa mashirika kadhaa likiwemo TIME kwa lengo la kuwalinda waandishi habari wanaoshambuliwa kutokana na kazi zao.

Orodha ya mwezi huu Septemba imewatambua waandishi habari kutoka mataifa ya Tanzania, Saudi Arabia, Mexico, Colombia na India miongoni mwa mataifa mengine duniani waliofungwa gerezani, walionyanyaswa kwa kazi zao na wengine hata kuuawa.

Mwaka jana Time iliwatambua waandishi wanne na shirika moja la habari kwa kazi zao wakati wakikabiliwa na tishio dhidi ya uhuru wa habari.

Jamal Khashoggi, mwandishi habari maarufu aliyeangazia taarifa kubwa kwa mashirika tofauti nchini Saudia na ambaye alidaiwa kuuawa ndani ya ubalozi wa Saudia nchini Uturuki mnamo 2018, ni miongoni mwa waandishi waliotambuliwa na amejumuishwa pia katika orodha ya mwezi huu.

Chanzo cha picha, @MARIASTSEHAI/TWITTER

Maelezo ya picha,

Wanaharakati waliidhinisha kampeni katika mitandao ya kijamii Tanzania kuonesha kumuunga mkono Kabendera kufuatia taarifa za kukamatwa kwake

Kabendera anakabiliwa na mashtaka gani?

Katika nafasi ya tatu ya orodha hiyo ni mwandishi wa habari za uchunguzi Erick Kabendera kutoka Tanzania ambaye anazuiwa gerezani nchini humo kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya ubadhirifu wa kiuchumi.

Kabendera alipandishwa kizimbani Agosti 5 na kusomewa mashtaka matatu.

Katika mashtaka hayo, Kabendera anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za kitanzania.

Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.

Kwa mujibu wa mashtaka yaliowasilishwa, Kabendera anadaiwa kuyatekeleza hayo baina ya Januari 2015 na Julai mwaka huu mjini Dar Es Salaam na kwa baadhi ya makosa anadaiwa kuyafanya kwa ushirikiano wa watu ambao hawakuwepo mahakamani.

Makosa yote hayana dhamana na Kabendera anaendelea kusota rumande.

Wengine kwenye orodha hiyo mwezi huu ni :

  • Lydia Cacho kutoka nchini Mexico mwandishi mpekuzi aliyelengwa kwa mashambulio na tishio za kuuawa kwakazi yake
  • Claudia Duque mwandishi kutoka Colombia
  • Roberto Jesús Quiñones mwandishi aliyefungwa Cuba
  • Aasif Sultan mwandishi aliye gerezani huko Kashmir kwa zaidi ya mwaka
  • Azimjon Askarov aliyehukumiwa kifungo cha maisha huko Kyrgyzstan
  • Khadija Ismayilova anayekabiliwa na kunyanyaswa kutokana na kazi yake huko Azerbaijan
  • Masoud Kazemi aliyefungwa nchini Iran kwa zaidi ya miaka minne kutokana na kazi yake

Chanzo cha picha, AZORY/FACEBOOK

Maelezo ya picha,

Azory Gwanda ametoweka tangu Novemba 2017 na hajaonekana nchini mpaka hivi sasa

Azzory bado hajulikani alipo

Na katika nafasi ya tano kwenye orodha hiyo ni mwandishi habari mpekuzi kutoka Tanzania Azory Gwanda ambaye tangu Novemba 2017 hajaonekana nchini mpaka hivi sasa.

Hii ni mara ya pili Azory kujumuishwa kwenye orodha ya One Free Press Coalition. Mnamo Mei mwaka huu, muungano huo wa uhuru wa vyombo vya habari duniani uliangazia tena habari za mwanahabari huyo kwa lengo la kuishinikiza mamlaka kuwajibika kwa kutoweka kwake.

Mwandishi huyo wa Tanzania alikuwa akiifanyia kazi kampuni ya Mwananchi wakati alipotekwa katika mazingira ya kutatanisha.

Alikuwa akiripoti kesi za mauaji ya kiholela katika eneo la kibiti katika mwezi uliopelekea kupotea kwake.

Serikali imedai kuchunguza kesi yake na za watu wengine waliotoweka lakini hakuna kilichoafikiwa hadi sasa.

Kuna shinikizo kutoka kwa makundi ya haki za kibinaadamu , waandishi na mashirika ya habari kama vile kamati ya kuwalinda wanahabari CPJ zikitoa wito kwa mamlaka ya Tanzania kuipatia kipau mbele kesi ya Gwanda na kutoa majibu kuhusu hatma yake kupitia hashtag WhereIsAzory na hashtag MrudisheniAzory zikisambazwa katika mitandao ya kijamii.

Kesi yake hivi karibuni imewasilishwa katika majukwaa ya umma kuhusu haki za raia na 2018 alishinda tuzo ya 'Daudi Mwangosi' bila ya yeye kuwepo ili kuheshimu kazi yake na ujasiri.