Faru weusi ni miongoni mwa wanyama wanaoripotiwa kutoweka

Faru

Serikali ya Tanzania imepokea faru weusi tisa kutoka nchini Afrika Kusini, tukio linaloelezwa kuwa la kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kupokea idadi kubwa ya faru kwa wakati mmoja.

Naibu waziri wa maliasili na utalii, Constantine Kanyasu amesema kuwa faru hao watapelekwa katika hifadhi mbalimbali nchini Tanzania.

Idadi ya faru waliopaswa kuwasili ni 10 isipokuwa mmoja alipoteza maisha akiwa njiani kupelekwa nchini humo.

Bwana Kanyasu amesema faru hao watalindwa kwa gharama yoyote kuhakikisha hawapungui kama ilivyotokea kwenye miaka ya 1970-1980.

Mamlaka imeagiza faru hao wafungiwe vifaa maalumu vitakavyobaini mienendo yao popote watakapokuwa.

Changamoto ya ujangili ndio sababu kubwa iliyosababisha kupungua kwa faru hata kutoweka kabisa na kubaki historia.

Ujio wa faru hao ni utekelezaji wa mchakato wa kuongeza idadi yao katika makazi yao ya asili.Kanyasu amesema watu wenye nia ovu ya kuhujumu faru hao watachukuliwa hatua kali za kisheria.

Tanzania ni miongoni mwa nchi chache kabisa Afrika kuwa na makazi ya faru weusi.

Faru waliotoweka

Kwa mujibu wa Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Wanyamapori (WWF), Tanzania imepoteza takribani asilimia 98 ya faru weusi.

Hivyo miezi michache iliyopita,Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangala alizindua mpango wa taifa wa miaka mitano (2019 - 2023) wa usimamizi na uhifadhi wa faru weusi Tanzania.

Mpango huu pamoja na mambo mengine una mikakati wa kuhakikisha faru weusi wanaongezeka walau kufikia 205 ifikapo mwaka 2023.

Huwezi kusikiliza tena
Hatma ya kizazi cha faru weupe wa kaskazini ni ipi?

Kukuza utalii wa faru weusi

Kwa kuona uhitaji wa watalii kuona faru, Shirika la hifadhi za taifa nchini Tanzania, TANAPA lilianzisha utalii wa faru katika mfumo wa aina yake.

Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na ujenzi wa miundombinu ndani ya hifadhi ikiwemo barabara za kupita watalii, mabwawa ya maji kwa ajili ya wanyamapori hao na kufunga vifaa vya kisasa vya ulinzi na teknolojia ya kuwafuatilia faru.

Shirika la kimataifa la muungano wa uhifadhi duniani limeorodhesha faru weusi kuwa miongoni mwa wanyama walio hatarini kutoweka.

Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiri wa Wanyamapori Tanzania [TAWIRI], Dkt. Edward Kohi alisema mpango huo unalenga kuongeza faru weusi kwa asilimia Saba [7%], lakini Dkt. Kigwangala amesema anatamani ongezeko hilo likifikie kati ya asilimia 10-14 kwa miaka mitano ya utekelezaji mpango.