Rwanda yatia saini mkataba wa kutoa hifadhi kwa wahamiaji wa Libya

Wahamiaji nchini Libya Haki miliki ya picha Getty Images

Rwanda, Shirika la kuhifadhi wakimbizi la umoja wa mataifa na AU zimetia saini makubaliano ya kuhifadhi mamia ya wahamiaji wa kiafrika ambao kwa sasa wanashikiliwa nchini Libya.

''Kundi la kwanza lenye watu 500, kutoka pembe ya Afrika, wataondolewa, wakiwemo watoto na vijana walio hatarini,'' taarifa ya pamoja imeeleza.

Ndege za kuwasafirisha kwa wale walio tayari kwenda Rwanda wanatarajiwa kuanza safari majuma kadhaa yajayo, ilieleza taarifa hiyo.

Maelfu ya wahamiaji wanaelekea nchini Libya kila mwaka wakijaribu kufanya safari ya hatari kupitia bahari ya Mediterranea kuelekea barani Ulaya- wale wanaoshindwa hukamatwa na mamlaka na kuishia kushikiliwa kwenye vituo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya pamoja, takriban watu 4,700 wanakadiriwa kushikiliwa kwenye maeneo yenye hali mbaya ndani ya vituo hivyo.

Rwanda ilitangaza kutoa hifadhi kwa wahamiaji mwezi Novemba mwaka 2017 baada ya chombo cha habari cha CNN kuonesha video ikiwaonesha wanaume wakipigwa mnada kuuzwa kama wafanyakazi wa mashamba nchini Libya.

Watanzania waishio Afrika Kusini mashakani

Watu wawili wapoteza maisha kutokana na vurugu Afrika Kusini

Sera ya kuwapa hifadhi wahamiaji barani Afrika ni moja kati ya njia ambayo umoja wa Ulaya hutumia ili kuzuia wahamiaji wa Afrika kufika katika pwani za nchi zao.

''Wakati baadhi watanufaika kupata hifadhi katika nchi za Afrika, wengine watasaidiwa kurejea kwenye nchi ambazo ruhusa ya kupatiwa hifadhi ilitolewa, au kurejea kwenye nchi zao za asili kama ziko salama kwao kurejea.''

''Baadhi wanaweza kupewa ruhusa kubaki nchini Rwanda baada ya mamlaka kufikia makubaliano.''

Mpango kama huo upo baina ya EU na Niger, ambapo wahamiaji kutoka Libya wanahifadhiwa wakati wakisubiri ruhusa ya kuingia ulaya, Camille Le Coz kutoka taasisi ya sera za uhamiaji ameiambia BBC.

Alikubali kuwa hakuna uwazi kuhusu namna gani nchi itanufaika kutokana na makubaliano hayo, mbali na sifa ya kuonesha umoja wa waafrika wenzao.

Shirika la kuhudumia wakimbizi limesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita limewaondoa wahamiaji 4,440 kutoka Libya, nchi ambayo haijaimarika tangu aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Muammar Gaddafi alipoondolewa madarakani na kuuawa mwaka 2011.