Mahakama ya Kisutu : Freeman Mbowe na viongozi wengine wa Chadema wana kesi ya kujibu

Vongozi wa Chadema wanatarajiwa kujitetea tarehe 17 mwezi Septemba Haki miliki ya picha Mwananchi

Viongozi 9 wa Chadema akiwemo mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe wamekutwa na kesi ya kujibu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Viongozi hao wataanza kutoa utetezi wao tarehe 17 mwezi wa Septemba.

Mbowe na viongozi wengine wanane wa chama hicho wakiwemo wabunge sita wanakabiliwa na kesi ya jinai yenye mashtaka 13 yakiwemo ya uchochezi.

Uamuzi huo umetolewa Alhamisi na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

Hakimu Simba amesema amepitia ushahidi wa mashahidi nane wa upande wa mashtaka pamoja na vielelezo, kujiridhisha kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu.

"Baada ya kupitia ushahidi uliotolewa mahakama hapa na upande wa mashtaka, nimejiridhisha kuwa washtakiwa wote wana kesi ya kujibu wanatakiwa kujitetea," amesema Hakimu Simba.

Baada ya kueleza hayo Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Septemba 17, 18 na 19, 2019 na washtakiwa wataendelea kuwa nje kwa dhamana.

Awali, wakili wa Serikali mkuu, Faraja Nchimbi alieleza mahakama hiyo kuwa upande wa mashtaka wamefunga ushahidi wao.

Tayari mashahidi wanane wa upande wa mashtaka wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.

Miongoni mwa mashahidi hao ni mkuu wa upelelezi kutoka Wilaya ya Kipolisi ya Mbagala, Bernard Nyambari(42), ambaye alieleza mahakama hiyo kuwa hotuba zilizotolewa na viongozi wa Chadema katika mkutano wa kufunga kampeni ya uchaguzi mdogo wa ubunge Kinondoni, zilizofanyika katika viwanja vya Buibui ndio chanzo cha wananchi kuandamana.Gazeti la Mwananchi limeripoti.

Amedai akiwa mpelelezi wa kesi hiyo, uchunguzi waliofanya walibaini kuwa hotuba hizo ndio chanzo wananchi na viongozi hao kufanya maandamano.

Washtakiwa wengine ni mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko; Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Naibu Katibu Mkuu Taifa-Zanzibar, Salum Mwalimu; Mbunge wa Kibamba, John Mnyika; Mbunge wa Kawe, Halima Mdee; Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche; Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya na katibu mkuu wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji.

Mada zinazohusiana