UNHCR: Watoto wakimbizi 220,000 washindwa kuendelea na shule Uganda

Wakimbizi wengi nchini Uganda wametoka Jamuhuri ya kidemokrasia ya Kongo na Sudani Kusini Haki miliki ya picha AFP

Ofisi ya Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani UNHCR nchini Uganda imesema zaidi ya watoto wakimbizi 220,000 wameacha shule kutokana na ukosefu wa edha.Uganda inahifadhi wakimbizi takribani milioni 1.3, wengi wao kutoka Sudani Kusini, DRC na Burundi.

UNHCR imesema inahitaji zaidi ya dola za Marekani milioni 120 kwa ajili ya programu ya elimu kwa ajili ya wakimbizi. Mwezi Mei mwaka huu, wakati shirika lilipoomba kiasi hicho cha fedha, ilipokea 30% pekee ya fedha hizo.

Mkurugenzi wa shirika hilo ameiambia BBC kuwa kutopata elimu kunawafanya vijana kutokuwa na matumaini ya kutimiza ndoto zao.

Zaidi ya wakimbizi 300,000 wako shuleni nchini Uganda, wakisoma sambamba na watoto wengine wa jamii zinazowazunguka.

UNHCR imesema iliomba zaidi ya dola milioni 900 katika mkutano wa kuchangisha jijini Kampala mwaka 2017, lakini walipokea milioni 570 pekee.

Je, wakimbizi wa Burundi wanaohamia Uganda wametokea Tanzania?

UNHCR yasisitiza Burundi sio salama wakimbizi kurudi

Ingawa Uganda imekuwa ikisifiwa ulimwenguni kwa kuwa rafiki wa wakimbizi, mchakato huo wa kuhodhi ulitawaliwa na vitendo vya rushwa.

Mwaka 2018, ripoti ya ofisi ya ukaguzi ya umoja wa mataifa ilibaini mamilioni ya dola yalitumika kwa njia za udanganyifu, kukiwa na mikataba isiyofuata sheria na malipo ya fedha nyingi kwa ununuzi wa bidhaa na huduma mbalimbali.

Haki miliki ya picha AFP

Elimu kwa watoto wakimbizi duniani

Zaidi ya nusu ya watoto wakimbizi walio na umri wa kwenda shule milioni 7.1 duniani wanashindwa kupata elimu ingawa watoto wengi wameandikishwa shule hivi karibuni, Shirika la kuhudumia wakimbizi duniani limebaini.

Uwepo wa shule chache, upungufu wa walimu katika nchi zinazotunza wakimbizi ni miongonimwa vikwazo vinavyowakabili wanafunzi wakimbizi milioni 3.7 wenye umri kati ya miaka 5-18 ambao kwa sasa hawako shuleni, kwa mujibu wa ripoti ya UNHCR . Wengine wengi hawapo katika shule za sekondari.

Kamishna wa shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia wakimbizi Filippo Grandi, alisema kuwa uwekezaji mkubwa kwenye programu ya elimu katika nchi zinazohifadhi wakimbimbizi ni jambo la lazima ili kusaidia wakimbizi waweze kumudu kuishi na jamii nyingine katika nchi walizomo au katika jamii nyingine nje ya nchi na waweze kufanya kazi na kujitegemea.

Kwa mujibu wa umoja wa mataifa asilimia 63% pekee ya watoto wakimbizi duniani wanaandikishwa shule ya msingi, ukilinganisha na 91% wasio wakimbizi, ripoti imeeleza, huku wachache zaidi ya robo (24%) wanaingia shule za sekondari ikilinganishwa na 84% watoto wasio wakimbizi, na asilimia 3% pekee wanaenda elimu ya juu ikilinganishwa na 37% wasio wakimbizi.