Mahakama Kenya : Rastafari ni dini kama nyengine yoyote ile

Chikayzea Flanders: Maandamano yalifanyika kumuunga mkono kijana mmoja nchini Marekani ambaye alikuwa ametishiwa kutimuliwa shule kutokana na nywele zake

Rastafari ni dini kama nyengine yoyote ile na waumini wake wanafaa kuchukuliwa kama wengine , mahakama moja nchini Kenya imeamuru.

Hakimu Chacha Mwita alitoa amri hiyo katika kesi ambayo kijana mmoja alifukuzwa shule kutokana na nywele zake za rasta mnamo mwezi Januari 10.

Mahakama hiyo ilisema kwamba uamuzi wa shule ya upili ya Olympic ya kumfukuza shule kutokana na mtindo wa nywele zake ni ukiukaji wa katiba .

Wazazi wake walisema kwamba rasta hizo ni ishara ya dini yake na kwamba hawawezi kumnyoa.

''Mtoto ana haki za kikatiba kupata elimu'', Mwita alisema katika mahakama ya Milimani siku ya Ijumaa.

Ufugaji wa rasta ni njia moja ya kuabudu na ni makosa kumlazimisha kunyoa nywele hizo hatua ambayo ni kinyume na dini yake.

Kijana huyo aliandika katika stakhabadhi za kujiunga na shule kwamba yeye ni wa dini ya Rastafari. Hatua iliochukuliwa na shule hiyo inakiuka sheria.

Babake katika malalamishi yao anasema kwamba kitendo cha shule hiyo ni sawa na ubaguzi wa dini yake ya Rastafari.

Kifungu 30 {1} cha katiba kinasema kwamba kila mtu ana haki ya uhuru wa maoni, imani na dini.

Awali babake mtoto huyo aliambia mahakama alitakiwa kukata nywele zake na kwamba mawalimu wake alimlazimisha kutoa kilemba alichokuwa amevaa.

Anasema kwamba mwalimu huyo alimwambia kuchagua kati ya urembo na elimu. Hatahivyo Mwalimu mkuu wa shule hiyo alitoa picha tofauti ya kilichotokea.

Mwalimu huyo alisema kwamba mwanafunzi huyo alimwambia kwamba yeye ni Muislamu .

Kulingana na mwalimu huyo mkuu uchunguzi wa cheti cha jamii ya rastafari haikuonyesha iwapo watoto pia ni miongoni mwa wafuasi wa dini hiyo.

Alisema kwamba usimamizi wa shule ulimruhusu mwanfunzi huyo kuingia darasani siku aliyojiunga na shule hiyo lakini akalazimishwa kufuata sheria siku iliofuatia.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii