Robert Mugabe kuzikwa na familia yake katika uwanja wa mashujaa

Maelfu ya raia wa Zimbabwe walikusanyika mjini Harare kuushuhudia mwili wa Mugabe ukiwasili Haki miliki ya picha Getty Images

Mwili wa aliyekuwa raisi wa Zimbabwe Robert Mugabe utazikwa kifamilia katika viwanja vya mashujaa, karibu na mji wa Harare, mpwa wake ameiambia BBC.

Leo Mugabe, msemaji wa familia, amesema mazishi hayatafanyika siku ya Jumapili kama ilivyokuwa ikitarajiwa.

Badala yake, mwili wake utapelekwa katika kijiji alichozaliwa Kutama ambapo machifu na wazazi watapata nafasi kufanya shughuli zao za kimila .

Baaadae siku ambayo haijatajwa mwili wa Mugabe aliyefariki juma lililopita akiwa na miaka 95 utazikwa katika uwanja wa mashujaa.

Eneo hilo ndilo serikali ililokuwa inalitarajia kumuhifadhi kiongozi huyo wa zamani.

Na inaonekana kuwa wamefikia muafaka baada ya siku kadhaa za mjadala mkali.

Kumekuwa na mvutano kati ya familia ya Mugabe na wale waliomshinikiza hayati Mugabe kuondoka madarakani kwa mapinduzi mwezi Novemba mwaka 2017.

Awali, Familia ya Robert Mugabe ilisema imeshutushwa kwa kutoshauriwa na serikali kuhusu mipango ya mazishi ya aliyekuwa rais wa Zimbabwe.

Mwili wa Mugabe kuwasili leo Zimbabwe

Mzozo watokota kuhusu mazishi ya Mugabe

Mugabe, alifariki wakati alipokuwa nchini Singapore akipata matibabu.

Mwili wake unatayarishwa kulazwa ili kupewa heshima za mwisho kitaifa katika uwanja wa soka katika mji mkuu wa Zimbabawe, Harare.

Familia yake na serikali zinatofuatiana kuhusu sehemu atakapozikwa Mugabe.

Familia ya Mugabe inasemekana kuwa na uchungu kwa namna Mugabe alivyotimuliwa na aliyekuwa mshirika wake Mnangagwa miaka miwili iliyopita.

Mugabe alimfuta kazi Mnangagwa mnamo 2017, katika kile ambacho wengi waliamini ni njia ya kumtayarisha Bi Mugabe kumrithi.

Mugabe alikuwa kiongozi wa kwanza wa Zimbabwe baada ya taifa hilo kupata uhuru mnamo 1980. Alishikilia madaraka kwa takriban miongo minne kabla ya kutimuliwa katika mapinduzi mnamo 2017.

Haki miliki ya picha Getty Images

Kauli kuhusu nchi yake dhidi ya Ulaya

Baadhi ya maneno ambayo Mugabe aliyowahi kuyasema dhidi ya bara la ulaya kuhusu nchi yake.

"Zimbabwe ni huru kwa sababu watu wake wako huru na watu wake wanapaswa kuwa huru daima"

"Sisi si watu wa ulaya, hatujawahi kuomba hata sehemu ndogo ya ulaya, Blair kaa na Uingereza yako na mimi niache nibaki na Zimbabwe yangu"

Awali Mugabe alisifiwa kwa kupanua sekta ya afya na elimu kwa weusi walio wengi, baadaye alitumia ghasia dhidi ya wapinzani wake na kuongoza uchumi wa taifa hilo ulioanguka vibaya.

"Hawawezi kuanzisha demmokrasia hapa, sisi tumeanzisha demokrasia"

"Hii ni ardhi ya mtu mweusi hivyo ni mtu mweusi ndiye mwenye haki ya kuamua nani akae na nani asikae"

"Tuna ardhi yetu na katika ardhi yetu ndio tutapata fedha"

Kimataifa mpiganaji huyo wa zamani alionekana kama dikteta kufuatia hatua ya jeshi lake kuwashambulia wapinzani wake mbali na kunyakuwa ardhi kutoka kwa wakulima wachache weupe ili kupiga jeki umaarufu wake miongoni mwa wapiga kura.

Uongozi wake umezua mjadala mkubwa tangu kifo chake.

Alikuwa maarufu miongoni mwa wapiga kura wengi hata katika kipindi chake cha hivi karibuni alipong'atuliwa mamlakani.

Aliondolewa mamlakani alipomfuta kazi makamu wake wa rais Emmerson Mnangagwa ambaye baadaye alikuwa raisi wa taifa hilo.

Mada zinazohusiana