Shambulio la vituo vya mafuta Saudia: Masalio ya silaha 'yanathibitisha Iran imehusika'

Debris from drones and missiles that Saudi Arabia says prove Iranian involvement in oil installation attacks. Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Saudia inasema muelekeo wa mashambulio unaonyesha makombora hayawezi kuwa yametoka Yemen

Wizara ya ulinzi Saudi Arabia imeonyesha inachosema ni masalio ya ndege zisizo kuwa na rubani na makombora yanayothibitisha kuhusika kwa Iran katika mashambulio dhidi ya vituo vyake viwili vya mafuta mwishoni mwa juma.

Imesema ndege 18 zisizokuwa na rubani na makombora saba yalifyetuliwa kutoka muelekeo unaoonyesha kwamba hayawezi kuwa yanatoka Yemen.

Waasi nchini Yemen wanaoiunga Iran mkono wamesema walihusika na mashambulio hayo.

Iran imekana kuhusuika kwa namna yoyote na kuonya kwamba italipiza dhidi ya shambulio lolote dhidi yake.

Marekani imeendelea kuituhumu Iran kuhusika na mashambulio hayo. Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema baada ya kuwasili Saudia hapo jana Jumatano kwamba ilikuwa ni 'hatua ya kivita'.

Rais Donald Trump amesema Marekani "ina njia nyingi" za kujibu.

"Kuna njia kuu, na kuna hatua nyingine zilizo chini ya hilo," amesema. "Na tutaona. Tupo katika nafasi yenye nguvu."

Nini kilichoibuka katika utafiti wa Saudia?

Ushahidi uliwasilishwa katika kikao cha wizara ya ulinzi, ambapo masalio ya ndege zisizokuwa na rubani (UAV) na makombora kutoka kwenye mashambulio hayo yaliwekwa wazi.

Msemaji wa wizara ya ulinzi kanali Turki al-Malki amesema ushahidi unaonyesha mashambulio hayo yaliidhinishwa kutoka kaskazini na “bila shaka yalifadhiliwa na Iran”.

Hatahivyo, kanali Malki amesema Saudia ingali "inashughulika kubaini eneo maalum ambako mashambulio yalitoka".

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kanali Malki aliwasilisha ramani, picha na video kutoka kwenye hsmabulio hilo Jumamosi

Miongoni mwa vifusi vilivyokusanywa ni pamoja na kilichosemekana kuwa ni bawa la ndege isiyokuwa na rubani aina ya Delta ya Iran.

Kanali Malki amesema: "Data iliokusanywa kutoka kwenye kompyuta inaonyesha ni ya Iran."

Amesema ndege hizo 18 zilipeperushwa katika kituo cha mafuta cha Abqaiq na makombora saba yakafyetuliwa katika maeneo yote yaliolengwa.

Makombora manne yalifyetuliwa dhidi ya kituo cha mafuta cha Khurais na mengine matatu yalianguka karibu na Abqaiq.

Kanali Malki amesema taarifa kuhusu maeneo ambako makombora hayo yalikotoka haiwezi kutolewa kwa sasa lakini punde watakapobainisha hilo watalitangaza.

Amesema: "Licha ya jitihada nzuri kutoka kwa Iran kufanya ionekane hivyo, ushirikiano wake na maeneo ya karibu kuunda hoja hii ya uongo in wazi."

Ameyataja mashambulio hayo kuwa "shambulio kwa jumuiya ya kimataifa… Wale waliohusika wanapaswa kuwajibishwa kwa hatua zao".


Hatua gani zinafuata?

Licha ya kwamba Marekani imeweka wazi kuwa inaamini Iran imehusika na mashambulio hayo, Rais Trump ameonekana kwa ujumla kusita kuhusika katika hatua za kijeshi.

Hapo jana Jumatano alisema ni "rahisi sana" kuingia katika mzozo wa kijeshi lakini amependekeza funzo jingine kutoka mashariki ya kati limedhihirisha hilo lilikuwa gumu.

Kabla ya kikao hicho cha wizara ya ulinzi Saudia kufanyika, Trump alitangaza kwamba ameagiza wizara ya fedha "kuongeza vikwazo vya Marekani" dhidi ya Iran kufuatia mashambulio hayo.

Trump amesema kutakuwa na taarifa zaidi katika saa 48. Vikwazo vya sasa ni vipana vilivyonuiwa kupunguza usafirishaji wa mafuta ya Iran na kudhoofisha uchumi wa taifa hilo.

Pompeo baadaye alikutana na mwanamfalme Mohammed bin Salman, kujadili muelekeo wa hatua kuhusu suala hilo.

Wataalamu wa Umoja wa mataifa wameelekea Saudia kufanya uchunguzi kuhusu mashambulio hayo, Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Antonio Guterres amesema, akionya kuhusu "athari mbaya" za makabiliano makubwa.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii