Mashambulio ya vituo vya mafuta Saudi Arabia: Je kunaweza kuwa na vita?

US Secretary of State Mike Pompeo shakes hands with Saudi Crown Prince Mohammed bin Salman in Jeddah (18 September 2019) Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Waziri wa mamabo ya nje wa Marekani Mike Pompeo amesema mashambulio ya Jumamosi yalikuwa ni "hatua ya kivita"

Saudi Arabia inasema ina ushahidi unaoonyesha kuwa Iran ilifadhili mashambulio ya Jumamosi ya ndege zisizokuwa na rubani na makombora yaliotumika dhidi ya vituo vyake vya mafuta na kuitaka jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua.

Swali hapa ni je kunaweza kuwa na vita?

Kiwango cha mashambulio hayo inamaanisha kuwa Saudia haiwezi kupuuzia kilichotendeka na uamuzi wake kuitambua Iran kama mtuhumiwa unaushurutisha ufalme huo kujibu.

Huenda Saudia ikasubiri mpaka kundi la wataalamu kutoka Umoja wa mataifa watakapokamilisha uchunguzi wao kuhusu tukio hilo.

Licha ya kwamba wataalamu hao huenda wakaishia kuwa na jibu sawiya - kwamba mashambulio hayo hayawezi kuwa yametekelezwa pasi usaidizi na muongozo wa Iran - utaratibu huo utaipatia Saudia muda wa kufikiria hatua ya kuchukua.

Kwa Iran, haisaidii kukana.

Saudi Arabia na washirika wake wanaamini taifa hilo limechukua hatua ya ziada katika kumshawishi rais wa Marekani Donald Trump kulegeza vikwazo vya uchumi alivyoviidhinisha upya wakati alipojitoa katika makubaliano ya nyuklia na Iran mwaka jana na kutaka majadiliano kwa makubaliano mapya.

Haki miliki ya picha Reuters

Viongozi wa Iran wanatumai hatari ya eneo kuingia katika vita kutayafanya mataifa yenye nguvu duniani kutambua kwamba vikwazo hivyo vinaelekea kuzusha janga.

Walitumai kwamba mpango wa rais wa Ufaransa Emmanuel Macron kutoa mkopo wa $15bn kwa Iran, ili kwa upande wake itii makubaliano ya nyuklia na kusitisha shughuli zake za vurugu kieneo utazaa matunda. Lakini mpango huo haujaidhinishwa na Trump.

Siku ya Jumatano rais huyo wa Marekani ameitaka wizara ya fedha Marekani iongeze vikwazo dhidi ya Iran. Huenda basi Iran ikawa imeongeza chumvi kwenye kidonda.

Mashambulio ya kiwango hiki hayawezi kuwa yamefanyika pasi idhini ya kiongozi mkuu wa kidini nchini, Ayatollah Ali Khamenei.

Alitoa hotuba wiki hii ambapo hakutaja hata mara moja mashambulio katika vituo vya mafuta nchini Saudi Arabia, au hatari ya kuzuka vita wakati wowote.

Badala yake alichukua fursa kukataa kwa mara nyingine uwezekano wowote wa kufanyika mazungumzo na maafisa wa Marekani katika kiwango chochote ili mradi vikwazo vya Marekani vinaendelea kuwepo dhidi ya taifa hilo.

Lakini punde sio punde Ayatollah Khamenei huenda akabadili msismamo wake na akubali mazungumzo hayo, wakati viongozi wa msimamo wa kadri nchini humo wakiendelea kulishinikiza hilo kimya kimya.

Iran inasafirisha kiasi kidogo cha mafuta, kipato chake kinakauka na inadhaniwa akiba yake ya fedha inawatosha kwa miezi kadhaa.

Kushuka kwa thamani ya sarafu kumeshinikiza gharama ya maisha kwa 40% na kufanya maisha kuzidi kuwa magumu kwa raia nchini.

Kwahivyo basi je Saudi Arabia itachukua hatua za kijeshi kuikanya Iran? Huenda ikaeleweka iwapo Ufalme utalisusia hilo.

Iran ina jumla ya watu milioni 80 ikilinganishwa na watu milioni 33 wanaoishi Saudi Arabia.

Iran ina maelfu ya makombora, inayohatarisha vituo vya mafuta , kambi za jeshi na maeneo ya kuishi watu Saudia. Kwa ulinganisho, Saudia ina mamia ya makombora ya kichina na kiasi fulani tu cha makombora ya ulinzi.

Kwa kadirio, Saudi Arabia ina idadi sawa ya ndege za kivita kama Iran. Lakini ndege zake ni za kisasa na uhudumu wake ni bora zaidi huku za Iran zilkiwa ni za zamani na zisizoaminika.

Iran ina wafuasi wake kieneo na pia miongoni mwa kundi la wachache la madhehebu ya Shia nchini Saudi Arabia.

Saudia pia imehusika katika vita nchini Yemen dhidi ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.

Lakini vita vya moja kwa moja dhidi ya Iran vitakuwa bila ya shaka ni kuhusu nguvu ya angani na uwezo wa makombora. Hakuna upande utakaoibuka mshindi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ayatollah Ali Khamenei anasema Marekani inataka kuipigisha Iran magoti

Licha ya kwamba kuna vikosi vya Marekani, ndege na meli zinazotumwa katika eneo la Ghuba, rais Trump anaonekana hana azma ya kutaka kuhusika katika mzozo wa kivita.

Vyombo vya Marekani na kambi zinaweza kuwa katika hatari ya kushambuliwa na makombora ya Iran na kiasi cha khumusi moja ya mafuta duniani hupita katika mfereji wa Hormuz.

Huenda Trump ana wasiwasi kuhusu athari ya kampeni yake ya kuchaguliwa tena kutokana na kupanda kwa kiwango kikubwa gharama ya mafuta nchini mwake.

Kwa Saudi Arabia, Uungwaji mkono wa jeshi la Marekani ni muhimu. Lakini Trump anataka kuongoza katika kuijibu Iran na pia kupata faida kwa kutoa usaidizi wa Marekani.

Huenda pia Saudi Arabia ikataka washirika wake kieneo - Umoja wa falme za kiarabu na Bahrain - kuwa sehemu ya jibu hilo.

Huenda Marekani ikaorodhesha usaidizi wa kisiasa na kidiplomasia wa washirika wake wa Ulaya.

Hatahivyo wanaona kupamba moto huku ni matokeo ya moja kwa moja ya uamuzi wa Trump kujitoa katika mkataba wa nyuklia.

Wakati huo huo, watu wenye mrengo mkali Iran huenda wanatafakari iwapo mpango wao unaiongoza nchi hiyo kuingia vitani na katika uharibifu, badala ya kuishia kuondolewa vikwazo.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii