Hamad Masauni: Waziri ataka wapenzi wa jinsia moja kukamatwa Zanzibar

Wapenzi wa jinsia moja

Naibu waziri wa mambo ya ndani Tanzania Mhandisi Hamad Masauni ameliagiza jeshi la polisi visiwani humo kuwakamata wanaoendesha maswala ya Ushoga na unyanyasaji wa kijinsia.

Amesema kwamba swala hilo ni kinyume na misingi ya dini zote ambazo Watanzania na Wazanzibare wanaamini.

''Ni jambo la kusikitisha kuona kwamba baadhi ya watoto wa kiume wameharibiwa na baadaye tunaona ongezeko la wimbi la vijana wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja'', alisema.

''Natoa wito kwa jeshi la polisi kuhakikisha kwamba wale wote ambao wamekuwa na desturi ama utamaduni wa kushiriki ama kuhamasisha vitendo hivi vibovu na viovu katika nchi yetu kuhakikisha kuwa wanachukuliwa hatua kali'', aliongezea.

Amesema kwamba mbali na vijana kujihusisha katika vitendo hivyo pia wamekuwa wakihusika pakubwa katika ulanguzi wa mihadarati katika maeneo hayo.

Amesema kwamba visiwa hivyo vinakumbwa na changamoto hizo ambazo anadai kwamba zinachafua taswira na heshima ya visiwa hivyo viwii mbali na kusababisha mmomonyoko wa maadili katika visiwa hivyo viwili.

Hatahivyo amesisitiza kwamba ili kukomesha tabia kama hizo ni sharti wananchi wote kuwa kitu kimoja katika kuyakemea na kuyazuilia maovu hayo yasiendelee.

Tayari shirika moja linaloshughulikia kuwabadilisha tabia wapenzi wa Jinsia moja mbali na kuwapa msaada wa kiafya wanaume hao limebuniwa .

Shirika la IYAHIZA linahusika na mapambano ya virusi vya ukimwi kwa vijana visiwani Zanzibar na miongoni mwa miradi wanayoshugulikia ni kuyasaidia makundi maalum, ikiwemo wanaume wanaojihusisha na Mapenzi ya Jinsia Moja.

Mbinu mbalimbali hutumiwa, kwanza hufuatwa kisha kupewa ushauri na kupimwa ikiwa wana maambukizi ya magonjwa yoyote ikiwemo virusi vya Ukimwi.

Ingawa kundi hili limekua likijificha kutokana na kuwa hawaruhisiwa kisheria na wanaweza kufungwa hadi miaka 30 jela, imekua vigumu kwa Shirika la IYAHIZA kuwapata hivyo wamekua wakitumia mbinu ya kutumia wale walioacha ili kuwatambua ambao bado wanajihusisha na vitendo hivyo.

Mwaka 2017, Mamlaka ya kisiwani Zanzibar iliwakamata watu 20 wanaotuhumiwa kushiriki katika mapenzi ya jinsia moja, kisa hicho kikitokea wakati wa msako dhidi ya watu wa jinsia moja katika kisiwa hicho cha Afrika mashariki.

Wakati wa msako huo Wanawake 12 na wanaume 8 walikamatwa kufuatia uvamizi wa polisi katika hoteli moja ambapo washukiwa hao walikuwa wakishiriki katika warsha kulingana na afisa mkuu wa polisi Hassan Ali.

Chanzo cha picha, DEA / G. COZZI

Mapenzi ya jinsia moja ni uhalifu nchini Tanzania na ngono miongoni mwa wanaume ni hatia inayovutia kifungo cha kati ya miaka 30 jela na kifungo cha maisha.

Mwaka 2016 mwezi Februari , serikali ilisitisha huduma za vituo 40 vya afya vya kibinafsi kwa madai kwamba vilikuwa vikitoa huduma kwa wapenzi wa jinsia moja.

Lakini vijana hawa ilikuaje hadi wakaingia katika mapenzi ya jinsia moja?

Vijana ambao wapo katika mradi huo, wengi wanasema kuwa waliingia katika tabia hiyo kutokana na ushawishi wa vijana wenzao.

Lakini kijana mmoja ambae jina lake limehifadhiwa anasema kuwa shemeji yake ndiye aliyekua akimfanyia vitendo hivyo.

''Nilikua naishi na dada yangu, aliyeolewa huko mkoani mwanza, sasa shemeji alikua akinifanyia vitendo hivi mara kwa mara, alikua akiniingilia kinyume na maumbile, na ananiambia nisiseme kwa mtu yoyote, mimi nilikua naogopa, sasa ikaendelea hadi nikazoea, nilikuja kusema nyumbani nikafukuzwa''

Mbali na kuwa shirika hili linataoa msaada wa kiafya na mabadiliko ya tabia, wamesisitiza kuwa hawashawishi kwa namna yoyote watu kujihusisha na vitendo hivyo.

Mapenzi ya jinsia moja miongoni mwa wanaume ni kosa la jinai nchini Tanzania na hatia yake inaadhibiwa kwa kifungo cha kati ya miaka 30 au maisha jela.