Jamii ya Wahadzabe Tanzania yajishindia tuzo ya kimataifa kwa uhifadhi wa mazingira

Wahadza Haki miliki ya picha Jeff Leach, Chuo kikuu cha King's College London
Image caption Jamii ya Wahadzabe hula matunda ya msituni

Jamii ya wawindaji ya Wahadzabe Tanzania inatarajiwa kupokea tuzo mjini New York kwa jitihada zake kukabiliana na umaskini kupitia uhifadhi wa mazingira na matumizi ya uhai anuai.

Jamii hiyo iliopoteza 90% ya ardhi yao kwa wakulima na wafugaji wanyama inatuzwa hii leo mjini New York Marekani katika tuzo ya shirika la Umoja wa mataifa UNDP kwa kutunza vyema misitu na kuzuia mabadiliko ya tabia nchi.

Tuzo hiyo Equator Prize 2019 inakuja ikiwa ni siku moja baada ya kufanyika kwa mkutano wa mabadiliko ya tabia ya nchi wa Umoja wa Mataifa, unaosisitiza viongozi wa nchi kujitoa katika kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi.

Kwa ushikirikiano na shirika la kijamii - Carbon Tanzania, walifanikiwa kuratibu mbinu ya kufaidika kutokana na mazingira asili.

Waliidhinisha mradi wa kutoza malipo kifedha kwa kila kunapofanyika uteketezaji wa mbao katika misitu iliyo kwenye maeneo yao, shughuli ambayo huchangia utoaji wa hewa chafu ya mkaa au Carbon dioxide.

Na ni mradi huo sasa uliowapatia ushindi wa tuzo ya mwaka huu ya Equator Prize.

Haki miliki ya picha Jeff Leach, chuo kikuu cha King's College London
Image caption Shughuli ya kuvuna asali, ikiwa ni sehemu ya vitu wanavyokula Wahadzabe

Tuzo hii ina maana gani kwa Wahadza?

Marc Baker, ni mwanzilishi wa shirika la Carbon Tanzania, linalotekeleza miradi ya utunzaji wa misitu katika vijiji mbalimbali nchini Tanzania anaeleza kwamba kando na ushindi huu, jamii hiyo inasaidia dunia nzima katika jitihada za kupunguza uharibifu unaotokana na mabadiliko ya tabia nchi.

Ameeleza kwamba shirika hilo husaidia kwa kuratibu ununuzi au malipo hayo hewa hiyo ya Carbon , ambao baada ya kutoa malipo shirika la carbon tanzania hupeleka fedha kwa jamii.

Fedha hizo baada ya zinagawanywa, 'Kijiji kinapata asilimia, jamii wanapata kutumia kwa ajili ya kusaidia watu kwa elimu, hospitali na vitu mbali mbali kule kijijini' baker ameielezea BBC Swahili.

Kufikia sasa mradi huo umeinufaisha jamii hiyo , ilio masikini kwa zaidi ya $300,000 kwa mujibu wa shirika hilo la Carbon Tanzania.

Kiongozi mmoja kutoka jamii hiyo anatarajiwa kuipokea tuzo hiyo hii leo Marekani inayotolewa na UNDP kwa miradi au jitihada katika kuidhinisha suluhu za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na kuhimiza maendeleo endelevu.

Haki miliki ya picha Jeff Leach, chuo kikuu cha King's College London
Image caption Wahadzabe ni moja kati ya makabila yaliyobaki duniani yanayoendeleza shughuli za uwindaji,

Wahadzabe ni kina nani?

Jamii ya Wahadzabe ni moja kati ya makabila yaliyobaki duniani yanayoendeleza shughuli za uwindaji, inadhaniwa kuwa jamii hii imeishi kaskazini mwa Tanzania, ikila matunda na mizizi, na aina mbalimbali za wanyama kwa miaka 40,000.

Ingawa Wahadzabe ni wachache sana - wanaume, wanawake na watoto 1000 hivi, kufikia mwaka 2017 inaaminika kuwa wale wanaotegemea maisha ya uwindaji pekee ni kati ya 200 na 300, ambao hawalimi wala kufanya aina yeyote ya kilimo.

Jamii hii inawaona wakulima kama wa kushangaza.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii