Mohamed Ali: Raia wa Misri aliyeanzisha maandamano nchini humo akiwa mafichoni

Picha ya Mohamed Ali Haki miliki ya picha Photo supplied
Image caption Mohamed Ali amechapisha kanda za video mitandaoni akimshutumu rais al-Sisi kwa ufisadi

Wakati mamia ya raia wa Misri walipofanya maandamano wakimtaka rais Abdul fattah al Sisi kung'atuka mamlakani katika miji kadhaa nchini Misri siku ya Ijumaa , lilionekana jambo la kushangaza kwa wengi waliokuwa wakifuatilia tukio hilo.

Lakini mtu mmoja , Mohamed Ali , alitarajia maandamano hayo na anasifika kwa kuyaandaa.

Katika kipindi cha wiki chache , mfanyabiashara huyo mwenye umri wa miaka 45 amekuwa mtu maarufu nchini Misri , akionekana kama mmojawapo ya wakosoaji wakubwa wa rais wa taifa hilo kufuatia msako wa miaka ya hivi karibuni ambao umekuwa ukilenga kuwanyamazisha wapinzani.

Tangu mapema mwezi Septemba , bwana Ali amekuwa akichapisha kanda za video za kila siku kutoka maficho yake nchini Uhispania, akimshutumu rais Sisi na wakuu wa jeshi kwa kufanya ufisadi.

Kanda zake za video zimechochea msururu wa alama za reli katika mitandao ya kijamii ambazo zinaonyesha hasira miongoni mwa raia wa Misri na kusababisha maandamano yaliofanyika wikendi.

Kiwango cha umaarufu wa bwana Ali kilimshinikiza bwana Sisi kujibu madai aliokuwa akiyawakilisha , akiyataja kuwa uongo na kuwakemea raia wa Misri kwa kuitazama kanda hiyo ya video.

Akijibu taarifa ya bwana Sisi bwana Ali aliapa kumtimua madarakani.

Je Bwana Mohamed Ali ni nani?

Mmiliki wa zamani wa biashara ya kibinafsi iliojulikana kama Amlaak, Mohamed Ali ana historia ya kufanya kazi katika miradi ya jeshi la Misri.

Pia anajulikana kwa kuwa muigizaji ijapokuwa kwa muda mfupi - pia akiwa na sifa za mtu asiyejulikana licha ya kushiriki katika filamu ya The Other Land - kabla ya kuuza mali yake na kuhamia Uhispania.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mamia ya waandamanaji walikongamana katika bustani ya Tahriri siku ya Ijumaa

Umaarufu wake uliongezeka kufuatia kutolewa kwa msuruu wa kanda za video ambapo alidai kuwa na habari za ndani kuhusu jeshi la Misri hususan kuhusu utumuzi wa fedha za serikali.

Babake Ali Abdul Khalek , alikuwa bingwa wa kuinua mizani kabla ya kuanzisha biashara ya kandarasi yake na ile ya wanawe wawili, akiwemo Mohamed.

Katika mahojiano na mtangazaji anayeunga mkono serikali Ahmed Moussa , Abdul Khalek alionekana kumshutumu mwanawe huku akipinga madai yake akidai kwamba mali ya familia yake inatokana na jeshi.

Je anadai nini?

Bwana Ali anayedai kulidai jeshi mamilioni ya pauni za Misri kama mashahara ambao hakulipwa anasema kwamba alitoroka taifa hilo kutokana na hofu kufanyiwa kisasi na mamlaka baada ya kulikabili jeshi.

Mazoea yake na jsehi kuhusu miradi ya ujenzi kupitia kazi yake yalimpatia sifa miongoni mwa watazamaji wa Misri huku wengi wakimsifu kama mfichuaji.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Video za bwana Ali zimeungwa mkono na raia wengi wa taifa hilo

Pia amemshutumu bwana Sisi kwa ufujaji wa fedha za serikali kutengeza majumba ya rais pamoja na yale ya kifahari, huku akidai kwamba miradi ilikuwa ikifanyiwa majenerali katika jeshi.

Ameendeleza kupaza sauti yake dhidi ya bwana Sisi, huku mara nyengine akisema kwamba sio wanajeshi wote ni wafisadi.

Katika kanda zake za video za hivi karibuni, alimtaka waziri wa ulinzi Mohamed Zaki kumkamata rais huyo huku akidai kwamba amepokea ujumbe wa kumuunga mkono kutoka kwa jeshi na maafisa wa polisi.

Tangu alipotoa kanda hizo za video, wakili mmoja amemshutumu bwana Ali kwa uhaini na amekabiliwa na ukosoaji kutoka kwa vyombo vya habari nchi humo.

Kwa nini raia wa Misri waliitikia wito wake?

Madai ya bwana Ali kuhusu ubadhirifu wa fedha za serikali yalionekana kuungwa mkono na raia wengi wa Misri ambao wanaendelea kuzorota kiuchumi licha ya hatua ya serikali kupunguza matumizi yake ili kulipa madeni.

Mwezi Julai , takwimu za serikali zilibaini kwamba asilimia 32.5 za rais wa Misri walikuwa wakiishi katika umasikini, ambao umepanda hadi asilimia 27.8 mwaka 2015.

Na licha ya shinikizo za kiuchumi , uwezekano wa kuwepo kwa maandamano haukuwepo kutokana na uchovu mbali na hatua zitakazochukuliwa kufuatia upinzani wowote wa serikali.

Lakini kwa mshangao wa wengi maandamano madogo yalifanyika nje na karibu na bustani ya Tahrir pamoja na miji mingine yakivunja hofu iliokuwa na raia wengi iliojengwa na utawala wa rais Sisi.

Madai ya bwana Ali yaliohusisha ufahamu wake wa maswala ya ndani pamoja na uzungumzaji wake ulimtenga na upinzani wa Kiislamu pamoja na wanaharakati ambao mahitaji yao yalilenga sana haki badala ya faida za kiuchumi kwa raia.

Zaidi, Ali aliwahakikishia Wamisri watakuwa salama iwapo watafanya maandamano huku kukiwa na sherehe ya mechi ya kandanda siku hiyo ambayo huenda ilichangia zaidi kufanyika kwa maandaano hayo.

Yalipokuwa yakifanyika mamia ya watu walikamatwa baada ya waandamanaji kuingia katika barabara kuu za miji.

Kabla ya wito huo wa bwana Ali, hasira ilikua imepanda miongoni mwa raia nchini humo kutokana na mabadiliko ya kiuchumi ambayo yamewakabili raia.

Hayo ni pamoja na kupunguzwa kwa thamani ya sarafu ya Misri 2016 ambayo ilisababisha kupanda kwa bei za bidhaa.

Bwana Sisi ametetea hatua yake ya kupunguza matumizi serikalini akisema itazaa matunda baadaye.

Katika hotuba yake , alisema, ''Sisi wamisri ni watu masikini sana'' na kutoa wito kwa raia nchini humo kuchangisha masalio yao kwa wakfu wake wa maisha.

Licha ya kukana madai ya ufisadi yaliowasilishwa na Ali, bwana Sisi alionyesha msimamo wake wakati alipokuwa akijibu kanda hiyo ya video, akikiri kuhusu ujenzi wa majumba hayo ya rais na kusema kwamba ataendelea kufanya hivyo kwa manufaa ya Misri.

Thibitisho hilo kutoka kwa Sisi kwamba mamilioni ya fedha yametumika katika miradi ya majumba hayo na miradi mingine, pamoja na jibu la bwana Ali lilitosha kuwashinikiza watu wachache kutoa hasira zao katika maandamano.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii