Uchunguzi dhidi ya Trump: Mfichua siri ni 'afisa wa CIA'-Ripoti zinasema

US President Donald Trump and Ukrainian President Volodymyr Zelensky meet in New York on September 25, 2019, Haki miliki ya picha AFP

Mfichua siri ambaye ushahidi wake umesababisha uchunguzi wa dhidi ya Rais Trump ni afisa wa shirika la ujasusi la Marekani CIA, vinaripoti vyombo vy ahabari vya Marekani.

Afisa huyo ambaye jina lake halijatajwa aliwahi kufanya kazi katika Ikulu ya House, vinasema vyombo kadhaa vya habari nchini humo..

Mfichua siri huyo amesema maafisa wa ngazi ya juu wa Ikulu ya White House walijaribu kuficha vielelezo vya mawasiliano ya simu baina ya rais Donald Trump na rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky.

Bw. Trump anataka kujua ni nani aliyempatia taarifa mfichua siri huyo,akiongeza kuwa aliyefanya hivyo ''anakaribia kuwa jasusi".

Trump anashutumiwa kwa kutafuta msaada kutoka nchi ya kigeni kwa minajili ya kumchafua kisiasa mpinzani wake Joe Biden na kutumia msaada wa kijeshi kama nyenzo ya kutaka matakwa yake yatimizwe.

Bw Biden ndiye kinara wa mbio za tiketi ya kugombea urais 2020 kwa chama cha Democrats.

Haki miliki ya picha EPA

Bwana Trump amekiri kuwa alimzungumzia Joe Biden na Bwana Zelensky, na kuwa alizuia msaada wa kijeshi kwa nchi hiyo wa thamani ya dola milioni 400.

Lakini amekanusha kuwa alifanya hivyo kama shinikizo kwa Ukraine ili kumchunguza Biden.

Mfichua siri ni nani?

Hakuna taarifa za kina kumhusu lakini wakili wake ameonya kuwa jaribio la kubaini ni nani litamweka hatarini.

Magazeti ya New York Times, Washington Post, na shirika la habari la Reuters yanadai kuwa mfichua siri huyo ni afisa wa CIA.

Mazungumzo baina ya Trump na Zelensky yalikuwaje?

Kwa mujibu wa mukhtasari uliotolewa jana na Ikulu ya White House, Trump alimwambia Zelensky juu ya namna ambavyo Joe Biden akiwa makamu wa rais alishawishi Ukraine kumtimua kazi mwendesha mashtaka wake mkuu, Viktor Shokin mwaka 2016.

Ofisi ya Shokin ilifungua jalada la uchunguzi dhidi ya Burisma, kampuni ya gesi asili ambayo mwana wa Joe Biden, Hunter alikuwa ni mjumbe wa bodi yake.

Nchi kadhaa za magharibi pia zilikuwa zikishinikiza Bw Shokin atimuliwe kazi kwa madai alikuwa akivumilia vitendo vya rushwa.

"Nimesikia mlikuwa na mwendesha mashtaka ambaye alikuwa ni mzuri kweli na alifutwa kazi kwa njia ya uonevu. Watu wengi wanalizungumzia jambo hilo," Trump ananukuliwa akisem kwenye mazungumzo hayo na kuongeza: "Kitu kingine, kuna mjadala mkubwa kumhusu mtoto wa Biden, kuwa baba yake alizuia waendesha mashtaka na watu wengi wanataka kujua undani wa hilo, so chochote unachoweza kufanya na Mwanasheria Mkuu (wa Marekani) litakuwa jambo jema.

"Biden alikuwa akijitamba kuwa amezuia uchunguzi angalia utakachokifanya hapo...ni jambo baya sana kwangu."

Zelensky anaripotiwa kujibu: "Tutalishughulikia hilo na tutafanyia kazi uchunguzi wa kesi hiyo.

"Juu ya hilo, pia ningeomba kama una taarifa zozote za ziada pia tupatie, zitatusaidia sana."

Akimshukuru Trump, bw Zelensky alisema kuwa alikaa kwenye jumba lake la jijini New York, Trump Tower, mara ya mwisho alipozuru nchini humo.

Zelensky amesema nini?

Haki miliki ya picha EPA
Image caption Bw Zelensky na Trump wamekutana Jumatano jijini New York Jumatano

Raisi huyo wa Ukraine amesema alidhani kuwa maelezo ya Trump pekee katika mawasiliano hayo ndiyo ambayo yangechapishwa.

"Nadhani, wakati mwengine, mawasiliano ya simu baina ya marais wa nchi huru hayatakiwi kuchapishwa," Zelensky ameviambia vyombo vya habari vya Ukraine akiwa jijini New York, kwa mijubu wa shirika la habari la kimataifa la Reuters.

Bw Zelensky ameongeza kuwa kesi ya Hunter Biden ni miongoni mwa kesi nyingi ambazo huwa anazijadili na viongozi wa kimataifa.

"Kwangu mie, hii ni moja ya kesi nyingi ambazo huwa nazifanyia mazungumzo na viongozi wa mataifa mengine, endapo wananiuliza," ameeleza raisi huyo.

"Wakati mwengine, kesi hizi huchunguzwa ama huwa hazijachunguzwa kwa muda mrefu - na sijui kwanini," ameeleza.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii