Mwanamfalme wa Saudia ameonya vitimbi vya Iran kupandisha bei ya mafuta

Saudi Arabia's Crown Prince Mohammed bin Salman. Photo: September 2019 Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mohammed bin Salman amekubali lawama juu ya mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi japo amekanusha kuamuru kuuawa kwake.

Mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salaman ameonya kuwa vita baina ya nchi yake na Iran vitaharibu kabisa uchumi wa dunia.

Bin Salman ameyasema hayo huku nchi yake pamoja na washirika wao wakuu Marekani, wakiishutumu Iran kushambulia visima vya mafuta ndani ya Saudia.

Pia ameonya kuwa, bei ya mafuta itapanda maradufu iwapo dunia haitaidhibiti Iran.

Iran imekanusha vikali kuhusika na mashambulizi dhidi ya Saudia.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na kituo cha runinga cha CBS News, Bin Salman mesema: "Iwapo dunia haitachukua hatua kali na madhubuti dhidi ya Iran, tutashuhudia kuchupa zaidi (kwa bei ya mafuta) na kutishia maslahi ya dunia."

"Upatikanaji na usambazaji wa mafuta utaparaganyika, na bei itafikia kiwango kikubwa ambacho hakiyumkiniki na hakijawahi kushuhudiwa katika maisha yetu."

Amesema kuwa Mashariki ya Kati inachangia upatikanaji wa "asilimia 30 ya nishati ya dunia, asilimia 20 ya njia ya biashara ya dunia, na asilimia 4 ya pato la dunia."

"Fikiria vitu vyote hivyo vitatu visimame. Hiyo inamaanisha kusambaratika kabisa kwa uchumi wa dunia na si Saudi Arabia ama nchi za Mashariki ya Kati tu," amesema Mwanamfalme huyo.

Vipi kuhusu tuhuma za mashabulizi?

Haki miliki ya picha Reuters

Saudi Arabia inasema ndege zisizo na rubani 18 na makombora ya masafa marefu saba yalishambulia visima vyake viwili katika maeneo ya Abqaid na Aramco Septemba 14.

Wanamgambo wa wa Houthi wa Yemen ambao wanafungamana na Iran wamedai kutekeleza mashambulio hayo.

Lakini Saudi Arabia pamoja na Marekani wanailaumu Iran kwa mashambulizi hayo ambayo yametibua asilimia tano ya uasambazaji wa mafuta duniani na kusababisha kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo.

Rais wa Marekani Donald Trump ameonya kuwa nchi yake ina "machaguo ya kutosha" kukabiliana na mashambulio hayo, ikiwemo "chaguo la mwisho kabisa".

Iran ni mshindani mkubwa wa Saudia katika ukanda wa Mashariki ya Kati, na ni adui mkubwa Marekani ambao wamejitoa kwenye mkataba wa nyuklia mara baada ya Trump kuchukua madaraka.

Uadui baina ya Iran na Marekani umekuwa kwa kasi zaidi mwaka huu.

Marekani imeishutumu Iran kwa kushambulia meli mbili za kubeba mafuta katika ghuba mwezi Juni na Julai, pamoja na meli nyengine nne mwezi Mei.

Iran imekanusha kuhusika na mashambulizi yote hayo.

Uhusika wake kwenye mauaji ya Khashoggi

Haki miliki ya picha Getty Images

Katika mahojiao hayo na runinga ya CBS, Bin Salman pia amekubali kwa kiai fulani kubeba lawama juu ya mauaji ya mwanahabari Jamal Khashoggi.

Lakini amekanusha tuhuma kuwa aliamuru mwanahabari huyo auawe.

Mwanamfalme huyo anashutumiwa kuamuru mauaji hayo ya mwanahabari huyo ambaye alikuwa mkosoaji mkubwa wa utawala wa kifalme wa nchi hiyo.

Bwana Khashoggi aliuawa kwenye ubalozi mdogo wa Saudia nchini Uturuki Oktoba 2 mwaka jana.

"Ninakubali uhusika nikiwa kama kiongozi wa Saudi Arabia, kwa kuwa [mauaji] yalitekelezwa na watu ambao wanafanya kazi kwenye serikali ya Saudia."

Ingawa alikanusha kuagiza watu kumuua Khashoggi na kudai kuwa alikuwa hafahamu jambo lolote lililoendelea.

Mamlaka ya Saudia imelaumu operesheni ambayo imekuwa ikifanyika nchini mwake dhidi ya mauaji na kuwaweka watu 11 kizuizini.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii