Kenya Ferry: ''Tumebaini maeneo ya gari lililozama Kivuko cha Likoni Ferry''

Ferry ya Likoni

Shughuli za kutafuta miili ya watu wawili ambao gari lao lilizama baharini baada ya kudondoka katika feri ya kivuko cha likoni imeanza katika mji wa Mombasa, pwani ya Kenya.

Video inayoonyesha gari, hilo likidondoka ndani ya ferry na kuzama bahari hindi ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumapili na kuzua hamasa miongoni mwa Wakenya kuhusu usalama wa usafiri wa ferry nchini humo.

Wakati tulipokuwa tukienda hewani kivuko hicho cha feri kilikuwa kimefungwa kwa saa tatu ili kuruhusu usakaji wa miili hiyo.

Kundi lililokuwa likiongoza utafutaji huo linashirikisha maafisa wa jeshi la waamaji, wale wa shirika la bandari ya Kenya KPA, maafisa wa taasisi ya uvuvi pamoja na waogeleaji wa mashirika ya kibinafsi.

Kundi hilo limesema kwamba limefanikiwa kupata maeneo mawili yalio kina cha Futi 75 na 173 ambapo huenda gari hilo lipo.

''Tunawaarifu watumizi wa kivuko cha likoni kwamba kutokana na zoezi linaloendelea la kulisaka gari iliozama tutakuwa tukichelewesha huduma za feri kwa takriban nusu saa hadi saa moja lilsema shirika la Ferry katika mtandao wake wa Twitter.

Siku ya Jumatatu mkurugenzi mkuu wa shirika la Ferry Bakari Gowa alisema kwamba wataalam walibaini kwamba gari hilo lilizama kima cha mita 60, hivyobasi kuwa vigumu kuliokoa.

Akizungumza na BBC Gowa alisema kinyume na madai ya wengi kwamba shughuli hiyo imechukua muda mrefu, muda pekee unaoweza kutumika kutafuta miili ya waathiriwa ni saa tatu pekee kila siku.

''Hatujachukua muda mrefu, shughuli hii haiwezi kufanyika muda wa usiku pia kwa sababu operesheni ya feri haiwezi kufanyika jioni na asubuhi wakati watu wanatumia kivuko hicho''.

Kuhusu usalama wa kivuko cha feri Mkurugenzi huyo pia alikana madai kwamba vyombo hivyo havijawekewa usalama wa kutosha na kusisitiza kwamba kivuko hicho kina vifaa vilivyo na usalama wa hali ya juu na kwamba usalama wa pekee unaohitajika ni kuongeza idadi ya feri hizo.

''Ferry zinavusha watu 300,000 kwa siku magari 5800 kwa siku baiskeli 5000 kwa siku iwapo hilo linaweza kufanyika sidhani kwamba tuna matatizo ijapokuwa zipo changamoto katika operesheni. Ili kuimarisha usalama tunafanya hamasa miongoni mwa watumizi wa ferri kila uchao'', alisema bwana Gowa.

Aliongezea kwamba waogealeaji waliokuwa wameingia ndani ya maji sasa wataingia kwa mara nyengine wakiwa na lengo la kutoa miili pamoja na gari hilo.

Haitachukua muda kutoa miliili na gari hilo.

Familia ya waathiriwa imelalamikia kujikokota kwa serikali katika kuitoa miili ya waathiriwa .

Tayari baadhi ya wabunge wametaka maafisa wa shirika la Ferry kuwajibika kwa tukio hilo.

Mbunge wa Likoni Mishi Mboko ametaka serikali kuliwajibisha shirika la Coast Guards pamoja na lile la wanamaji wa Kenya Navy kwa kutochukua hatua za haraka kuokoa maisha.

Waogealeaji walikuwa wameingia kulisaka eneo la gari hilo na sasa wataingia kwa lengo la kutoa gari hilo.Haitachukua muda kutoa miliili katika gari hilo.

Dadake mwanamke aliyekuwa akiendesha gari hilo bi Shila Karembo alisema kwamba familia yao inataka kumuona mama na mtoto waliozama huku wakionya kutoondoka kando kando ya kivuko hicho hadi pale miili yao itakapopatikana.

Bi Karembo ameongezea kwamba kufikia sasa hajaona juhudi za shirika la Kenya Ferry Kutaka kuitoa miili ya waathiriwa chini ya maji.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii