Trump alimuomba Waziri mkuu wa Australia kumchunguza Muller

Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison ni mshirika wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump Haki miliki ya picha AFP/Getty Images
Image caption Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison ni mshirika wa karibu wa Rais wa Marekani Donald Trump

Rais wa Marekani Donald Trump alimpigia simu Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison kumuomba amsaidie kuchunguza chanzo cha uchunguzi wa Robert Mueller, maafisa wa Australia wamethibititisha.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Marekani na Australia, Bw. Trump alimuomba Morrison amsaidie na ushahidi utakaotia dosari uchunguzi huo.

Australia ilithibitisha kuwa mawasiliano kati ya viongozi hao yalifanyika na kwamba Waziri Mkuu alikubali kutekeleza ombi la Rais Trump.

Ufichuzi huu unakuja wakati ambapo Bw. Trump anakabiliwa na uchunguzi wa kutaka kumuondoa madarakani kupitia kura ya kutokua na imani nae kuhusiana na mawasiliano ya kisiri na kati yake na kiongozi mwingine wa kigeni.

Rais Trump anasadikiwa mnamo Julai 25, alimuomba mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelenski kumchunguza makamo wa rais wa zamani wa Marekani Joe Biden katika mawasiliano ya simu yaliofichuka.

Image caption Makamo wa rais wa zamani wa Marekani, Joe Biden

Mazungumzo hayo ya simu baina ya maraisi hao wawili yalifanyika siku chache baada ya Trump kuiagiza serikali yake kuzuia msaada wa kijeshi wa dola milioni 391 kwenda Ukraine.

Mawasiliano hayo yamewafanya wabunge wa chama cha Democratic kuanzisha mchakato wa kutaka kumuondoa madarakani rais Trump.

Siku ya Jumatatu wakili wa Rais Rudy Giuliani alikabidhiwa ombi rasmi la kumtaka afike mahakamani.

Huku hayo yakijiri gazeti la Washington Post limeripoti kuwa mwanasheriak mkuu wa Marekani, William Barr amefanya mazungumzo ya faragha na maafisa wa ujasusi wa Italia na Uingereza kuomba usaidizi wa katika uchunguzi wa ripoti ya mchunguzi maalum Robert Mueller.

Vyanzo vya habari vimelifahamisha gazeti hilo kuwa Bw. Barr alizuru Italia wiki iliopita na kwamba hiyo haikua mara ya kwanza.

Kwanini hatua ya Australia imezua utata?

Mawasiliano ya simu kati ya Bw. Morrison na Bw. Trump yalijulikana na maafisa wa wachache wa Ikulu ya White House ambao ni wasaidizi wa rais, ripoti zinasema - tofauti na hali ilivyokawaida.

Usiri sawa na huo ulifanyika wakati wa mawasiliano ya simu ya Rais Trump na mwenzake wa Ukrain, hali iliyozua maswali ikiwa maafisa wa Ikulu walikua wakijaribu kuficha au kuweka siri rekodi ya mawasiliano ya rais na viongozi wa kigeni.

Mawasiliano kati yake rais na viongozi wa kigeni yamekua yakifuatiliwa kwa karibu tangu uchunguzi dhidi yake ulipoanza.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais wa Marekani Donald Trump

Ripoti ya Mueller ilichunguza ikiwa Bw. Trump alikula njama na Urusi ili imasaidie kushinda katika uchaguzi wa Urais wa mwaka 2016.

Matokeo ya uchunguzi huo uliotolewa mwezi April, haukubaini ikiwa kampeini ya Trump ilishirikiana kiharamu na Urusi kushawishi matokeo ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2016.

Matokeo hayo hata hivyo hayakumuondolea makosa rais huku ripoti ya mchunguzi maalum Robert Mueller ikielezea kwa kina jinsi rais alivyofanya kila juhudi kuvuruga uchunguzi huo.

Ripoti ya Mueller ni kitu gani?

Ripoti ya Muller ni uchunguzi wa miezi 22 juu ya uwezekano wa kula njama baina ya timu ya kampeni ya uchaguzi ya Trump mwaka 2016 na Urusi.

Uchunguzi huo uliongozwa na Mueller, ambaye aliteuliwa kuongoza kazi hiyo mwaka 2017 baada ya vyombo vya kiintelinjesnia vya Marekani kubaini kuwa Urusi walijaribu kushawishi Trump ashinde uchaguzi.

Mueller pia alichunguza iwapo Trump aliingilia uchunguzi pale alipoamuru uchunguzi dhidi ya mshauri wake wa usalama wa taifa Michael Flynn usitishwe, na baadae kumfuta kazi Mkuu wa FBI James Comey.

Flynn amekiri kuwa aliwadanganya FBI juu ya mahusiano yake na Urusi.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Mwanasheria Mkuu wa Marekani, William Barr amekuwa akishutumiwa kufanya mkutano na wana habari kabla ya kutolewa ripoti

Hili ni swali la msingi: upi unatakiwa kuwa ukomo wa tabia ya Rais wa Marekani?

Rais huyu wa 45 amekua akifurahia kuvunja kanuni na sheria-wengine wamedai kuwa mashambulizi yake mara kwa mara dhidi ya Mueller kulikosababisha kuingiliwa na kutishiwa.

Anasema kuwa Rais amefedheheka na kughadhabishwa kutokana na imani kuwa uchunguzi ulikua ukidhoofisha kiti chake.Lakini Mwanasheria maalum Rober Mueller amebainisha mazingira 10 wakati Rais alipokiuka sheria-moja kati ya uhalifu mkubwa kutekelezwa kama inavyoeleza katiba ya Marekani ambapo madhara yake yanaweza kuwa kuondolewa madarakani.

Mwanasheria Mkuu amesema kuwa hawavuki kizingiti hali itakayosababisha kushtakiwa.Bwana Mueller hata hivyo anasema kitu kingine tofauti:''Wakati ripoti hii haihitimishi kuwa Rais ametenda kosa, pia haina maana kuwa halaumiwi.''

Lakini ni sawa? Unaweza kufanya unachokipenda kwa vile si makosa kisheria? Mwisho wa mchakato huu kwa kweli tunaweza kusema kuwa Rais Donald Trump amebaudilisha urais lakini urais haujambadilisha.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii