Kwanini wakili huyu anataka kuondolewe majina ya wakoloni kwenye barabara za Kampala?

kampala

Mamlaka ya Baraza la Mji Mkuu Kampala, ina zaidi ya 2110km za lami, kama barabara 1000. Baadhi ya barabara hizo ni za zamani, nyingine ni mpya bado hazijapewa majina.

Barabara kadhaa za zamani zina majina ya wakoloni wa Uingereza.

Kwa sasa kuna msukumo mkubwa wa kutaka majina ya wakoloni hao kwenye barabara za Uganda yaondolewe.

Mmoja wa wachagizaji, ni wakili na mshauri wa Kabaka Mutebi (mfalme) wa Buganda, Apollo Makubuya, mtunzi wa kitabu - Udhamini, Udhalilishaji au Uporaji - yaani, Protection, Patronage or Plunder? zaidi kutetea Mada ya Buganda katika Uganda.

Apollo Makubuya, anakosoa mipango ya urathi, Uganda ilipopata uhuru, miaka 57 iliopita: hususan kikatiba na kisiasa, ambayo anaieleza kama 'mchafuko'.

Lakini katika makala ya maoni, iliochapishwa gazetini, inayoitwa 'Uondoaji Ukoloni, Upaji upya majina ya barabara na mbuga za Uganda' - 'Decolonisation and renaming of Uganda's streets, parks', anaongeza katika ukosoaji wake, mpango wa majina ya barabara.

Nami Makubuya anatoa mifano ya wakoloni, miongoni mwao Sir Harry Johnston, aliyewasili nchini humo kujadili mapatano ya 1900. Na Majina kama Henry Coleville, na hujuma ambayo ilishinda nguvu Bunyoro baada ya kuteketeza eneo hilo na kuwafukuza viongozi wake.

'Watu kama Fredrick Lugard aliyehusika na ukatili mkubwa Buganda na mauaji ya watu wengi waso makosa, kama maendeleo ya utawala wa Uingereza.' anaeleza Makubuya.

'Kinachouma, ukiona majina hayo katika kitovu cha mji wetu mkuu na sehemu nyingine za Uganda unasimama na kujiuliza, kuna sababu yoyote kwanini, miaka mingi baada ya kupata uhuru wetu kama Uganda, tuadhimishe watu kama hao ambao wana jukumu la kutisha, kudhalilisha na uvunjaji wa kila aina ya haki za bindamu katika Uganda?' ameongeza.

Apollo Makubuya hakuona haya wala vibaya kumwandikia Spika wa Bunge la Uganda kuhusu kiroja hicho, kishughulikiwe.

Katika uhakiki wake wa kitabu Protection, Patronage or Plunder? Msomi na mwanasiasa wa zamani Uganda Yosh Tandon, anamweleza Makubuya kama 'Mbaganda wa kisiasa', mwenza wa ufalme, aliyetumika kama Mwanasheria Mkuu wa Kabaka na sasa naibu wa Tatu wa Katikiro.

Kwa maneno mengine Makubuya ni mhafidhina na kabaila.

Kuambatana na historia ya Uganda, Buganda, shauri ya ushirika na Uingereza, ilifaidi chini ya ukoloni.

Makubuya, anafafanua majina hayo yana nini, kiasi cha yeye leo kuhisi wakati umepita, majina hayo yabadilishwe?

Haki miliki ya picha @ANMakubuya
Image caption Apollo N Makubuya

'Jina ni uhakikisho, ni muhimu ikija masuala ya utambulisho. Sina ugomvi na majina ya Maskofu, ambao hawakuwa na shida katika kuendeleza Ukristo au maendeleo ya kijamii.

Tuko huru miaka 57 na uondoaji ukoloni ni mchakato unaoendelea; si kitu kilichoanza na kukoma miaka ya 1960. Lazima uendelee' anasema Makubuya.

Je, kubadili majina ni sawa na kunabadilisha historia?

Anasema haibadili historia hata kidogo.

Mtazamo wake ni kwamba majina ya wakoloni na kile walichokifanya ni sehemu ya historia.

Ila anachopinga ni 'kusisuguliwe machoni mwetu, kwenye barabara kuu mijini'.

Badala yake anaona kwamba wanastahili kusalia katika makumbusho na vitabuni.

Afisa wa mahusiano wa Mamlaka ya Jiji, Peter Kawujju anaeleza utaratibu unaostahili kufuatwa kuweka au kuondoa jina la barabara.

Anafafanuwa kwamba mchakati huo huanzia katika 'Kamati za Vijiji' ambazo hushauri majina kwa utawala wa mji.

Baada ya hapo mamlaka ya Jiji, nayo inaweza kukaa na kufanya mapendekezo.

Hatahivyo anaeleza kuwa mji wa Kampala una historia yake, 'kama watu wanahisi kwa kweli wana madukuduku kwa majina fulani au hawana raha nayo, watume mapendekezo, wawasiliane na sisi, halafu uamuzi unaweza kuchukuliwa' amesema Kawujju.

Apollo Makubuya anaeleza, mavuguvugu mawili yameibuka nchini: moja lisemalo 'usiguse majina ya kikoloni ya barabara' licha ya ukatili na maonevu yanayohusishwa nayo.

Na vuguvugu la pili 'gusa na ondoa majina ya kikoloni ya barabara' kwa sababu yamepitwa na wakati; wakati umewadia Uganda iadhimishe 'mashujaa wake' wananchi; na wapo tele.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii