Baadhi ya walioandika barua kwenda kwa DPP wajitaja mahakamani Tanzania

Michael Wambura
Image caption Michael Wambura anakabiliwa na mashtaka ya kutakatisha fedha zaidi ya shilingi za Tanzania milioni 100.

Baadhi ya watuhumiwa wa makosa ya uhujumu uchumi ambao wameandika barua za kuomba msamaha wameanza kujitaja mahakamani nchini Tanzania.

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli alitangaza msamaha Septemba 22, kwa watuhumiwa wa makosa hayo ambao wataandika barua za kukiri makosa, kuomba radhi na kukubali kulipa fedha wanazotuhumiwa kujipatia kinyume cha sheria.

Jumatatu wiki hii, Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) wa Tanzania, Biswalo Mganga, ambaye ndiye anaepokea barua hizo alibainisha kuwa kufikia siku hiyo ofisi yake ilishapokea barua 467.

Jumla ya Shilingi bilioni 107 za Tanzania sawa na takribani dola milioni 4.6 zinatarajiwa kurejeshwa na watuhumiwa hao.

Majina ya waliotuma barua hizo hayakutajwa, lakini tayari kuna ambao wameshaanza kuziambia mahakama kuwa wameomba msamaha huo.

Aliyekuwa Makamu wa Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Michael Wambura ni moja ya watu maarufu ambao wanakabiliwa na mashtaka hayo, na Jumatano ameieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa amekwishaandika barua kwa DPP kwa ajili ya kuomba msamaha na kukiri makosa yanayomkabili mahakamani hapo na ameuomba upande wa mashtaka ufuatilie barua hiyo ili upate majibu kwa haraka.

Wambura ambaye amefungiwa maisha kujihusisha na soka, alifikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Februari 11 mwaka huu, akikabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashitaka 17 yakiwemo ya kutakatisha fedha zaidi ya shilingi za Tanzania milioni 100.

Katika mahakama hiyo jana pia upande wa utetezi wa aliyekuwa Mkurugenzi wa Mipango wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) nchini Tanzania bi Kulthum Mansoor umedai kuwa mteja wao ameandika barua ya msamaha kwa DPP.

Haki miliki ya picha NMG
Image caption Bi Kulthum Mansoor anakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha shilingi za Tanzania bilioni 1.4.

Bi Kulthum anakabiliwa na mashtaka ya kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha shilingi za Tanzania bilioni 1.4. Afisa huyo wa zamani wa Takukuru alikamatwa na kufikishwa mahakamani mwezi Machi mwaka huu kwa tuhuma za kuwadhulumu viwanja wafanyakazi wenzake.

Katika kesi nyengine, watu watano ambao ni wakuu wa kampuni ya mawasiliano ya Six Telecoms Limited, akiwemo wakili maarufu nchini Tanzania Dk Ringo Tenga pia wamemwandikia DPP kukiri makosa yao. Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Hafidhi (au Rashidi) Shamte, Mkurugenzi wa kampuni Peter Noni, Mkuu wa fedha Noel Chacha na kampuni yenyewe ya Six Telecoms.

Wastakiwa hao walifikishwa kwa mara ya kwanza Novemba 2017 na kufunguliwa mashtaka sita ya uhujumu uchumi ikiwemo kusababishia hasara Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA) hasara ya dola za Marekani milioni 3.7.

Katika hatua nyengine, Mahakam ya Kisutu jana imemhukumu mfanyabiashara Hilaly Akida kulipa shilingi za Tanzania milioni 100, baada ya kukiri mashtaka kufuatia wito wa msamaha wa rais Magufuli.

Akida alikuwa akikabiliwa na mashtaka ya uwindaji haramu, na upande wa mashtaka uliiambia mahakama kuwa mfanyabiashara huyo amekiri kosa na kushauri apewe adhabu ya kurudisha fedha hiyo serikalini, adhabu ambayo mahakama iliizingatia.

Hata hivyo, washtakiwa wenza wanne wa Akida katika kesi hiyo hawajakiri makosa na wamerudishwa rumande kuendelea na kesi.

"Msamaha uharakishwe"

"DPP mfanye haraka, msichukue muda mrefu kupitia maombi hayo ili watu hawa warudi kwenye jumuiya zao. Ikichukua mwezi ama mwaka hata dhana nzima ya msamaha itaondoka," ameagiza rais Magufuli Jumatatu wiki hii.

Toka aingie madarakani takribani miaka minne iliyopita Magufuli amejipambanua kwa kupigana dhidi ya rushwa na ufisadi.

Katika vita hiyo, vigogo kadhaa wa serikali walifutwa kazi kwa tuhuma za uzembe na rushwa.

Watu kadhaa pia wamefunguliwa mashtaka ya uhujumu uchumi na kesi nyingi kati ya hizo bado zinaunguruma.

"Najua wanateseka. Unaona wanavyopelekwa mahakamani, wengine wamekonda kweli, inatia huruma na inaumiza. Najua wengine wanataka kuomba msamaha..." alisema Magufuli Septemba 22, wakati akitangaza msamaha.

Hata hivyo alionya kuwa kwa wale watakaoshindwa kuomba msamaha, waendelee kubanwa hata kama kesi zao zitachukua miaka 20.

"Nimetoa siku saba hizi na baada ya hizi sitatoa tena...watakaoendelea kukaa gerezani wasimlaumu mtu," ameseisitiza hii leo.

Mada zinazohusiana