Sex for Grades: Mhadhiri asimamishwa kazi na chuo kikuu cha Nigeria baada ya makala ya BBC Africa Eye

Huwezi kusikiliza tena
BBC Africa Eye: Unyanyasaji wa kingono wa wanafunzi katika Chuo kikuu cha Lagos na Ghana.

Mhadhiri wa chuo kikuu cha Lagos amesimamishwa kazi baada ya kuonekana katika video ya uchunguzi ya 'BBC Africa Eye' akimfanyia unyanyasaji wa kingono mwandishi wa BBC wa habari za uchunguzi.

Boniface Igbeneghu ambae pia ni mchungaji wa kanisa amesimamishwa pia na kanisa lake.

Ni miongoni mwa wahadhiri walionekana katika makala ya siri iliyofanyika kwa zaidi ya mwaka mmoja na kitengo cha BBC Africa Eye.

Makala hii imeamsha hisia na maoni mbalimbali katika mitandao ya kijamii na kuzua mjadala juu ya wahadhiri kutoka vyuo vya hadhi ya juu Afrika magharibi.

Katika taarifa hiyo pia inaonesha baadhi ya wanafunzi wakiwa wamefichwa sura zao wakielezea unyanyasaji wa kingono waliopitia kutoka kwa wahadhiri.

Kwanini amesimamishwa?

Image caption Dr Igbeneghu alipigwa picha kwa siri na BBC Africa Eye

Mhadhiri huyu alirekodiwa akimuuliza maswali yasiyofaa mwandishi wa uchunguzi wa BBC aliyeigiza kama mwanafunzi mwenye umri wa miaka 17.

Katika mkutano na mhadhiri huyo alikua akimpapasa na kumwambia ambusu wakiwa ndani ya ofisi yake iliyofungwa na kumtisha kuwa atamwambia mama yake kama atakataa kufuata maelekezo yake.

Wanafunzi kadhaa walionekana katika makala hii wamemshutumu pia mhadhiri huyu kwa unyanyasaji wa kingono. Mwanafunzi mmoja ambae amefichwa uhalisia wake amesema kuwa alimsababishia kutaka kujiua mara kadhaa.

Chuo kikuu cha Lagos katika kujibu shutma hizo, walifanya mkutano siku ya Jumatatu kujadiliana kisha Dr. Igbeneghu, alisimamishwa mara moja kuingia katika maeneo ya chuo.

Katika taarifa ya chuo kikuu cha Lagos, imesema kuwa kitendo hicho ni cha udhalilishaji wa hali ya juu, wamesisitiza pia kufanya uchunguzi na kuhakikisha tabia hiyo inakoma kabisa.

Taarifa hiyo imesema kuwa wamekifunga chumba cha ''cold room'' ambacho kilioneshwa katika makala hiyo kama sehemu ambao wahadhiri wanakutana na wanafunzi na kufanya starehe mbalimbali.

Kanisa la Four square ambapo Dr Igbeneghu anaongoza, wamejitenga nae katika taarifa yao, wamesema kuwa kanisa linakemea tabia kama hizo na kumtaka ajiuzulu katika nyadhifa zote.

Kitu gani kingine kimeoneshwa katika Makala?

Makala hii ya urefu wa saa moja imeonesha pia wahadhiri wawili kutoka chuo kikuu cha Ghana wakihusika na vitendo vya unyanyasaji wa kingono kwa wanafunzi.

Wote wawili Profesa Ransford Gyampo na Dr Paul Kwame Butakor wamekanusha kuhusika na kuomba rushwa kwa kutoa alama za darasani.

Profesa Gyampo amesema kwa vyombo vya ndani vya habari kuwa ana mpango wa kuchukua hatua za kisheria dhidi ya BBC.

Chuo kikuu cha Ghana kimetoa taarifa kuwa watafanya uchunguzi kwa wahadhiri hao na kusisitiza kuwa hawahusiki na kumtetea mhadhiri yoyote ambae ameshukiwa kujihusisha na rushwa ya ngono chuoni.

Image caption Ofisi ya Dr Igbeneghu imefungwa


Kumekua na maoni gani?

Uchunguzi huu wa BBC umezusha mjadala mkali katika mitandao ya kijamii na maoni mbalimbali.

Watumiaji wengi wa mtandao wa twitter wametaka hatua kali zichukuliwe lakini pia baadhi wametoa ushuhuda kwa vitendo kama hivyo vimewahi kuwatokea.

Mwandishi wa habari Kiki Mordi aliyeshiriki katika Makala hii, ametoa historia yake binafsi ya kukubwa na unyanyasaji wa kingoni wakati yupo chuoni.

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii