Rais Magufuli: 'Tusiwadanganye mabinti kwa kuwaambia 'I Love you'

MIMBA Haki miliki ya picha AFP

Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli ameshangazwa na kutokuchukuliwa hatua dhidi ya wanaume wanaotuhumiwa kuwapachika mimba wanafunzi 229 mkoani Rukwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Magufuli amewataka viongozi wa serikali pamoja na wa kidini mkoani humo kulivalia njuga tatizo hilo.

"Serikali inatoa mchango kwa kutoa elimu bure na wanaume bure wanawapa mimba watoto wa shule! Hao wanaume bure 229 ndio viongozi? Kwa sababu kama sio hao viongozi, je viongozi wameshindwa kitu gani kuwapeleka hawa watoto kwenye haki?

"Watoto 229 wamekatiliwa maisha yao katika elimu," alisema Rais Magufuli.

Haki miliki ya picha AFP

"Tuwaogope mabinti zetu na tuwalee binti zetu na tusiwadanganye kwa fedha tunazopata, maana wanaume wanaofanya hayo mambo ni wanaume wakubwa tu na inawezekana hata wana wake wawili nyumbani na hawajawahi kuwanunulia hata nguo na bado wanawakimbilia watoto wadogo wa shule..." aliongeza Magufuli akiwa katika ziara yake mkoani Rukwa, kusini magharibi mwa Tanzania.

Rais Magufuli aliwasisitiza wanafunzi kusoma kwa bidii na kuwa na malengo madhubuti ya kesho yao.

"Lengo la serikali ni wanafunzi wote wasome bure kuanzia shule ya msingi, sekondari na matarajio ni mpaka chuo kikuu. Ukiambiwa wewe mzuri mwambie akamwambie mama yake, msiogope kuwapa maneno magumu, nataka msome, nyinyi ndio marais wa kesho, mawaziri na wabunge."

"Nia ya serikali yangu ni kuleta maendeleo, kila mmoja awe tajiri, watoto someni..."

"Hata kama mwalimu wako anakwambia anakupenda penda mwambie hayohayo majibu, takwimu za mimba mkoa huu zinatisha. Nilitegemea wanaume 229 wawe wamefungwa ila mpaka sasa sina hakika kuwa hata mmoja amefungwa".

"Viongozi wa mkoa na wilaya mbalimbali, hii ni aibu. Kwenye kata yako diwani awepo na watoto wamepata mimba basi wewe hutoshi. Viongozi wa dini inabidi tukemee jambo hili kwa nguvu zote, hili linatupa doa katika taifa leo," Magufuli alisisitiza.

Mnamo mwaka 2014, takribani wasichana 808 mkoani Rukwa waliachishwa shule kutokana na mimba.

Idadi hiyo ikijumuisha wasichana 59 kutoka shule za msingi na 749 kutoka shule za sekondari.

''Ni wazi kwamba tunakabiliwa na changamoto katika eneo hili,wazazi wengi bado wanaamini tamaduni ambazo tayari zimepitwa na wakati. Wasichana wananyimwa haki zao za kupata elimu kutokana na tamaduni potofu," alisema kiongozi wa mkoa huo mwaka 2014.

Aliongezea kuwa ukosefu wa hamasa kuhusu maswala ya elimu miongoni mwa wazazi ni sababu nyengine ya wasichana wengi wa shule kuacha masomo katika mkoa huo.

Mwaka 2012 Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu, pamoja na Shirika la Taifa la usaidizi wa Kisheria, walifungua kesi dhidi ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa niaba ya wasichana wa shule nchini Tanzania, wakidai kuwa kuwapima wasichana ujauzito kwa lazima ni ukiukaji wa masharti ya Katiba ya Tanzania, hasa, Ibara ya 13 ya Katiba inayotoa haki ya usawa bila ubaguzi.

Mnamo Agosti 2017, karibu miaka mitano baada ya waombaji kufungua kesi, Mahakama Kuu ilifutilia mbali madai yao.

Mnamo mwaka 2013, Center for Reproductive Rights kilitoa chapisho lilipewa jina "Forced Out: Mandatory Pregnancy Testing and the Expulsion of Pregnant Students in Tanzanian" (Upimaji Mimba wa Lazima na Kufukuzwa Shule kwa Wanafunzi Wajawazito Tanzania) likionesha kwamba viongozi wa shule nchini Tanzania wanalazimika kuwafukuza wasichana wenye ujauzito shuleni.

Chapisho hilo pia lilitanabahisha kuwa kila mwaka, wastani wa wanafunzi 8,000 wa kike huacha shule kutokana na ujauzito. Kulazimishwa kupima mimba ni ukiukwaji mkubwa wa haki za wasichana za faragha na uhuru.

Kwa mujibu wa shirika la haki za kibinadamu la Human Rights Watch, nchini Tanzania zaidi ya watoto 15,000 hukatisha masomo yao kila mwaka kutokana na mimba za utotoni na kwa mujibu wa utafiti wa afya uliofanywa na wizara ya afya mwaka 2015 hadi 2016 , asilimia 27 ya watoto wa kike wamepata watoto wakiwa kati ya miaka 15 na 19.

Haki miliki ya picha IKULU

Mwaka jana Agosti, rais Magufuli alisisitiza marufuku kwa wasichana wanaopata ujauzito kuendelea na masomo katika shule za serikali.

Rais Magufuli alisema kuwa chini ya uongozi wake wanafunzi wa kike ambao watakaopata ujauzito wakiwa shuleni hawataruhusiwa tena kurudi shuleni.

Aidha Magufuli alikumbusha kwamba sheria inasema mwanaume ambaye atapatikana na hatia ya kumpa mimba mtoto wa shule, atafungwa jela miaka 30.

Magufuli aliongeza kwamba mwanaume huyo atapata fursa ya kutumia nguvu alizotumia kumpachika mimba msichana huyo, kufanya kilimo akiwa gerezani.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii