Cynthia Wambua: Muathiriwa wa msongo wa mawazo asema yeye sio mwenda wazimu

Cythia Wambua

Bi Cynthia Wambua, 40, ni mgonjwa wa akili ambaye ameshanusurika kifo baada ya kupanga kumeza madawa ili kujitoa uhai.

Kwa karibu miaka tisa sasa, Bi Cynthia ambaye ni raia wa Kenya amekuwa akimeza dawa za kukabiliana na msongo wa mawazo (depression).

Hii leo, Oktoba 10, inapoadhimishwa siku ya afya ya akili duniani, Cynthia ameisimulia BBC safari yake ya maisha tangu alipogudua kuwa anakabiliwa na hali hiyo.

Anasema alitumia mbinu tofauti za tiba lakini hakufanikiwa kung'amua tatizo lake ni lipi hasa.

"Kabla nijue naugua maradhi ya akili, nilikuwa na tatizo la kunywa pombe kupita kiasi kwa sababu sikuwa napata usingizi wala sikuwa mtulivu."

Cynthia anasema ndoa yake ilianza kukabiliwa na changamoto kwa sababu alikuwa akigombana na mume wake kuhusiana na masuala ya kawaida kati ya mume na mke kama vile utumizi wa fedha na mpangilio wa mambo nyumbani.

''Hali ile ilikuwa mbaya sana mume wangu alikua akinidhulumu kila tulipogombana'', alisema Bi. Cynthia.

Ndoa kuvunjika

Aliposhindwa kuhimili hali mzozo wa kifamilia akaamua kujiondoa katika ndoa.

"Niliingia kwenye ndoa na dhana kwamba mwanamke lazima avumilie, lakini uvumilivu katika ndoa iliendelea kuniumiza," Bi Cynthia aliongeza.

Katika jamii mwanamke ametwikwa jukumu la kuhakikisha kuwa ndoa yake inadumu, hali iliyomfanya Cynthia kuweka siri masaibu yake licha ya kuwa alihisi kuwa ndoa inaelekea kuvunjika.

Cythia anasema hakutarajia tukio la ndoa yake kuporomoka na ghafla mama yake akagunduliwa kuwa na maradhi ya saratani.

Anasema matukio hayo yalichangia yeye kukumbwa na msongo wa mawazo.

Alijiingiza katika unywaji wa pombe kama njia rahisi ya kujiliwaza.

"Nilianza na gilasi moja ya mvinyo nikagundua kuwa nilikuwa napata usingizi na mawazo yalipungua nikinywa. Gilasi ikageuka na kuwa chupa, mara nikajikuta nimelewa kupindukia," alikariri Bi Cynthia.

Kutokana na athari ya unywaji pombe Cynthia alianza kuzembea kazini, wakati mwengine hafiki kabisa ama akifika ni kwa kuchelewa na kunuka harufu ya pombe.

Image caption Bi Cyntia amekuwa akikabiliana na hali yake ikiwemo kuonana na daktari kwa miaka tisa iliyopita.

Anaongeza kuwa alipoteza matumaini maishani hadi wakati mmoja akamua kujiua kwa kutumia dawa nyingi kupita kiasa.

''Nilinusurika kutokana na simu ya rafiki yangu'' alisema.

Baada ya kuepuka kifo Cynthia alianza kukubali hali yake na kuamua kwenda hospitali kupata ushauri wa kimatibabu kuhusu ugonjwa wa akili.

Daktari wa ugonjwa wa akili Bwana Gatere anasema kuwa watu wengi wanadhania kuwa mtu akiwa na ugonjwa kama uliyomwathiri Cythia Wambua ana wazimu.

Dakatari anasema kuwa kuna zaidi ya magonjwa 200 ya akili.

"Ugonjwa wa akili una dalili zake kwa hiyo kinachotizamwa sana ni mabadiliko katika hisia na tabia za mtu na wala sio ugonjwa ambao mtu anapatwa na maumivu.''

''Ni lazima uwe maakini na kubadilika ghafla kwa hisia zako kama vile kukasirika kwa muda wa zaidi ya wiki mbili," daktari Gatere aliongeza.

Mtaalamu huyo wa magonjwa ya akili pia anasema kuwa mzigo wa matatizo ya akili miongoni mwa watu ni dhahiri lakini watu wengi hawajitokezi kutibiwa kwa wakati kwa kuhofia kunyanyapaliwa kwa kuitwa wenda wazimu au waraibu wa dawa za akili.

Anasema watu walioathiriwa na matatizo ya kiakili huonesha na dalili za msongo wa mawazo ambayo huchangi avifo vya vijana wa kati ya umri wa miaka 15-19.

Matatizo ya akili kuwa moja ya changamoto kubwa katika nchi nyingi duniani .

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii