Gari lililozama kivuko cha Likoni mjini Mombasa Pwani ya Kenya limeonekana

Likoni Ferry
Image caption Jitihada zimekuwa zikiendelea kwa siku 11 leo kujaribu kuyaopoa miili ya watu wawili na gari lililozama katika kivuko cha Likoni pwani ya Kenya

Gari limepatikana lililokuwa limezama katika kivuko cha feri huko Likoni, Mombasa Pwani ya Kenya.

Hatahivyo msemaji wa Serikali Cyrus Oguna anasema kwamba hawawezi kuthibitisha iwapo gari hilo lililopatikana ni lile ambalo jitihada za kuliopoa zimekuwa zikiendelea kwa siku 11 hii leo.

Jitihada hizo zimekuwa zikiendelea kujaribu kuyaopoa miili ya watu wawili, mama na mwanawe wa kike wanaorifiwa kuwemo ndani wakati lilipozama kutoka kwenye kivuko hicho mnamo Septemba 29.

"Usiku wa jana wakapata sehemu mbili ambazo walikuwa wanakisia gari liko pale. Wamechunguza asubuhi ya leo na tukaamua kutuma wapiga mbizi wa Kenya Navy kwenda kuchunguza ni kitu kipi kinachoweza kuwa pale chini.

"Kufikia mida ya saa saba au nane wakaja na taarifa kwamba wameona kitu ambacho kinafanana na kifaa au chombo ambacho tunatafuta." Oguna ameeleza hivi punde katika mkutano na waandishi habari katika eneo hilo la Likoni.

Ameeleza kwamba mipango ya ukaguzi na kulitoa majini ingali inaendelea.

Wanamaji wa Kenya wamekuwa katika shinikizo kali kumaliza zoezi hilo la uopoaji kabla ya Oktoba 20 - tarehe inayoadhimishwa kama sikukuu ya Mashujaa iliyopangiwa kufanyika kitaifa katika mji huo wa Pwani ya Kenya.

Wakaazi walikuwa wametishia kuisusia sherehe hiyo ambayo rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa kuhudhuria, iwapo miili hiyo haitakuwa imeopolewa.

Image caption Kivuko cha Likoni pwani ya Kenya

Tunayoyafahamu kufikia sasa:

Sept 29: Gari dogo aina ya soloon lililoarifiwa kuwa na watu wawili ndani lazama katika kivuko cha Likoni

Sept 30: Mkurugenzi mkuu wa shirika la Ferry Bakari Gowa asema kwamba wataalam wamebaini kuwa gari hilo lilizama kima cha mita 60, hivyobasi kufanya kuwa vigumu kuliokoa.

Sept 30: Shughuli za uokoaji ambazo zimejumuisha maafisa kutoka vitengo vya Kenya Navy, Kenya Ferry, na wapiga mbizi wa kibinafsi zaanza.

Okt 1: Kivuko cha feri chafungwa kwa saa tatu ili kuruhusu utafutaji ulioendelea wa gari na miili ya waliokuwemo ndani.

Okt 2: Familia ya waathiriwa yalalamikia kujikokota kwa operesheni ya uopoaji miili ya waathiriwa.

Okt 2: Kikosi cha pamoja katika operesheni ya uopoaji kinasema kimegunuda sehemu lilipo gari. Hii ni baada ya kuyakagua maeneo kadhaa yalioshukiwa kuwepo gari hilo.

Okt 3: Maafisa wanaendelea kushughulika na ukaguzi wa maeneo yalioshukiwa kuwepo gari hilo.

Okt 7: Wapigambizi wa Afrika Kusini wajiunga katika operesheni hiyo ya uopoaji.

Okt 8: Wapigambizi waanza kazi ya kutafuta miili na gari.

Okt 9: Gari lililokuwa limezama katika kivuko cha Likoni limeonekana. Msemaji wa serikali Cyrus Oguna asema haiwezi kuthibitishwa iwapo ndilo gari lililozama Jumapili Septemba 29.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii