Mawakili wa Kabendera wathibitisha kusudio la mteja wao kuingia makubaliano na mwendesha mashitaka

Erick Kabendera
Image caption Erick Kabendera

Mwandishi wa habari za uchunguzi nchini Tanzania, Erick Kabendera, anakusudia kufanya majadiliano na Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DPP) kuhusiana na tuhuma zinazomkabili.

Mwanahabari huyo, anakabiliwa na mashtaka matatu ya matatu ya ubadhirifu wa kiuchumi .

Katika mashtaka hayo Kabendera anatuhumiwa na kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini Tanzania, shtaka la pili ni la kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja sabini za kitanzania. Kosa la tatu ni la utakatishaji fedha zenye thamani ya zaidi ya millioni mia moja na sabini.

Jopo la wanasheria wanaomtetea Kabendera kutoka Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) linaloongowa na wakili Jebra Kambole limeileza Mahakama hii leo juu ya kusudio la kufanya majadiliano hayo.

"Kifungu cha 194 A (2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (Marejeo ya mwaka 2019) kinaeleza bayana kwamba mtuhumiwa, au wakili wa mtuhumiwa au mwendesha mashitaka mkuu wa serikali anaweza kuanzisha majadiliano (plea bargaining) na kuijulisha mahakama juu ya kutaka makubaliano ya pamoja," imeeleza taarifa ya THRD.

Makosa yote hayana dhamana na Kabendera anaendelea kusota rumande, na kesi yake inatarajiwa kutajwa tena Oktoba 24.

Septemba 5 mwaka huu, Bunge la Tanzania lilipitisha muswada wa maboresho ya sheria mbalimali ikiwemo Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ambapo mapatano baina ya watuhumiwa na mwendesha mashtaka (plea bargain) yalipitishwa na tayari imesainiwa kuwa sheria na rais John Pombe Magufuli.

Katika makubaliano hayo, mshukiwa anaweza kukiri tuhuma ama sehemu ya tuhuma dhidi yake ili kupata afueni fulani ikiwemo kuondolewa baadhi ya mashtaka,ama kupunguziwa muda ama aina ya adhabu.

Mabadiliko hayo ya sheria pia yanabainisha kuwa mtuhumiwa anaweza kutakiwa kulipa fidia ama kurejesha fedha ambazo zinahusishwa na kesi anayoshitakiwa nayo.

Makubaliano hayo yakishafikiwa yatapelekwa mahakamani na kutambuliwa rasmi, na mahakama awali itajiridhisha kuwa hayakuingiwa kwa kushurutishwa.

Pia mshukiwa atatakiwa kula kiapo cha kukubaliana na makubaiano hayo, pia atasomewa haki zake ikiwemo kumuondoshea haki ya kukata rufaa, isipokuwa kuhusu urefu ama uhalali wa hukumu atakayopatiwa.

Kesi ya Kabendera imekuwa ikivutia hisia mbalimbali ndani na nje ya Tanzania awali ilikuwa namna ambavyo amekamatwa, na taswira inayotokana na hatua hiyo kwa uhuru wa yombo vya habari nchini humo.

Pia baadhi ya wanaharakati wameonyesha kushangazwa na namna ambavyo tuhuma dhidi ya mwanahabari huyo zilivyokuwa zikibadilika.

Awali maafisa wa polisi na wale wa idara ya uhamiaji walisema anachunguzwa kuhusu utata wa uraia wake. Baadaye mawakili wake walitoa taarifa wakieleza mteja wao atashtakiwa kwa kuhusika na ripoti iliyochapiswha katika jarida la The Economist, lakini mahakamani kibao kikageuka tena na kuwa kesi ya ubadhirifu wa kiuchumi.

Mada zinazohusiana