Kenya Ferry: Gari lililozama baharini limetolewa

Gari lililozama baharini

Gari lililozama baharini siku 13 zilizopita katika kivuko cha Likoni feri, mjini Mombasa pwani ya Kenya hatimae limetolewa.

Hii ni baada ya wapiga mbizi wa jeshi la Kenya kwa ushirikiano na wapiga mbizi kutoka Afrika kusini kufanikiwa kufikia gari hilo.

Miili ya mama Mariam Kighenda, 35, na mwanawe wa kike Amanda Mutheu, 4, pia imeopolewa kutoka ndani ya maji.

Aliyekuwa mume wa Mariam, bwana John Wambua aliweza kutambua miili ya marehemu kabla haijaondolewa katika eneo la tukio.

Vilevile ibada maalum ya kuwaombea marehemu , iliendeshwa na mchungaji mara tu baada ya miili hiyo kutolewa kwenye maji.

Jitihada za kuopoa miili ya mama na mtoto wake wa kike waliokuwemo ndani ya gari hilo lililozama zilianza mnamo Septemba 29.

Wakenya wamekua wakitumia mitandao ya kijamii kuelezea masikitiko yao.

Wanamaji wa Kenya walipata shinikizo kubwa la kumaliza zoezi hilo la uopoaji kabla ya Oktoba 10 - tarehe inayoadhimishwa kama sikukuu ya Mashujaa iliyopangiwa kufanyika kitaifa katika mji huo wa Pwani ya Kenya.

Wakaazi walikuwa wametishia kuisusia sherehe hiyo ambayo rais Uhuru Kenyatta alitarajiwa kuhudhuria, iwapo miili hiyo haitakuwa imeopolewa.

Tukio lilivyojiri:

Sept 29: Gari dogo aina ya soloon lililoarifiwa kuwa na watu wawili ndani lazama katika kivuko cha Likoni

Sept 30: Mkurugenzi mkuu wa shirika la Ferry Bakari Gowa asema kwamba wataalam wamebaini kuwa gari hilo lilizama kima cha mita 60, hivyobasi kufanya kuwa vigumu kuliokoa.

Sept 30: Shughuli za uokoaji ambazo zimejumuisha maafisa kutoka vitengo vya Kenya Navy, Kenya Ferry, na wapiga mbizi wa kibinafsi zaanza.

Okt 1: Kivuko cha feri chafungwa kwa saa tatu ili kuruhusu utafutaji ulioendelea wa gari na miili ya waliokuwemo ndani.

Okt 2: Familia ya waathiriwa yalalamikia kujikokota kwa operesheni ya uopoaji miili ya waathiriwa.

Okt 2: Kikosi cha pamoja katika operesheni ya uopoaji kinasema kimegunuda sehemu lilipo gari. Hii ni baada ya kuyakagua maeneo kadhaa yalioshukiwa kuwepo gari hilo.

Okt 3: Maafisa wanaendelea kushughulika na ukaguzi wa maeneo yalioshukiwa kuwepo gari hilo.

Okt 7: Wapigambizi wa Afrika Kusini wajiunga katika operesheni hiyo ya uopoaji.

Okt 8: Wapigambizi waanza kazi ya kutafuta miili na gari.

Okt 9: Gari lililokuwa limezama katika kivuko cha Likoni limeonekana. Msemaji wa serikali Cyrus Oguna asema haiwezi kuthibitishwa iwapo ndilo gari lililozama Jumapili Septemba 29.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii