Pentagon imesema vikosi vya Marekani vinavyoondoka Syria vinahamia Iraq

Msafara wa magari ya kijeshi ya Marekani umeonekana ukiondoka kaskazini mwa Syria Haki miliki ya picha AFP
Image caption Msafara wa magari ya kijeshi ya Marekani umeonekana ukiondoka kaskazini mwa Syria

Vikosi vyote vya Marekani vinavyoondoka kaskazini mwa Syria vinatarajiwa kuhamia magharibi mwa Iraq, waziri wa ulinzi Mark Esper, amethibitisha.

BW. Esper amewaambia wanahabari kuwa, chini ya mpango wa sasa karibu wanajeshi 1,000 watapelekwa Iraq kusaidia katika juhudi za kuzuia kurejea upya kwa kundi la Islamic State (IS).

Rais Donald Trump amewahi kuahidi kuwarejesha nyumbani wanajeshi wa Marekani.

Kuondoka kwa vikosi vya Marekani kaskazini mwa Syria kulitoa nafasi kwa Uturuki kuanzisha oparesheni ya kijeshi dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi.

Pande zote mbili zimekuwa zikilaumiana kwa kukiuka mkataba wa kusitisha mapigano ulioongozwa Marekani.

Ankara inawachukulia wanamgambo walijumuishwa katika vikosi vya Kikurdi ni magaidi, hatua iliyoifanya kubuni "eneo salama" ndani ya Syria.

Haki miliki ya picha Getty Images
Image caption Maelfu ya watu wametoroka makazi ya katika eneo la kaskazini mwa Syria tangu Uturuki ilipoanzisha opareshani dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi

Siku ya Jumapili, Uturuki ilisema kuwa mmoja wa wanajeshi wake ameuawa na mwingine kujeruhiwa wakati wakikabiliana na wapiganaji wa Kikurdi karibi na mji wa Syria wa Tal Abyad.

Vikosi vya Kikurdi viliwahi kuilaumu Uturuki kwa kuvikataza kuwahamisha watu wake kutoka mji wa mpakani.

Huku hayo yakijiri, Spika wa bunge la Marekani Nancy Pelosi amewasili nchini Jordan kufanya mazungumzo na Mfalme Abdullah.

Bi Pelosi, ambaye ameandamana na wanasiasa wa ngazi ya juu wa Marekani, amekosoa vikali hatua ya rais Donald Trump kuwaondoa wanajeshi wa nchi hiyo kaskazini mwa Syria.

Vikosi vya Marekani vitafanya nini?

Akiwa safarini kuelekea eneo la mashariki ya kati waziri wa ulinzi wa Marekani, Mark Esper amesema wanajeshi hao watatumiwa "kutoa ulinzi kwa Iraq" na kukabiliana na jaribio la IS kurejea tena nchini humo.

"Marekani inajiondoa taratibu kaskazini mashariki mwa Syria... tunazungumzia wiki chache zijazo, sio siku"alisema.

"Mapango wa sasa ni wa vikosi hivyo kujikita katika ngome maalum magharibi mwa Iraq."

Afisa wa ngazi ya juu wa idara ya ulinzi ya Marekani ameonya kuwa mpango huo huenda ukabadilika ".

Katika Twitter yake, rais Trump alimnukuu Bw. Esper - ambaye alimtaja kama Mark Esperanto - akisema mkataba wa kusitisha mapigano "unaendelea vyema".

Siku ya Alhamizi Uturuki ilikubali kusitisha mashambulizi yake hadi Jumanne usiku, ili kuwapatia nafasi wapiganaji wa Kikurdi kuondoka katika ngome yao.

Wizara ya ulinzi ya Uturuki imeripoti kuwa mwanajeshi mmoja ameuawa na mwingine kujeruhiwa karibu na mji waTal Abyad.

Ilisema kuwa vikosi vya Uturuki vilijibu mashambulizi katika hatua ya kijilinda.

Image caption Ramani inayoonyesha hali halisi ya mzozo wa Syria

Ni nini kinachoendelea Syria?

Baada ya kufikia makubaliano na vikosi vinavyoongozwa na wapiganaji wa Kikurdi, jeshi la Syria lilianza kufanya mashambulizi kuelea mpakani siku ya Jumatatu.

Vyombo vya habari vya Syria vilitangaza kuwa vikosi vya serikali vimeingia katika mji wa Manbij, eneo ambalo Uturuki inataka kubuni "eneo salama".

Wanajeshi wa Uturuki na wapiganaji wanaopinga serikali ya Uturuki walianza kukusanyika karibu na mji huo.

Mkataba huo ulionekana kuimarisha utawala wa rais wa Syria Bashar al-Assad kwani ulimaanisha vikosi vyake vitarejea katika maeneo ya kaskazini mashariki kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2012, baada ya kujiondoa kwao katika maeneo mengine ili kukabiliana na waasi kutoa nafasi kwa wanamgambo wa Kikurdi kuchukua udhibiti wa eneo hilo.

Licha ya kupinga jaribio lao la kutaka kujitenga na kujitawala, Bw. Assad hakupigania kukomboa eneo hilo, hasa baada ya wapiganaji wa Kikurdi kuwa washirika wake katika vikosi vya muungano dhidi ya IS kwa ushirikiano na vikosi vya Marekani.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Uturuki na washirika wake wakiendelea na mashambulizi dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi wanaoshikilia mji wa mpakani kaskazini mashariki mwa Syria

Kando na kupiga vita IS, Wakurdi walikuwa kiungo muhimu kwa Marekani katika hatua ya kudhibiti ushawishi wa mahasimu wao Urusi na Iran katika mzozo wa Syria.

Kwa sasa, vikosi vya Syria havitapelekwa katika miji ya Tal Abyad na Ras al-Ain, ambako Uturuki imeelekeza juhudi zake.

Rais Erdogan wa Uturuki anasisitiza kuwa oparesheni hiyo itaendelea hadi pale inchi hiyo itakapofikia "malengo yake" licha ya kuingiliwa na vikosi vya serikali ya Syria.

"Mungu akitujaalia tutakomboa maeneo yanayokaribia mpaka wetu kutoka Manbij hadi Iraq na kuhakikisha kwamba katika awamu ya kwanza, watu milioni moja wanarudi makwao na katika awamu ya pili wakimbizi milioni mbili wa Syria wanarejea nyumbani kwa hiari," alisema katika hotuba yake kupitia Televisheni siku ya Jumanne .

Umoja wa Mataifa unasema watu takribani 160,000 wametoroka makazi yao lakini shirika kutetea haki la Syrian Observatory (SOHR) linasema idadi hiyo huenda ni zaidi 250,000 huku likiripoti vifo vya raia 70.

Shirika hilo lillilo na makao yake nchini Uingereza pia linasema wanachama 135 wa SDF wameuawa katika oparesheni hiyo kufikia sasapamoja na wapihanaji 122 wanaounga mkono serikali ya Uturuki na wanajeshi wanane wa Uturuki.

Shirika la habari la Uturiki, Anadolu limeripori vifo vya raia 18 katika mpaka wa kusini mwa Uturuki.

Mada zinazohusiana

Maelezo zaidi kuhusu taarifa hii