Zaidi ya makazi 1000 yasombwa na mafuriko mashariki mwa Uganda

Mvua kubwa zinasababisha madhara makubwa sana ya kimazingira

Wakazi walioathiriwa na mafuriko katika wilaya ya Butaleja Mashariki mwa Uganda wameishutumu serikali kwa kuchelewa kupeleka msaada.

Kwa mujibu wa mamlaka za eneo hilo, mamia ya watu wameyaacha makazi yao na bustani zilizombwa na mafuriko kutokana na mvua kubwa.

Gazeti la Monitor la Uganda lilipotembelea maeneo yaliyoathiriwa, waligundua watu wengi wakiwa kwenye hifadhi ya makazi kwenye shule na makanisa.

Waliwaambiwa wanahabari kuwa hawajapokea msaada wowote kutoka kwa serikali tangu siku ya Ijumaa.

Televisheni ya NTV nchini Uganda imeripoti kuwa mafuriko yalileta athari hasa baada ya kupasuka kwa kingo za mto Manafwa.

Miundo mbinu ya usafiri imeharibiwa vibaya.

Bi Hellen Namuhaini, mkazi wa eneo la Doho, amesema nyumba yake imezama majini na vitu vyake kama nguo, ndege na wanyama wa kufugwa walisombwa na maji.

''Mafuriko hayo yalisababishwa na mvua zilizopiga kwa kipindi cha wiki mbili zilizopita, pia imeharibu bustani na mifugo,'' alisema bi Namuhaini.

Baadhi ya waathirika walichukuliwa na ndugu zao kwa ajili ya kuwapa hifadhi huku wengine wakibaki hawana makazi, chakua wala mavazi.

Bwana Abdu Maliki, mwenyekiti wa kijiji cha Muhuyu, ameliambia gazeti la Daily Monitor kuwa hawana msaada.

''Tunapata taabu sana kwenye mafuriko bila msaada. Tunaomba msaada kwa serikali,'' alisema Maliki.

Wakazi walikuwa wanahofu kwa nini serikali imechukua muda mrefu kuwapa msaada. Lakini serikali ya Uganda imeiambia BBC iko kwenye mipango ya kuwasaidia waathirika baada ya tathimini kukamilika lakini hawajasema wataanza lini shughuli hiyo.

Mvua kubwa yanyesha Msumbiji

Mwanamke ajifungua juu ya mti

''Tunahofu kuwa kipindupindu kinaweza kukumba maeneo yetu kwa sababu vyoo vyetu vimesombwa na mafuriko na sasa watu wanajisaidia haja kubwa kwenye maji hayohayo,'' alisema mmoja wa viongozi wa eneo hilo.

Msemaji wa serikali ya wilaya amesema kuwa kamati inaoshughulikia majanga bado inatathimini hali ilivyo na madhara yaliyojitokeza.

Mamlaka zinasema kuwa wanafanya mipango ya kufanya tathmini siku ya Jumatatu ili kupata idadi kamili ya watu walioathiriwa na mafuriko.

Eneo la Butaleja pekee nyumba 650 ziliathiriwa na mvua, na si mara ya kwanza kwa eneo hilo kupata adha ya aina hiyo.

Serikali imesema ilitoa tahadhari kwa wakazi walioathirika.

Mada zinazohusiana