Kwanini maumivu yanaongezeka kwenye unyevu kuliko kwenye baridi

Condensation on a window

Chanzo cha picha, Getty Images

Watu walio na matatizo ya afya ya muda mrefu kama vile ugonjwa wa yabisi kavu au arthritis huenda wakahisi uchungu zaidi katika siku zenye unyevu, utafiti umeashiria.

Ngano za kale zinaashiria kuwa baridi huzidisha maumivu - lakini kuna utafiti kidogo unaothibitisha athari za hali ya hewa.

Na utafiti huu wa Chuo kikuu cha Manchester wa watu 2,500 uliokusanya data kwa kutumia simu za smartphone, umegundua kwamba maumivu yanazidi kuwa mabaya katika siku za joto, na zenye unyevu.

Watafiti wanatumai kuwa matokeo yatasaidia kutoa muelekeo kwa utafiti wa siku za usoni kuhusu kwanini hali inakuwa hivyo.

Ukimskia mtu akisema magoti yanamuuma kwasababu ya hali ya hewa ni jambo la kawaida - kawaida kutokana na baridi. wengine husema wanaweza hata kutabiri hali ya hewa kutokana na maumivu wanayoyapata kwenye viungo vya mwili.

Lakini kufanya utafiti wa kisayansi kuhusu namna aina tofauti za hali ya hewa zinavyoathiri maumivu umekuwa vigumu. Utafiti wa siku za nyuma umekua mdogo au wa muda mrefu.

Katika utafiti huu, ulioitwa 'Cloudy with a Chance of Pain', wanasayansi waliwakusanya watu 2500 wanaougua maumivu ya viungo arthritis, ya kichwa migraine kutoka nchini Uingereza.

Walinakili maumivu waliohisi kila siku, kwa kati ya mwezi mmoja hadi miezi 15, huku simu zao zikinakili hali ya hewa waliko.

Siku za Unyevu na zenye upepo ziliongeza uwezekano wa kuugua maumivu zaidi kuliko kawaida kwa 20%.

Siku za baridi na zenye unyevu pia zilizidisha maumivu.

Lakini hapakuwa na uhusiano wa ujoto pekee au mvua.

'Kutabiri maumivu'

Profesa Will Dixon, mtaalamu wa yabisi kavu kutoka chuo kikuu cha Manchester, aliyeongoza utafiti huo anasema: "Imedhaniwa kuwa hali ya hewa huwaathiri wagonjwa walio na arthritis tangu [tabibu wa jadi wa ugiriki] Hippocrates.

Chanzo cha picha, Getty Images

"Karibu robo tatu za watu wanaoishi na yabisi kavu wanaamini maumivu hutokana na hali ya hewa."

Dixon anasema iwapo watafiti wengine sasa wanaweza "kutazama kwanini unyevu unahusiana maumivu, hilo litafungua milango kwa matibabu mapya".

Na huenda ikawezekana kutengeneza "utabiri wa maumivu" unaoweza kuwaruhusu watu walio na maumivu makali kupanga shughuli zao.