Mashambulio ya Uturuki Syria: Wakurdi waishutumu Uturuki kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha vita

Mazishi yalifanyika siku ya Alhamisi ya wapiganaji watatu wa SDF waliouawa wakipigana karibu na eneo la Ras al- Ain

Chanzo cha picha, AFP

Wapiganaji wa Kikurdi kaskazini mashariki mwa Syria wameshutumu vikosi vya Uturuki na washirika wake walio waasi wa Syria kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha vita ambayo yalisitisha mashambulio ya wiki mbili.

Kiongozi wa muungano wa vikosi vya Syria Mazloum Abdi alisema kwamba kulikuwa na mashambulizi katika eneo la vita karibu na mji wa Ras al-Ain.

Aliwataka wasimamizi wa makubaliano hayo Urusi na Marekani kuwazuia Waturuki.

Hatua hiyo inajiri baada ya Marekani kuondoa vikwazo dhidi ya Uturuki siku tisa baadaye kufuatia hatua yake ya kuwashambulia wapiganaji wa Kikurdi kaskazini mwa Syria kulingana na rais Donald Trump.

Uamuzi wake unajiri baada ya Urusi kukubaliana na Uturuki kuwapeleka wanajeshi ili kuongeza makubaliano ya kusitisha vita katika mpaka wa Syria.

Mashambulio ya Uturuki yalianza baada ya Trump kuondoa wanajeshi wa Marekani kutoka eneo hilo la kaskazini mwa Syria mapema mwezi huu.

''Wawache wengine washiriki katika vita vya mchanga huu uliojaa damu'', rais huyo alisema katika hotuba ya runinga kutoka Ikulu ya Whitehouse.

Alikosolewa sana na Democrats pamoja na Republicans kufuatia hatua hiyo ya ghafla, wakati ambapo Wakurdi waliokuwa wakishambuliwa na Uturuki walikuwa washirika wakubwa wa Marekani katika vita dhidi ya wapiganaji wa Islamic State katika eneo hilo.

Ramani inayoonyesha mzozo wa Syria

Chanzo cha picha, Dinah Gahamanyi

Maelezo ya picha,

Ramani inayoonyesha mzozo wa Syria

Uturuki ilianzisha operesheni dhidi ya wapiganaji wa Kikurdi ambao inawachukulia kama magaidi tarehe 9 Oktoba , siku chache baada ya Marekani kutangaza kuondoka kwa wanajeshi wake.

Je rais Trump alisema nini?

''Vikwazo hivyo vitaondolewa hadi pale kitu kibaya ambacho hatukipendelei kitakapotokea siku ya Jumatano''.

Alisema kwamba Uturuki imemuhakikishia itasitisha mapigano katika eneo hilo na kuweka makubaliano ya hivi majuzi kuwa ya kudumu.

Uturuki inataka kuweka eneo la kilomita 30 la usalama katika mpaka wa Syria na Uturuki mbali na wapiganaji wa Kikurdi.

Inataka kuwapeleka katika eneo hilo takriban wakimbizi milioni 2 wa Syria ambao inawahifadhi.

Wizara ya fedha baadaye ilithibitisha kwamba vikwazo , vilivyowekwa tarehe 14 mwezi Oktoba dhidi ya wizara ya ulinzi na kawi, pamoja na maafisa wakuu watatu vimeondolewa.

Maelezo ya video,

Magari ya kijeshi ya Urusi

Rais Trump alisema siku ya Jumatano kwamba ataweka idadi ndogo ya wanajeshi katika baadhi ya maeneo ili kulinda hifadhi za mafuta.

Pia aliitaka Uturuki kuwalinda wapiganaji wa IS , na kuhakikisha kuwa kundi hilo la Kijihadi halikuteka eneo lolote la Syria.

Afisa mmoja mwandamizi alisema kwamba zaidi ya wafungwa 100 wa IS walikuwa tayari wametoroka katika ghasia hizo tangu Uturuki kuanza mashambulizi na kwamba hawajaonekana.

Uchanganuzi wa Jonathan Marcus

Kulingana na rais Trump , ni diplomasia ya Marekani pekee iliositisha operesheni ya Uturuki nchini Syria na kuweka makubaliano ya kudumu ili kuokoa maisha ya Wakurdi.

''Wengine wataona lengo tofauti , kwamba Urusi na Uturuki waliafikia makubaliano hayo na kwamba mapngo wote huo ulisababishwa na hatua ya Marekani kuwaacha washirika wake wa Kikurdi.

Mkutano huo na vyombo vya habari haukuwa kuhusu ukweli wa kidiplomasia lakini uchaguzi - juhudi za rais Trump kujaribu kubadili mizozo ya kidiplomasi na kuwa ufanisi wa kisiasa.

Anatumai kwamba hatua yake ya kumaliza migogoro isioisha katika eneo la mashariki ya kati itampatia mafanikio upande wake .

Lakini hakutaja kuhusu maslahi ya taifa hilo katika eneo la mashariki ya kati.

Je makubaliano hayo yalikuwa na nini?

Rais Trump alipongeza makubaliano hayo yalioafikiwa kati ya Urusi na Uturuki siku ya Jumanne kama mafanikio makubwa.

Yaliafikiwa wakati wa usitishwaji wa vita na hatua hiyo itavifanya vikiso vya Urusi na Syria kuondoa wapiganaji wa Kikurdi katika eneo la kilomita 30 katika mpaka huo.

Mapema siku ya Jumatano, vikosi vya Urusi vilielekea katika miji miwili iliopo katika mipaka hiyo muhimu ya Kobane na Manbj.

Katika makubaliano hayo , Uturuki itaendelea kudhibiti eneo ililoliteka katika mashambulio ya hivi majuzi kati ya miji ya ras al-Ain na Tal Abyad.

Makubaliano hayo pia yanatoa mipango ya doria za pamoja kati ya Urusi na Uturuki katika mpaka huo kuanzia wiki ijayo.

Mazloum Abdi, kiongozi wa wapiganaji wa Kikurdi alimshukuru bwana Trump katika twitter , na kusema kwamba rais huyo wa Marekani aliahidi kuimarisha uhusiano.

Katika taarifa, SDF ilisema kwamba bwana Abdi pia alimshukuru waziri wa ulinzi nchini Urusi kwa kuwaokoa Wakurdi kutokana na janga hilo.

Je gharama ya mashambulio hayo ni ipi?

Umoja wa mataifa unasema kwamba takriban watu 176,000 ikiwemo watoto 80,000 wameachwa bila makao katika kipindi cha wiki mbili kaskazini mashariki mwa Syria ambako ni nyumbani kwa takriban watu milioni tatu.

Takriban raia 120 wameuawa katika vita hivyo, pamoja na wapiganaji 259 wa Kikurdi, waasi wa Syria 198 wanaoungwa mkono na Uturuki pamoja na wanajeshi saba wa Uturuki kulingana na shirika la haki za kibinadamu la Syria SOHR.

Raia 20 pia wameuawa nchini Uturuki kufuatia mashambulio ya YPG kulingana na maafisa wa Uturuki.