Viongozi wa wakimbizi wa Congo wakana kuichafua sifa ya Rwanda

Mahakamani

Chanzo cha picha, BBC Great Lakes Service

Maelezo ya picha,

Viongozi wa wakimbizi wakana shutuma za kuichafua Rwanda

Viongozi watano wa kundi la wakimbizi wa Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo walio Rwanda wamekana mashtaka ya kuchafua sifa ya nchi hiyo baada ya kuongoza maandamano mwaka jana yaliyosababisha madhara makubwa.

Katika kuyazima maandamani hayo ,vikosi vya Rwanda viliwaua wakimbizi 11 mwezi Februari mwaka 2018 baada ya kuzizunguka ofisi za Umoja wa Mataifa zinazoshughulikia wakimbizi katika eneo la mji wa Kibuye ulio mashariki mwa Rwanda. Wakimbizi hao kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo walikuwa wanaandamana wakipinga kupunguzwa kwa fedha ya msaada.

Maelfu waliondoka kwenye kambi ya Kiziba, ambayo inahifadhi wakimbizi karibu 17,000 kutoka Jamhuri ya Congo, na kuingia maeneo ya mjini.

Maafisa wanasema maandamano yalikua kinyume cha sheria na yalisababisha vurugu wakati waandamanaji walipokabiliana na vikosi vya usalama.

Maelezo ya video,

Uganda: Nchi iliyopata umaarufu kwa sera zake zinazowakaribisha wakimbizi

Maombi Louis, ambaye alikuwa kiongozi wa wakimbizi kwenye kambi hiyo ya Kiziba , alikana mashtaka akisema ilikua haki yao kuandamana kwa kuwa walikuwa hawajapata msaada wao wa kifedha, matibabu na kadi za wakimbizi.

Aliiambia mahakama kuwa walikuwa wageni ambao hawakuwa na nia yeyote ya kisiasa na hivyo hawapaswi kushutumiwa kuharibu sifa ya Rwanda.

Clemence Mukeshimana, ambaye alikuwa msaidizi wa Maombi, amesema mamlaka zinawahusisha na makundi yanayopinga utawala wa Rwanda-na kudai kuwa hiyo ndiyo sababu vikosi vya usalama viliamriwa kutumia risasi kwenye maandamano.

Chanzo cha picha, BBC Great Lakes Service

Maelezo ya picha,

Mauaji yalitokea baada ya waandamanaji kukabiliana na vikosi vya usalama

Alisema waandamanaji walikuwa hawapigani na serikali ya Rwanda na walikuwa wakitaka haki zao kama wakimbizi ziheshimiwe.

Hoja za washukiwa wengine watatu zitasikilizwa tarehe 7 mwezi Novemba.