Wakandarasi Wachina wafanyakazi chini ya usimamizi wa polisi Dar es Salaam

Kivule
Maelezo ya picha,

Eneo la Daraja la Kivule nje kando kando ya jiji la Dar es Salaam

Mamlaka nchini Tanzania zimewakamata wakandarasi raia wa China wanne kwa makosa ya kuzorotesha maendeleo ya mradi uliogharimiwa na serikali jijini Dr es Salaam.

Sasa wakandarasi hao watalazimika kukaa "ndani" na kurauka toka polisi kila siku kwenda kufanya kazi.

Wakandarasi hao waliajiriwa na Kampuni mbili zilizopewa kandarasi na serikali ya Tanzania ya kujenga daraja na sehemu ya barabara baada ya kuharibiwa na mvua kubwa.

Hali hii ilisababisha shughuli za kiuchumi kuzorota au kusimama katika eneo hilo kwa saa kadhaa.

Maelezo ya picha,

Daraja la kivule

Kukamatwa huko kwa wakandarasi kuliamriwa na Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, na kuwa ni ''mfano kwa wengine'' waliopewa majukumu ya namna hiyo na mamlaka,alieleza katibu wake Abubakar Kunenge, akinukuliwa na shirika la habari la Ufaransa.

Bwana Kunenge amesema watu hao ''watakua kwenye kituo kikuu cha polisi na kuamkia huko kwenda kusimamia kazi mpaka pale mkuu wa mkoa atakaporidhika na kasi ya kazi''.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda

Ameongeza kuwa miradi hii ni kwa ajili ya manufaa ya wananchi hivyo ''wale wasioheshimu mikataba hawana nafasi jijini humo.''

Serikali ya Raisi John Pombe Magufuli imekuwa ikifahamika kwa kuchukua hatua mbalimbali kama vile kuvunja au kupitia upya mikataba na makampuni ya kigeni ambayo yamekuwa yakionekana kutotenda haki.