Vikwazo nchini Zimbabwe: Je ni kina nani wanaolengwa ?

Waandamani nchini Zimbabwe wanaonekana walkibeba mabango

Chanzo cha picha, EPA

Ijumaa ilikuwa siku kuu nchini Zimbabwe kuadhimisha siku ya maandamao dhidi ya vikwazo ambavyo serikali inadai ndio vinavyolisababishia taifa hilo matatizo ya kiuchumi.

Hivyobasi ni kwa nini kuna vikwazo na athari yake ni ipi?

Marekani na Muungano wa Ulaya zote zimedai kuendeleza vikwazo vyao vikidai kwamba hakujakuwa na hatua zozote zilizopigwa katika mabadiliko ya kidemokrasi na yale ya haki za kibinadamu mbali na uhuru wa vyombo vya habari.

Vikwazo hivyo vinawalenga watu binafsi pamoja na makampuni.

Vikwazo vya Marekani vya kifedha na usafiri kwa sasa vinawalenga watu 85, akiwemo rais Emmerson Mnangagwa. Kuna makampuni 56 na mashirika ambayo pia yanakabiliwa na vikwazo hivyo.

''Tuna vikwazo dhidi ya watu fulani na mashirika kadhaa... sio dhidi ya taifa la Zimbabwe. Hakuna chochote kinachoweza kusitisha biashara za Marekani nchini Zimbabwe'', alisema naibu waziri wa maswala ya Afrika Tibor Nagy.

Washington inasema kwamba athari za kiuchumi zinalenga mashamba na makampuni yanayomilikiwa na watu hao binafsi.

Marekani pia ilipiga marufuku uuzaji wa silaha nchini Zimbabwe.

Vikwazo vya Muungano wa Ulaya vinalenga watu binafsi ndani ya serikali ya Zimbabwe na washirika wake.

Vikwazo vya usafiri na upigaji tanji wa mali umewekwa pamoja na uuzaji wa zana za kijeshi na vifaa ambavyo vitatumiwa kukandamiza watu.

Vikiwa vimewekwa tangu wakati wa utawala wa rais Robert Mugabe , vikwazo hivyo viliangaziwa upya mapema mwaka huu na vimeongezwa muda hadi februari 2020.

Muungano wa Ulaya unasema kwamba vikwazo hivyo havina athari yoyote kwa uchumi wa taifa hilo.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

Raia wa Zimbabwe wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa mafuta

Hali mbaya ya kiuchumi

Uchumi wa Zimbabwe umekabiliwa na hali mbaya katika kipindi cha miaka michache iliopita huku mfumuko ukikabili sarafu yake na kuifanya kutokuwa na thamani yoyote.

Wakati mwengine mwaka huu Zimbabwe imekabiliwa na mfumuko wa juu pamoja na uhaba mkubwa wa mafuta ya magari , umeme na maji.

Data ya hivi karibu ya kiuchumi inasema kwamba uchumi wa Zimbabwe umekuwa ukishuka kulingana na kiwango cha mapato ya mtu.

Je vikwazo ndio vya kulaumiwa?

Serikali ya Zimbabwe mara kwa mara imekuwa ikilaumu utendaji wa uchumi wake kutokana na vikwazo, na majirani zake kusini mwa Afrika wana wasiwasi jinsi uchumi huo unavyoathiri eneo hilo.

Lakini kuna ushahidi mchache kudai kwamba Marekani na Muungano wa Ulaya ndizo za kulaumiwa kwa matatizo yanayoikumba Zimbabwe.

Marekani inalaumu tatizo hilo kwa kile ambacho afisa mmoja alidai usimamizi mbaya wa kiuchumi.

Muungano wa Ulaya umedai sera mbaya za kiuchumi , marekebisho mabaya ya umiliki wa ardhi, ukame na HIV/Aids kama sababu zinazoathiri uchumi wa taifa hilo.

Data za mwaka 1980 hadi 2015 zinaonyesha kwamba hakuna ushahidi unaoonyesha kwamba vikwazo hivyo vimechangia ajira na umasikini kulingana na Carren Pindiriri, muhadhiri wa idara ya uchumi katika chuo kikuu cha Zimbabwe.

Upande wake serikali ya Zimbabwe inadai kwamba vikwazo vimegharimu mabilioni ya madola.

''Huwezi kusema kwamba vikwazo havina athari vinapolenga makampuni 56 makubwa nchini Zimbabwe. Ni nini kilichosalia''?, alisema katibu wa kudumu katika wizara ya mawasiliano Nick Mangwana.

Wakati Mugabe alipoondolewa madarakani 2017, wataalam wawili wa haki za kibinadamu katika Umoja wa mataifa walitoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo.

Wanasema kwamba vikwazo hivyo haviwezi kusemekana kwamba havina athari ya uchumi wa taifa hilo mbali na kwamba makampuni na watu wanaolengwa wanawakilisha eneo kubwa la uchumi huo.

Uchumi wa Zimbabwe umewekezwa katika sekta fulani , na vikwazo dhidi ya watu wachache ama kampuni vinaweza kuwa na thari mbaya zaidi.