Miché Solomon aligundua ameibiwa kupitia Selfie

Miché (kushoto), akiwa na miaka 21, na dada yake Cassidy Nurse
Maelezo ya picha,

Selfie,iliyopigwa miaka kadhaa baada ya kwanza inaonesha sura za kufanana

Mwezi Aprili mwaka 1997 mwanamke aliyevalia sare za muuguzi alitoka katika hospitali ya Cape Town akiwa amembeba mtoto wa siku tatu kutoka wodi ya kinamama kujifungulia huku mama yake mtoto huyo halisi akiwa amelala.

Miaka 17 baadae, mtoto huyo amegundua ukweli kuhusu yaliyojiri katika maisha yake.

Ilikuwa siku ya kwanza ya mhula katika shule ya upili ya Zwaanswyk mjini Cape Town na mwanzo wa mwaka wa mwisho wa masomo kwa Miché Solomon.

Siku hiyo ya Januari mwaka 2015, Miché aliye na miaka 17aliambiwa na wanafunzi wenzake kuhusu msichana mgeni kwa jina, Cassidy Nurse, ambaye wanafanana kama mapacha, japo ni mdogo wake kwa miaka mitatu

Mwanzoni Miché hakutilia maanani suala hilo.

Lakini wasichana hao wawili walipatana shuleni hapo baadae siku hiyo, na Miché anasema alipatwa na hisia ambayo hakuweza kuielezea.

"Nilihisi kana kwamba namjua," alisema. "Niliingiwa na uoga- Sikuelewa kwanini nilihisi hivyo."

Licha ya tofauti ya miaka, Miché walianza Cassidy kutumia muda mwingi pamoja.

"Ningelisema, 'vipi, mdogo wangu!' Na yeye angelinijibu, 'poa, dada mkubwa!''. "Wakati mwingine ningelienda bafuni naye na kumwambia, 'Naomba nikusaidie kutengeneza nywele zako, wacha nikupake mafuta na kadhalika.'"

Chanzo cha picha, Mpho Lakaje

Maelezo ya picha,

Muonekano wa Miché Solomon leo

Mtu yeyote angeliwauliza Miché na Cassidy kama ni ndugu walijibu kwa mzaha, "Hatujui- pengine katika maisha mengine!"

Halafu siku moja wasichana hao walipiga picha ya selfie nakuwaonesha rafiki zao. Baadhi yao walimuuliza Miché kama hana uhakika aliasiliwa . "Hamna! Wacha mcheza!" alisisitiza.

Baadae Miché na Cassidy walienda nyumbani kuwaonesha jamaa zao picha hiyo.

Lavona, mama yake Miché'ambaye alikuwa akimuita binti yake "Princess" alisema jinsi wasichana hao wawili walivyofanana.

Michael, baba yake Miché', pia aligundua jinsi rafiki ya binti yake alivyofanana na binti yao.

Lakini wazazi wa Cassidy, Celeste na Morne Nurse, waliangalia picha kwa mshangao. Walimwambia Cassidy kuwa wana swali wangelipenda kumuuliza Miché.

Wasichana hao walipokutana tena siku iliyofuata, Cassidy alimuuliza mwezake: "Ulizaliwa Aprili 30 mwaka 1997?"

"Niliuliza, 'mbona? Kwani unanifuatilia Facebook?'" Miché anasema.

Cassidy alimhakikishia Miché kuwa hafanyi hivyo, na kwamba alitaka kujua Miché amezaliwa lini.

Basi Miché akajibu ndio, nilizaliwa Aprili 30 mwaka 1997.

Wiki chache baadae, Miché aliitwa ghafla wakati wa somo la hisabati katika ofisi ya mwalimu mkuu, ambako alipata maafisa wawili wa huduma kwa kijamii wakimsubiri.

Walimhadithia Miché kuhusu kisa cha mtoto wa kike wa siku tatu kwa jina Zephany Nurse, ambaye aliibiwa kutoka hospitali ya Groote Schuur mjini Cape Town miaka 17 iliyopita na amabye hajawahi kuonekana.

Miché aliwasikiliza lakini hakuelewa kwa nini walimwambia kisa hicho.

Baada ya hapo wahudumu hao wa kijamii walimuelezea kuwa kuna ushahidi wa kutosha unaoashiria kuwa Miché huenda ndiye mtoto huyo aliyeibiwa miaka hiyo 17 iliyopita.

Ili kuweka mambo sawa, Miché aliwaelezea maafisa hao kuwa yeye hakuzaliwa katika hospitali ya Groote Schuur - na kuongeza kuwa alizaliwa katika hospitali ya Retreat.

Hayo ndio maelezo yaliandikwa katika cheti chake cha kuzaliwa, alisema. Lakini wahudumu hao walimuelezea kuwa hakuna kumbukumbu zinazothibitisha alizaliwa katika hospitali hiyo.

Maelezo ya picha,

Lavona Solomon kiwa na mtoto mchanga Miché

Licha ya kuhisi huenda hili ni suala ambalo huenda si la kweli, Miché alikubali kufanyiwa uchunguzi wa chembe chembe za vinasaba ,DNA.

"Nilimuamini sasa mama yangu aliyenilea - na kwamba hawezi kunidanganya, hususan kuhusu mimi ni nani na mahali nilikotoka," Miché alisema. "Kwa hivyo mawazo yangu yaliniamhia kuwa uchunguzi huo wa DNA utafeli tu."

Lakini mambo hayakwenda kama alivyotarajia. Matokeo yalipotolewa siku iliyofuata yalithibitisha kuwa Miché Solomon na Zephany Nurse, mtoto aliyeibiwa kutoka hospitali ya Groote Schuur, mwaka 1997, walikua wa mtu mmoja.

"Nilishtuka kupita maelezo," Miché anasema. "Maisha yangu yamebadilika sijui nifanye nini ."

Taarifa za mtoto aliyeibiwa, na ambaye sasa ni msichana mkubwa, kupatikana karibu miongo miwili baadae ziligonga vichwa vya habari nchini Afrika Kusini na ulimwengu mzima hali iliyobadilisha maisha ya Miché' hapo kwa papo.

Aliambiwa kuwa hawezi kurudi nyumbani kwao - na ilikuwa miezi mitatu kabla afikishe umri wa miaka 18 kabla aruhusiwe kufanya maamuzi yake binafsi. Kwa sasa atalazimika kuisha katika nyumba salama.

Baadaye Miché alipata habari kuwa Lavona Solomon, mwanamke aliyekuwa akimjua kama mama yake, amekamatwa.

"Hatua hiyo ilinivunja moyo sana," Miché anakumbuka. "Nataka awe pamoja nami ili nimuulize, 'kwa nini? Ninini kinachoendelea?' Nilipata msongo wa mawazo kila nikifikiria kuwa mimi ni mtoto wa mtu mwingine."

Maelezo ya picha,

Miché akiwa na umri wa miezi minane pamoja na baba yake mlezi Michael

Miché alikuwepo wakati mume wa Lavona, Michael - mtu aliyemfahamu kama baba yake - akihojiwa na piolisi.

Polisi walitaka kujua kama alihusika katika mpango wa wizi wa mtoto .

"Baba yangu alikuwa mtu mpole," Miché anasema. "Lakini ni shujaa wangu. Na hapa kuna huyo mtu anajaribu kumfanya aonekana kama mtoto mdogo, huku baba yangu akisema, 'Hapana, Siwezi kufanya hivyo. Miché ni binti yangu- iweje awe sio binti yangu? Sikuwa sehemu ya mpango huo.'"

Polisi haikupata ushahidi kuwa Michael Solomon alikuwa na ufahamu kuwa Miché amechukuliwa kutoka kwa wazazi wake halisi bila idhini na kumuachilila huru.

Michael anasema kuwa Lavona alikuwa mjamzito.

Inasadikiwa kuwa huenda alidanganya kuhusu ujauzito wake kabla ya kumuiba Zephany Nurse, na kumleta nyumbani kwa madai kuwa amejifungua mtoto.

Na sasa Lavona Solomon yuko kizuizini, akisubiri kufunguliwa mashtaka ya wizi wa mtoto.

Chanzo cha picha, Huisgenoot/Noncedo Mathibela

Maelezo ya picha,

Celeste Nurse (kushoto) na mwanawe wa pili, Cassidy

Japo Celeste na Morne Nurse, walipata watoto wengine watatu, hawakusitisha juhudi za kumtafuta mtoto wao wa kwanza, Zephany, na walikuwa wakisherehekea siku yake ya kuzaliwa kila mwaka - hata baada ya wao kutalakiana.

Lakini mtoto wao aliyepotea alikuwa akilelewa katika mji wa karibu na kwao.

Nyumbani kwa Solomon ni kama kilo mita tano kutoka kwa Nurse- wakati mtoto wao, Miché akicheza nyumba iliyo mkabala na ya Nurse, naye Michael alikuwa akicheza kandanda.

Sasa, maombi ya familia ya Nurse imejibiwa. Miché aliunganishwa na wazazi wake halisi katika kituo cha polisi mbele ya maafisa wahuduma kwa kijamii.

"Walinikumbatia kwa upendo na kuanza kuangua kilio," Miché anasema. Lakini hakujisikia huru..

"Nijiambia, 'Ni vile tu watu hawa wamepitia mengi wakinitafuta, wamepata usumbufu wa kiakili kwa muda mrefu,'" alisema. "Inasikitisha, lakini wajua nini, mimi sikuhisi chochote, Sikuwakosa hata kidogo kwasababu hawakuwa maishani mwangu."

Miché alikabiliwa na msongo mkubwa wa mawazo. Wazazi wake walikuwa na furaha kupita kiasi huku wakijitahidi kufidia muda waliopoteleaa, lakini walikuwa wageni kwake.

Wale aliowapenda kwa upande mwingine- walikua wanapitia wakati mgumu, na mmoja wao akiwa kizuizini.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Lavona Solomon (aliyefunika uso) akiwasili katika mahakama kuu ya Cape Town wakati wa kusikilizwa kwa kesi

Kesi dhi ya Lavona Solomon ilianza kusikilizwa katika mahakama kuu ya Cape Town, mwezi Augosti 2015.

Miché na wazazi wake halisi walifika mahakamani kusikiliza utetezi wa Lavona.

Kesi dhidi ya Lavona Solomon ilianza kusikilizwa katika mahakama kuu ya Cape Town, mwezi Augosti 2015.

Miché na wazazi wake halisi walifika mahakamani kusikiliza ushahidi wa Lavona.

Wakati wote wa kusikilizwa kwa wa kesi yake, Lavona Solomon alisisitiza kuwa hana makosa.

Aliifahamisha mahakama kuwa juhudui zake za mara kadhaa za kupata mtoto‚ziligonga mwamba kutokana na kuharibika kwa ujauzito wake na hatua alizochukuwa kuasili mtoto .

Lavona anasema alipewa mtoto na mwanamke anayefahamika kama Sylvia ambaye alipatia tiba ya mfuko wa uzazi.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha,

Morne Nurse, baba mzazi wa Zephanyakiondoka mahakamani

Sylvia alimwambia Lavona, kuwa mtoto huyo allikuwa msichana mmoja ambaye alitaka mtoto wake aasiliwe. Lakini hapakua na ushahidi wa uwepo wa Sylvia.

Karibu mwongo mmoja baada ya kisa hicho, shahidi aliyekumbuka kumuona mwanamke aliyevalia sarea za muuguzi na ambaye alikuwa amembeba mtoto Zephany wakati Celeste akiwa amelala, alimtambua Lavona Solomon katika foleni ya utambulisho.

Mwaka 2016, Lavona Solomon alipatikana na hatia ya wizi wa mtoto na kuhukumiwa kifungo cha miaka 10 jela.

Baadae mwaka huu, Miché alimtembelea Lavona jela na kupata nafasi ya kuzungumza naye kwa mara ya kwanza tangu maafisa wa huduma kwa jamii walipowasili shuleni.

"Mkutano wa kwanza tulizungumza kupitia dirishani, hatukukaribiana," Miché anasema. "Nilimuona mama yangu akiwa amevalia nguo za wafungwa wanawake, tukio ambalo linivunja moyo sana. Nililia na kulia."

Miché alitaka kujua ukweli, kuhusu kile kilichofanyika siku ambayo Lavona alimchukua kutoka kwa mama yake mzazi hospitalini.

"Nilimwambia, 'Kwa kujua kuwa mimi sio damu yako - kwamba hakika mimi ni mtoto wa mtu mwingine, na kwamba huenda uliniharibia nafasi ya malezi bora na kubadilisha maisha yangu kabisa - nimeumia sana. Naweza vipi kukuamini wakati umenidanganya, mimi mwanao? Umevunja uaminifu wako kwangu. Naomba unieleze ukweli ikiwa unataka kurudisha uhusiano kati yetu.'

Maelezo ya picha,

Michael na binti ya Miché wakielekea kumtembelea Lavona jela

"Alinijibu, 'Siku moja, Nitakwambia.'

"Bado anasisitiza kuwa hakuhusika na kosa hilo, lakini nadhani alifanya hivyo."

Hatahivyo, Miché anasema hana kinyongo.

"Kusamehe ni hatua moja kuelekea uponyaji wa jaraha moyoni," Miché anasema. "Maisha lazima yaendelee. Anajua kuwa nimemsamehe, na pia anajua kuwa bado nampenda."

Sasa ni zaidi ya miaka minne tangu Miché alipogundua ukweli kuhusu maisha yake. Alipofikisha miaka 18 mwisho wa mwezi Aprili mwaka 2015, alitafakari wazo la kurudi kwa wazazi wake halisi lakini akaamua kubadili wazo hilo.

"Wametalakiana, hiyo familia imesambaratika," Miché alisema. "Kwa hiyo niliamua kurudi -kwa baba yangu mlezi Michael, hapo ndipo najihisi kuwa huru na salama,kwasababu ni nyumbani kwetu."

Miché amekuwa akijitahidi kujenga uhusiano na familia yake halisi, japo wakati mwingine aliwachukia kwa kumchukua kutoka kwa "mama" yake.

Bado yeye humtembelea Lavona jela katika eneo la Worcester, karibu kilomita 120 kutoka mahali anapoishi, lakini ni mwendo mrefu kwa gari hasa wakati huu ambao na watoto wake wawili.

Lavona Solomon anatarajiwa kuachiliwa huru katika kipindi cha miaka sita ijayo lakini Miché anasema kuwa wakati mwingine anatamani muda "ungelienda mbio". Bado anaishi na familia yake nyumbani, akimsubiri mama yake arudi nyumbani.

Miché Solomon pia ameamua kutumia jina alilopewa na wazazi wake walezi badala ya lile alilopewa na wazazi wake alipozaliwa.

Licha ya changamoto za kisaikolojia aliyopitia baada ya kugundua mwanamke aliyemlea kwa kweli alimuiba kutoka kwa mama yake mzazi, amekubali kuishi na pande zote mbili za utambulisho wake.

"Kwanza nilimchukia Zephany," Miché anasema.

"Alikuja katika maisha yangu na kuyabadilisha kabisa, tukio ambalo limeniumiza sana baada ya kugundua kilichofanyika miaka 17 iliyopita. Lakini Zephany ni ukweli wa mambo na Miché, msichana wa miaka 17 niliyedhani alikuwa wa uwongo. Kwa hivyo nimeamua kutumia majina yote mawili. Unaweza kuniita Zephany au Miché, yote sawa."

Kisa cha Miché kimeelezewa katika kitabu kwa jina Zephany: Two mothers. One daughter na Joanne Jowell