Trump atangaza kuuawa kwa kiongozi wa IS Abu Bakr al-Baghdadi Syria

Baghdadi addressing crowd in Mosul, 2014

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha,

Ripoti ambazo hazijathibirishwa zinasema Marekani imefanya msako dhidi ya kiongozi wa kundi la Islamic State Abu Bakr al-Baghdadi

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuuawa kwa kiongozi mkimbizi wa wapiganaji wa Islamic State (IS) kaskazini magharibi mwa Syria.

Akizungumza kutoka Ikulu ya White House, bwana Trump amesema Abu Bakr al-Baghdadi alijilipua wakati alipozingirwa na kikosi maalum cha Marekani.

Katika hutuba isioyakawida siku ya Jumapili , Rais Trump alisema Baghdadi alikufa baada ya ya kufika ukingoni alipokuwa akitoroka huko "akilia na kupiga mayowe wakati anafukuzwa na mbwa wa Marekani".

Baghdadi wakati huo alikuwa anatoroka akiandamana na watoto wake watatu wadogo ,lakini hatimae akajilipua kwa bomu alilokuwa amevaa baada ya kugundua kuwa amezingirwa.

Katika mlipuko huo Baghdadi na hao watoto wake wote watatu walifariki papohapo.

Rais Trump alisema japo mwili wa Baghdadi ulikuwa umechanika lakini waliweza kumtambua baada ya kuufanyia uchunguzi.

"Jambazi ambae alijitahidi sana kuwaogofya na kuwahangaisha wengine siku zake za mwisho alionekana mwenye mahangaiko ,taharuki kubwa na kuchanganyikiwa ,alionekana mwenye uoga kupindukia alipogundua kikosi cha Marekani kilikuwa kinamkaribia , Rais Trump alisema.

Baghdadi alipata umaarufu mwaka 2014, alipotangaza kubuniwa kwa "himaya ya Kiislamu" katika maeoneo Iraq na Syria.

Wapiganaji hao walianzisha utawala wa kikatili dhidi ya watu wapatao milioni nane katika maeneo waliokuwa wanayashikilia.

Kundi hilo pia linalaumiwa kwa kufanya mashambulizi kadhaa katika miji mbalimabli duniani.

Kundi hilo la IS linalaumiwa kwa udhalimu pamoja na maovu yaliyosababisha vifo vya maelefu ya watu

Awali Bwana Trump aliandika ujumbe katika Twitter yake akisema: "Kutu kikubwa sana kimefanyika!"

Kiongozi huyo wa IS aliwahi kuripotiwa kimakosa kuwa amefarika siku zilizopita.

Maafisa ambao walinukuliwa na vyombo vya habari kuwa watu wasiojulikana walisema majeshi ya Marekani yanamsaka kiongozi wa kundi la Islamic State katika mkoa wa Idlib, kaskazini mashariki mwa Syria.

Kamanda wa vikosi vya Syria vinavyoongozwa na wapiganaji wa Kikurdi, Mazloum Abdi, siku ya Jumapili alisema kuwa oparesheni hiyo ya "kihistoria ilifaulu" kutokana na "kazi ya pamoja ya kiintelijensia" na Marekani.

Kabla ya tangazo la Rais Trump afisa mmoja wa Marekani aliliambia shirika la habari la Reuters kwamba oparesheni ilifanyika lakini hakutaka kuthibitisha madai kuwa Baghdadi aliuawa.

Maelezo ya picha,

Madai ya msako dhidi ya Abu Bakr al-Baghdadi hayajathibitishwa.

Abu Bakr al-Baghdadi ni nani?

Abu Bakr al-Baghdadi, kiongozi mkimbizi wa wapiganaji wa Islamic State (IS) na uongozi wake wa kidini amewekewa $25m (£19m) na serikali ya Marekani kwa mtu yeyote atakayempata.

Ni mzaliwa wa Samarra, nchini Iraq, mwaka 1971, Jina lake kamili ni Ibrahim Awad al-Badri.

Akiwa mfuasi mkuu wa dini ya Kiislamu tangu akiwa mdogo, baadaye alikuwa amefungwa katika kambi moja ya Marekani kwa jina Bucca 2004 kufuatia uvamizi wa Ufaransa na Marekani.

Akiwa katika kambi hiyo aliweka ushirikiano mzuri na wafungwa wengine wakiwemo maafisa wa zamani wa ujasusi nchini Iraq.

Alijifunza mengi kuhusu jinsi anavyoweza kufanya operesheni zake kutoka kwa maafisa wa kijasusi wa aliyekuwa rais wa Iraq ,Sadaam Hussein.

Usalama wake ni wa hali ya juu ,kutokana na kiwango cha juu cha wasiwasi alionao.

Kiongozi mkuu wa kijihadi

Hii sio mara ya kwanza kiongozi huyo mkimbizi wa IS ameripotiwa kuuawa, lakini wikendi hii maofisa wa Marekaniwamekuwa wakizungumza kwa ujasiri kuhusu oparesheni inayomlenga.

Baghdadi - ambaye alikuwa akitumia jina la siri badala ya jina lake halisi -amekuwa kiongozi kiungo muhimu katika uongozi wa makundi ya kijihadi nchini Iraq na Syria tangu mwaka 2010.

Kabla ya hapo alizuiliwa katika Bucca iliyokuwa ikiendeshwa na Marekani kusini mwa Iraq, ambako alibuni ushirika na wanamgambo wa siku zijazo za IS.

Baada ya Syria kutumbukia katika vita vya wenyewe kwa wenyewe na serikali ya Iraq kuwabagua wa waislamu wa dhehebu la Wasunni walio wachache.

Baghdadi aliunganisha wafuasi wachache wa waliosalia wa al-Qaeda kuwa kikosi cha mapigano ambacho kilifanikiwa kuuteka mji wa Raqqa huko Syria mnamo mwaka 2013 na kisha mji wa pili wa Mosul nchini Iraq mwaka uliofuata.

Kundi lake lililokuwa kikiendesha shughuli zake kwa ukatili mkubwa na ambalo lilidumu kwa miaka mitano liliwavutia maelfu ya wanamgambo wa kijihadiduniani.

Lakini mwezi Machi 2019, lilipoteza sehemu ya mwisho eneo lake katika mji wa Baghuz nchini Syria.

IS imeapa kuendelea na mapigano "ya kuvizia" dhidi ya maadui wake.

Map

Ripoti zinasema alikuwa kiongozi wa kidini katika msikiti mmoja wakati ambapo Marekani iliivamia kijeshi Iraq mwaka 2003.

Baadhi ya watu wanaamini tayari alikuwa mwanamgambo wa kijihadi wakati wa utawala wa kiongozi wa zamani wa Iraq Saddam Hussein.

Wengine wanafikiria huenda aligeuka kuwa mfuasi wa itikadi kali za kidini wakati alipozuiliwa katika kambi ya Bucca, iliyokuwa ikisimamiwa na Marekani kusini mwaka Ira, mahali ambapo makamanda wengi wa kundi la al-Qaeda walizuiliwa .

Alijitokeza tena mwaka 2010 kama kiongozi wa al-Qaeda nchini Iraq, moja ya makundi yalioungana na IS, nakupata umarufu mkubwa wakati wa jaribio la kutaka kuliunganisha na al-Nusra Front nchini Syria.

Wakati huo kundi la IS lilitoa kanda ya video ya mtu aliyedaiwa kuwa Baghdadi mapema mwaka huu.