Mashirika ya haki za binadamu yakemea ukandamizaji wa waandishi wa habari, upinzani na mashirika yasiyo ya kiserikali

Maafisa wa Humanrights Watch na Amnesty International , mjini Nairobi tarehe 28.10.2019
Maelezo ya picha,

Maafisa wa Humanrights Watch na Amnesty International yanaishutumu serikali ya Tanzania kubana uhuru wa waandishi wa habari, kukandamiza upinzani na mashirika yasiyo ya kiserikali

Mashirika ya haki za binadamu Amnesty International na Human Rights Watch yametoa ripoti zinazoishutumu Tanzania kwa kukandamiza waandishi wa habari, watetezi wa haki za binadamu pamoja na vyama vya upinzani, wakidai ukandamizaji huo umeongezeka tangu 2015.

Ripoti hizo mbili tofauti zilizotolewa leo mjini Nairobi zimebainisha kuwa serikali ya Rais John Magufuli imeidhinisha na kutekeleza sheria za ukandamizaji ambazo zinabana uandishi huru wa habari na kuweka sheria kuzuwia shughuli za mashirika yasiyo ya kiserikali na wanasiasa wa upinzani.

Unaweza pia kusoma:

"Huku Rais Magufuli akitarajiwa kutimiza mwaka wanne mamlakani mwezi ujao, hatunabudi kuwa makini kutathmini rekodi ya serikali yake ya unyanyasanyasaji usiojali mfumo wa haki za binadamu ," amessma Roland Ebole, mtafiti wa Amnesty International nchini Tanzania. "Serikali yake inapaswa kuondoa sheria za ukandamizaji zinazotumiwa kuwakamata wapinzani, na kumaliza haraka ukiukaji wa hakiza binadamu na dhuluma ."amesema.

Hali ya waandishi wa habari nchini Tanzania?

Hii ni pamoja na kesi ya mwandishi wa habari maarufu wa habari za uchunguzi Eric Kabendera. Kabendera ambaye amekuwa akiandika taarifa kwa ajili ya vyombo mbali mbali vya habari yakiwemo magazeti ya Times and the Guardian nchini Uingereza mnamo mwezi Julai alikamatwa na kushtakiwa kwa makosa mkiwemo kujihusisha na genge la uhalifu na uhujumu wa uchumi nchini, kukwepa kulipa kodi ya zaidi ya milioni mia moja za kitanzania, ambayo mawakili wake wameyakana wakidai yamechochewa kisiasa . Tangu wakati huo amekuwa gerezani.

Kesi kama vile ile inayomkabili Eric zimesababisha hofu miongoni mwa waandishi wa habari.Wengi miongoni mwa waandishi wa habari waliiambia BBC kuwa wanahofia kufuatilia taarifa zozote zenye utata kwa kuhofia upipizaji kisasi.

Maelezo ya picha,

Waandishi wengi wa habari waliimbia BBC kuwa kesi kama vile inayomkabili Eric zimesababisha hofu miongoni mwa waandishi wa habari

Waandishi wa habari kadhaa wanasema wamekwishawahi kukamatwa pia, kutishiwa na kupigwa na watu wanaoaminiwa kuwa ni maafisa wa usalama wa taifa.

'' Kwangu mimi nina huzuni sana kwamba mafanikio ambayo tulikuwa tumefikia karibu miaka 20 kuhusu uhuru wa mahakama, amani na demokrasia kwa ujumla sasa yanarudishwa nyuma''. Amesema Bi Fatma Karume.

Bi Fatma ambaye ni Wakili na Mwanaharakati wa haki za kiraia nchini Tanzania , ambaye kwa sasa amesimamishwa kazi ya uwakili na mahakama kwa kusema kuwa Rais na Mwanasheria Mkuu wa serikali wamekiuka katiba anailaumu serikali kwa kuidhinisha vipengele vya sheria ambavyo vinazuwia uhuru wa vyombo vya habari na utendaji wa vyama vya kisiasa.

''Walianza na kwa kubadili vifungu vya sheria ya mashirika yasiyo ya kiserikali na vyama vya kisiasa ili kumpatia uwezo msajiri wa vyama vya kisiasa ambaye ndio serikali na hivyo kudhibiti vyama vya kisiasa: '' unaweza kuamini kuwa msajiri wa vyama vya kisiasa anaweza kumfutia mtu chama cheke?'' anaoji Bi Fatma.

Maelezo ya picha,

Mwanasheria na mwanaharakati wa haki za kiraia nchini Tanzania Fatma Karume anasema sheria zimeundwa kubana uhuru wa vyombo vya habari, mashirika yasiyo ya kiserikali na upinzani

Katika mji wa mwambao wa bahari ya Hindi wa Kibiti tulikutana na Ann Pinoni, mke wa mwandishi wa habari wa Tanzania Azory Gwanda ambaye alitoweka November 2017. Kabla ya kutoweka kwake Azory alikuwa akichunguza msururu wa matukio ya kutoweka kwa kwa watu katika eneo hilo . Mke wake alimuona kwa mara ya mwisho akiwa nyuma ya gari jeupe, akiwa na watu wanne. Vyanzo ambavyo havikutaka kutaja majina yao vililiambia Shirika la kulinda waandishi wa habari CPJ kuwa wanaume waliokuwa na Azory walikuwa ni maafisa usalama.

Licha ya shinikizo za makundi ya haki za binadamu kuwataka polisi kuanza uchunguzi rasmi juu ya kutoweka kwa Azory, Mke wa Azory -Pinoni anasema familia bado inahangaika kuelewa ni nini kinachoendelea katika mchakato huo .

" Ninajaribu kuongea lakini sijui hata niongee nini. Sijui la kusema kwasababu wajibu nilionao kwa sasa ni mzito sana kiasi kwamba huwa kila mara nafikiria mume wangu na msaada ambao angekuwa ananipa . Lakini ninaendelea kuhangaika na maisha kwani sina chaguo . Mmoja wa watoto wangu yuko katika chuo cha sheria kwa sasa na ndiye aliyeathiriwa zaidi. Kila wakati Eanapowaona watu wengi wakinitembelea, anafikiri kuwa ninaficha ukweli kwamba baba yake amekufa. Ninajaribu kumliwaza lakini inaniumiza sana."

Maelezo ya picha,

Kabla ya kutoweka kwake Azory Gwanda alikuwa akichunguza msururu wa matukio ya kutoweka kwa kwa watu katika eneo la Kibiti

Mapema mwaka huu, Waziri wa mambo ya nje wa Tanzania aliiambia BBC kuwa Azory alikuwa ni miongoni watu ambao walitoweka na kufa. Hata hivyo baadae alisema katika kauli yake kwamba kauli zake zilieleweka vibaya na kwamba hajui kama Azory alifariki: Palamagamba: 'Azory Gwanda alitoweka na kufariki'

Wakati Magufuli alipoingia madarakani , aliapa kukabiliana ufisadi. Mtindo wake wa uongozi ulimfanya alitwe Tingatinga au Bulldozer. Lakini wakati wa utawala wake, Tanzania imeshuka katika kipimo cha Uhuru wa vyombo vya habari kwa sasa ikiwa nafasi ya 118 kati ya nchi 180.

Msemaji wa serikali Dr Hassan Abbas alipuuzilia mbali shutuma za kudhibiti uhuru wa vyombo vya habari akisisistiza kuwa sheria mpya za vyombo vya habari zilizopitishwa hivi karibuni zinalenga tu kukabiliana na taarifa gushi.

" Ngoja niwakumbushe kuwa kuna sheria mpya hususan kwa mabloga wa mtandao na wale wanaosambaza taarifa gushi, msianze kulalamika kwamba serikali inanyamazisha vyombo vya habari. Kama ukisoma vipengele katika sheria utaona kuwa ni wazi vinazuwia uchapishwaji wa taarifa gushi. Lazima mfuate sheria kwasababu tumekuwa wavumilivu sana kwa muda mrefu . Sasa ninawaonya, Tunaanza kuchukua hatua ."

Lakini afisa wa CPJ Muthoki Mumo anaamini kuwa maagizo haya yenye onyo yanatoka kwa maafisa wa serikali yanaenda kinyume na agenda za Magufuli za awali.

"Ni nani atawawajibisha maafisa ambao hawafanyi kazi yao ipasavyo? ama atakayewajibisha wale wanaokula rushwa ? Ni nani atakayefichua uozo ambao Magufuli anasema anajaribu kukabiliana nao? Unahitaji kuwa na vyombo huru vya habari iki kufikia malengo ambayo serikali imejiwekea yenyewe. Kwa hiyo ni kama serikali inatuma ujumbe tofauti na unaokinzana. Kwa upande mmoja hakuna nafasi ya vyombo huru vya habari na kwa upande mwingine tunataka kuwa serikali ambayo inakabiliana na ufisadi ambayo inafikia mambo haraka na hauwezi kutuma ujumbe wa aina mbili kwa wakati mmoja, kwasababu mambo haya utendaji bora katika serikali, vita dhidi ya rushwa nsa vyombo huru vya havbari ni mambo yanayokwenda pamoja . "

Uchaguzi wa Urais wa Tanzania unatarajiwa kufanyika mwaka ujao, lakini kutokana na upinzani dhaifu na na vyombo vya habari vyenye hofu mambo huenda yasibadilike.