Rais wa Uganda azitaka mahakama kuhakikisha wauaji wananyongwa

"Tutatumia sheria ya Musa ; jicho kwa jicho na jino kwa jino. Mtu yeyote atakayewauwa watu wengine atakufa pia ," Alisema Museveni.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha,

"Tutatumia sheria ya Musa ; jicho kwa jicho na jino kwa jino. Mtu yeyote atakayewauwa watu wengine atakufa pia ," Alisema Museveni.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amekuwa mara kwa mara akizitaka mahakama zihakikishe wauaji wananyongwa ili kumaliza uhalifu nchini nchini Uganda.

Bwana Museveni ambaye amekuwa akitoa kauli hiyo katika mikutano ya hadhara,hivi karibuni ameahidi kukabiliana na mahakama ili kuhakikisha wauaji wananyongwa.

Unaweza pia kusoma:

Wiki mbili zilizopita kiongozi huyo wa Uganda alimuagiza Mkuu wa polisi wa nchi hiyo Meja Jenerali Sabiti Muzeeyi, kuandaa mpango wa kumaliza ongezeko la silaha na ghasia za uhalifu katika mji mkuu wa nchi hiyo Kampala zinazotekelezwa na watu wenye silaha, limeeleza gazeti la the monitor nchini humo.

"Nina vita na mahakama, sitavumilia watu wanaowauwa watu wengine. Yeyote anayewauwa watu wengine atauawa ," Museveni amenukuliwa na vyombo vya habari akisema alipokuwa akizungumza na vijana wanaoishi katika maeno ya mabanda (ghetto) mjini Kampala hivi karibuni.

Chanzo cha picha, Yoweri Museveni /Twitter

Maelezo ya picha,

Rais Museveni alipotembelea aneo la mitaa ya mabanda mjini Kampala (ghetto) ambako visa vya uhalifu vimekithiri

Je agizo la museveni litatekelezwa na mahakama?

Adhabu ya kunyongwa ni moja ya adhabu zinazotolewa na mahakama kwa mujibu wa sheria na katiba ya nchi hiyo, ameiambia BBC Mwanasheria na Mbunge nchini Uganda Asuman Basalirwa.

Hata hivyo amesema uamuzi na mamlaka ya kumnyonga mtu au kutomyonga hutolewa na Jaji wa mahakama, na raisi Museveni hana mamlaka yoyote, wala ushawishi wowote wa kubadili uamuzi wa Mahakama.

''Maneno ya rais Museveni hayawezi kuilazimisha mahakama kubadili maamuzi yake wala kumpatia mtu fulani hukumu ya kunyongwa'' amesisitiza Bwana Basalirwa.

''Kile anachoweza kukifanya ni kutoa msamaha kwa mfungwa au wafungwa kwa misingi ya huruma, jambo analokubaliwa kikatiba'', aliongeza Basalirwa.

Chanzo cha picha, Asuman Basalirwa /Twitter

Maelezo ya picha,

Mwanasheria na Mbunge nchini Uganda Asuman Basalirwa anasema maagizo ya rais Museveni hayawezi kubadili utendaji wa mahakama

Katika magereza nchini Uganda kuna idadi kubwa ya wafungwa ambao tayari wamehukumiwa adhabu ya kifo, lakini adhabu ya kunyongwa haitekelezwi, kutokana na kwamba wengi hwanasita kutoa hukumu hiyo.

Ni kwanini Museveni anataka wauaji wanyongwe?

Visa vya uhalifu katika maeneo ya mitaa ya mabanda ya Najjanankumbi Ndeeba ambako kumekuwa kukiripotiwa visa vya uhalifu wa magenge kama vile lile linaloendesha wizi wa simu na bidhaa nyingine, linalofahamika kama Kifeesi.

Unaweza pia kusoma:

Kundi hilo limekuwa likiripotiwa kuwagonga wapitanjia kwa vyuma na kuwaibia mali zao.

"Tutatumia sheria ya Musa ; jicho kwa jicho na jino kwa jino. Mtu yeyote atakayewauwa watu wengine atakufa pia ," Alisema Museveni.

Wiki mbili zilizopita polisi waliandaa mpango utakaowawezesha kuongeza juhudi zao zaidi katika kuwasaka watu wanaorudia makosa , kuimarisha mawasiliano na Umma na kushughulikia matukio haraka pale yanapotokea.