Human Rights Watch: Yawasilisha malalmishi dhidi ya serikali ya Tanzania kuhusu wakimbizi wa Burundi

TZ imehifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi ukanda wa Afrika Mashariki

Maafisa wa serikali ya Tanzania walidaiwa kuwalazimisha zaidi ya wakimbizi 200 wanaotafuta hifadhi ambao hawakuwa wamesajiliwa, kurudi nchini Burundi mnamo tarehe 15 mwezi Oktoba mwaka huu

Kulingana na shirika la Human Rights Watch maafisa wao walitishia kuwanyima uhalali wao wa kuwepo nchini Tanzania iwapo wangekataa.

Hatahivyo mkimbizi mmoja kutoka Burundi anayeishi nchini Tanzania aliyehojiwa na BBC na ambaye hakutaka jina lake litajwe amesema kwamba awali kulikuwa na taarifa hizo za kulazimishwa kuondoka lakini kwa sasa wakimbizi wamekuwa wakirudi nyumbani kwa hiari yao.

lakini kwa mujibu wa taraifa hiyo ya HRW kurudishwa huko kwa lazima kunafuatia makubaliano ya mwezi Agosti 24 kati ya Tanzania na Burundi ambapo takriban wakimbizi 180,000 wa Burundi nchini Tanzania wanatarajiwa kurudi makwao kwa hiari ama kwa lazima kufikia tarehe 31 Disemba 2019.

Shirika la Umoja wa mataifa kuhusu wakimbizi UNHCR lilitoa msaada wa kuwasajili wanaotafuta hifadhi nchini humo chini ya mpango wake wa kuwasaidia wanaotaka hifadhi, licha ya vitisho kutoka kwa serikali ya Tanzania kwamba wakimbizi hao watakamatwa iwapo watasalia nchini humo.

''Serikali ya Tanzania imeimarisha shinikizo dhidi ya wakimbizi wa Burundi ambao hawajasajiliwa kwa kuwalazimisha kuondoka nchini humo, kitendo ambacho kinakiuka sheria za kibinadamu chini ya sheria ya kimataifa kuhusu haki za kibinadamu'', alisema mkurugenzi wa wakimbizi katika Human Rights Watch.

''Taifa hilo linaonekana linatekeleza tishio lake la kuwatimua wakimbizi 180,000 ambao watakuwa hatarini iwapo watarudi nchini Burundi'', aliongezea.

Mnamo tarehe 11 mwezi Oktoba rais wa Tanzania John Pombe Magufuli alisema kwamba wakimbizi wa Burundi wanapaswa kurudi nyumbani kufikia tarehe 31 mwezi Disemba.

Kupitia taarifa hiyo shirika hilo la haki za kibinadamu sasa limeandikia tume ya haki za kibinadamu ya bara Afrika ikiitaka kuishinikiza nchi hiyo kutowalazimisha wanaotafuta hifadhi kurudi makwao, huku likitoa wito kwa UNHCR kutosaidia katika kuwarudisha nyumbani watu hao.

Chanzo cha picha, STEPHANIE AGLIETTI

Katika makubaliano ya mwezi Machi 2018, Tanzania na Burundi zilikubaliana kuwarudisha nyumbani takriban wakimbizi 2000 kwa wiki chini ya makubaliano yalioafikiwa na pande tatu na UNCHR kusaidia kuondoka kwa hiari kwa wakimbizi wa Burundi.

Hatahivyo kiwango kilichoafikiwa kimekuwa cha chini mno, huku wakimbizi 76,000 wakirudi kati ya wastani wa takriban wakimbizi 730 kwa wiki.

Kulingana na taarifa hiyo kati ya mwezi Julai na Septemba , shirika la UNCHR na mamlaka ya Tanzania walifanya zoezi la ukaguzi ili kubaini idadi ya raia wa Burundi wanaoishi katika kambi za Tanzania ambao walisajiliwa na wale ambao hawajasajiliwa.

Idadi kubwa ya raia wa Burundi wamekabiliwa na vikwazo katika kujisajili, kulingana na vyanzo viwili vilivyo huru ambayo vilizungumza na Human Wrights watch.

Huku mamlaka ikiwa bado haijachapisha matokeo ya zoezi hilo, takriban wakimbizi 3000 wa Burundi ambao hawajasajiliwa walitambuliwa kulingana na chanzo chengine cha HRW.

Taarifa hiyo inasema kwamba mnamo tarehe 11 mwezi Oktoba 2019, usimamizi wa kambi hizo zilizopo chini ya wizara ya maswala ya ndani nchini Tanzania ulisema kwamba mamia ya wakimbizi wa Burundi ambao hawajasajiliwa walikuwa wanaishi katika kambi moja kati ya tatu zilizopo ikiwemo Nduta, Nyarugusu na Mtendali - kaskazini magharibi mwa eneo la Kigoma karibu na mpaka wa Burundi na kwamba iwapo hawakusajiliwa ili kurudi makwao watakuwa wakiishi katika kambi hizo kwa njia isio halali na kwamba huenda watakamatwa kulingana na chanzo chengine.

Wale waliopo katika kambi hizo kinyume na sheria waliambiwa kwamba watapata msaada wa chakula lakini sio usaidizi mwengine.

Human Wright Watch linasema kwamba takriban wakimbizi 200 walilazimishwa kurudi nchini Burundi mnamo tarehe 15 mwezi Oktoba kutokana na shinikizo kali kutoka kwa serikali ya Tanzania.

Imesema kwamba tangu mwezi Agosti maafisa wa Tanzania wameweka na kubadilisha mahitaji ya mara kwa mara ya mashirika ya misaada yanayoendesha operesheni zao katika kambi.

Chanzo cha picha, Alamy

Makubaliano ya hivi majuzi kati ya maafisa wa polisi wa Burundi na wenzano wa Tanzania kulingana na ripoti hiyo , kuruhusu doria za mipakani miongoni mwa maafisa wa mataifa yote mawili imezua hofu ya kukamatwa kwa wakimbizi.

Wakimbizi wa Burundi Tanzania wasema 'wametishiwa kurudishwa nyumbani'

Mnamo mwezi Julai 2019, wakimbizi kutoka Burundi katika kambi moja nchini Tanzania walisema kwamba maafisa wasimamizi katika eneo hilo waliwatishia kuwarudisha kwa lazima nyumbani.

Wakimbizi hao waliambia BBC kwamba hawatokuwa salama iwapo watarudishwa Burundi.

Serikali ya Tanzania imekuwa ikikana kuwa kuna mpango wa kuwarudisha nyumbani wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu iliyo karibu na mpaka na Burundi.

Wakimbizi hao waliezea ya idhaa ya kiswahili BBC katika maziwa makuu kwamba mkuu wa kambi hiyo, aliwataka warudi kwa hiari kabla ys kushurutishwa kurudi nchini humo.

Mkuu huyo alisikika katika kanda ya sauti iliyotumwa kwa BBC na baadhi ya wakimbizi, akiwaomba waondoke kwasababu wanachangia matatizo kwa wakaazi wa eneo hilo.

Mchango wa Tanzania katika kuwahifadhi wakimbizi wa Burundi ni upi?

Zaidi ya wakimbizi 200,000 wa Burundi wanaishia Tanzania, wengi wao wakiwa wametoroka ghasia nchini mwao zilizozuka mnamo 2015.

2018 Serikali ya Tanzania ilisema kuwa inajiondoa katika mpango wa Umoja wa mataifa wa kuwasaidia wakimbizi kuanza maisha mapya katika mataifa yanayowahifadhi.

Tanzania limekuwa eneo salama kwa wakimbizi wengi.

Mwaka 2017 taifa hilo lilisimamisha kwa muda usajili wa wakimbizi wapya na kuwataka wakimbizi wa Burundi kurudi nyumbani, hatua ambayo ilishtumiwa na makundi ya kupigania haki za kibinaadamu.

Shirika la wakimbi la Umoja wa Mataifa UNHCR linasema kuna wakimbizi Laki 2 kutoka Burundi wanapatiwa makazi nchini Tanzania.

Katika idadi kubwa ya watu waliokimbia nchi yao, shirika hilo linaeleza kwamba asilimia 60 ni watoto.

Maelezo ya picha,

TZ imehifadhi wakimbizi wengi zaidi kutoka Burundi ukanda wa Afrika Mashariki

Serikali ya Tanzania imesifiwa kwa kuendelea kubeba mzigo huu mkubwa wa wakimbizi lakini zaidi kwa kukubali kutekeleza mkakati wa kimataifa ujulikanao kama Comprehensive Refugee Response.

Ni mkakati uliolenga kutafuta namna endelevu ya kuwasaidia wakimbizi kupata ulinzi na mahitaji mengine ya msingi ya kibinadamu.

Lakini zaidi katika kutafuta namna ya kuwashirikisha wakimbizi hawa katika shughuli mbali mbali za maendeleo katika nchi wanazokimbilia.